Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hili hapa Jeshi la Samia CCM

Wajumbe wa CCM wakiwa katika Kikao Maalum cha kwanza cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa kwa Mwaka 2023 wkkilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam jana.Picha Ikulu

Muktasari:

  • Ni kipindi ambacho Watanzania wanataka kusikia kauli za matumaini kwa chama hicho, kuhusu hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha ambapo kuanza kwa mikutano ya hadhara kutaibuka hoja mbalimbali zikiwamo za mambo yanayowagusa moja kwa moja wananchi.

Dar es Salaam. Hilo ndilo jeshi jipya la Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kuliita.

Ni jeshi linalokuja kukabiliana na hoja za vyama vya upinzani vilivyoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, baada ya kuzuiwa kwa takribani miaka sita mfululizo.

Ni kipindi ambacho Watanzania wanataka kusikia kauli za matumaini kwa chama hicho, kuhusu hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha ambapo kuanza kwa mikutano ya hadhara kutaibuka hoja mbalimbali zikiwamo za mambo yanayowagusa moja kwa moja wananchi.

Ni kama CCM imeliona hilo na sasa imeunda sekretarieti mpya ya kupambana na hoja za upinzani.

Awali Rais Samia aliwaeleza wanachama wa CCM, kukaa sawa kujibu kwa hoja si kupayuka hoja zitazokuwa zikiibuliwa na wapinzani.

Mabadiliko hayo ya yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia ambapo pamoja na mambo mengine kiliteua sekretarieti mpya ya chama hicho na kujaza nafasi saba za Kamati Kuu.

Katika sekretarieti hiyo iliyotangazwa yenye wajumbe saba, waliosailia kutoka ya awali ni wawili pekee ambao ni Katibu Mkuu, Daniel Chongolo pamoja na Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha, Dk Frank Hawasi.

Mabadiliko hayo yalitangazwa jana ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na Shaka Hamdu Shaka ambaye nafasi yake ya uenezi imechukuliwa na Sophia Mjema ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Shaka aliwataja pia manaibu Katibu wawili, akiwamo Annamringi Macha (Naibu Katibu Mkuu Bara) aliyechukua nafasi ya Christina Mndeme.

Macha amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Pia, amewahi kuwa katibu msaidizi wa CCM kuanzia ngazi za wilaya na baadaye mkoa. Akaja kuwa katibu msaidizi mkuu idara ya uenezi.

Shaka ambaye anabaki na nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu alisema, Mohamed Said Dimwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar akichukua nafasi ya Dk Abdallah Juma Sadalla.

Pia, Mbarouk Nassor Mborouk ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ye Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Kanali mstaafu Ngemela Lubinga

Mwingine ni Issa Haji Ussi ‘Gavu’ aliyeteuliwa kuwa Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni akichukua nafasi ya Mauldine Castico.

Awali, Shaka alisema uteuzi wa kwanza ulikuwa ni wa kuziba nafasi saba za Kamati kuu, ambapo walioteuliwa ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Hassan Wakasovi aambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora na Halima Mamuya (aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa UWT).

Kwa upande wa Zanzibar, walioteuliwa kuziba nafasi hizo ni pamoja na Mohamed Aboud Mohamed, Mhandisi Nasir Ally (mjumbe wa NEC) na Leyla Burhan Ngozi.

Mabadiliko hayo yamekuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu CCM ilipofanya mkutano mkuu jijini Dodoma uliohitimisha uchaguzi wa ndani wa chama hicho ikiwa pamoja na kuchagua viongozi wakuu akiwemo Mwenyekiti Rais Samia na Makamu wake, Abdulrahman Kinana (Bara) na Rais Hussein Mwinyi (Zanzibar).

Katika uchaguzi huo, Shaka aligombea na kushinda nafasi ya ujumbe wa NEC sawa na Sadalla ambao kwa sasa wameondolewa kwenye sekretarieti.

Mabadiliko hayo yamekuja wakati tayari Rais Samia ameshatangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, ambapo amewataka viongozi na makada wa chama hicho kuwa tayari kujibu hoja za vyama vya upinzani.

Rais Samia alitoa ruhusa hiyo Januari 3 katika mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa Ikulu ya Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya mazungumzo ya maridhiano kati ya CCM, Chadema na Serikali.

Tayari baadhi ya vyama vimeshaanza kufanya mikutano ya hadhara ikiwamo CUF iliyofanya jijini Dar es Salaam, huku Chadema ikitangaza kuzindua mikutano yake ifikapo Januari 21.


Uteuzi unamaanisha nini?

Akizungumzia uteuzi huo, Mhadhiri wa Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa siasa, Dk George Kahangwa alisema unalenga kukabiliana na joto la siasa lililopo kwa sasa.

“Tunaiangalia 2025, mikutano imeruhusiwa na hata mapambano ya kisiasa yanayotarajiwa hivi karibuni, aliyewateua anaona hawa wanaweza kuwa watu sahihi.

“Yawezekana ndani ya chama waliowapendekeza, wanawajua kuwa huyu na huyu hatuvuki, lakini na hawa waliokuwepo wameona wanaweza kuwa sahihi eneo fulani’’ alisema Dk Kahangwa na kuongeza:

“Kwa kifupi chama kinajiandaa kwa mwaka 2025 na kwa ajili ya mikutano ya hadhara kwani haitakuwa rahisi na wameona hawa wanafaa.”

Kwa upande wake, mwandishi mkongwe nchini, Absalom Kibanda alisema sekretarieti hiyo imejengwa na mchanganyiko wa watu ambao baadhi ya watu CCM wanakiri kuwa huenda wakakirudisha chama kwenye misingi.

‘‘Kuna watu walikuwa nyuma ya pazia hawaonekani kama Ana Mringi na Gavu. Nimezungumza na wana CCM wanasema CCM imerudi katika misingi,”alisema.

Kibanda aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) aliongeza: ”Ukimwona (Abdulrahman) Kinana pale juu kama Makamu Mwenyekiti, Ana na Gavu utaona wana-CCM wamekipata kile walichokipoteza kwa miaka mitano nyuma. Sasa wamepata CCM inayotoka ndani na kwa mara ya kwanza imepata Katibu wa Itikadi mwanamke.”

Alisema kwa sasa si sahihi kumpima Sophia Mjema lakini ukimfuatilia tangu akiwa mkuu wa wilaya na sasa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, anajua kuzungumza.

“CCM inajua wapiga kura wengi ni wanawake. Wakati Rais anapambana, Sophia Mjema atakuwa na shughuli naye ya kutafuta kura na kwa kuona hilo, limewafanya (CCM) wampandishe wakijua wanawake ni jeshi kubwa,” alisema

Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Consolatha Sulley alisema ni mabadiliko ya kawaida ndani ya chama hicho.

Alifafanua mabadiliko kama hayo hufanyika baada ya sekretarieti kujitathmini na kuona haja ya kuwepo kwake.

“Sekretarieti imejitathmini na wameona kuna haja ya kuwepo mabadiliko, hivyo ikatekeleza na si vinginevyo,” alisema Dk Consolatha.

Mhadhiri huyo alibainisha mabadiliko katika nafasi ya Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi yameendeleza falsafa ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia ya kuwapa nafasi wanawake.


Gavu mguu sawa

Mara baada ya kutangazwa kuteuliwa, Gavu akizungumza na Mwananchi, alisema ameupokea kwa mikono miwili uteuzi huo, kwa kuwa ni fursa adhimu ya kukitumikia chama na Taifa

“Uteuzi huu ni sawa na wa mzazi kwa mwanawe au wa mkubwa kwa mdogo; hakuna ambaye anayeweza kutoufurahia. Nitashirikiana na wenzangu kufikia maendeleo tunayoyatarajia ndani ya chama na Taifa kwa ujumla” alisema.

Alisema anaamini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, CCM itaendelea kung’ara na Tanzania kupiga hatua zaidi.