Hivi hapa vituo vitakavyotoa chanjo ya Uviko-19 nchini

Dar esa salaam. Baada ya taasisi tano zilizo chini ya wizara ya afya kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa chanjo za Johnson & Johnson ni salama kutumika kwa Watanzania, zimeanza kusafirishwa mchana huu katika mikoa 26 kwa ajili ya makundi matatu yaliyopewa kipaumbele wakiwemo watoa huduma za afya, wazee na wenye magonjwa sugu.

Taasisi zilizochunguza chanjo hiyo ni pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu NIMR, Chuo Kikuu cha Sokoine SUA, Muhimbili na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi wakati akizindua ugawaji wa chanjo ya hiyo leo Ijumaa, Julai 30, 2021 katika Bohari ya dawa MSD.

“Serikali kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa, na vyombo vingine, vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa hizi chanjo za Janssen kutoka kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani,” amesema Profesa Makubi.