Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa nondo nne za Chadema 2025

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Mwanza.Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua kampeni yake ya operesheni ‘+255 Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu’ mjini Bukoba Julai 28, 2023, kikiainisha hoja itakazonadi kwa Watanzania kupitia mikutano yake ya hadhara, ikiwa pamoja na mabadiliko ya Katiba kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, viongozi wa Chadema waliohutubia mkutano uliofanyika Uwanja wa Uhuru maarufu kama uwanja wa Mayunga mjini Bukoba, walitaja madai ya Katiba mpya, mkataba wa uwekezaji bandarini, hali ya wananchi na Taifa kiuchumi na matumizi ya rasilimali za Taifa kuwa ajenda kuu za operesheni hiyo itakayosambaa kote nchini.

Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisisitiza msimamo wa chama hicho wa kupatikana Katiba mpya kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ili kuweka mazingira sawa ya kushindana kisiasa kwa vyama vyote.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imeviandikia barua vyama vya siasa na asasi za kiraia kuvitaka kutoa maoni kuiwezesha Serikali kuandika upya Sheria ya Uchaguzi ya Vyama vya Siasa, ikiwa ni ishara ya kujiandaa kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025 bila Katiba mpya. Tatizo la Watanzania siyo sheria ya uchaguzi wala vyama vya siasa, bali ni Katiba,’’ alisema Mnyika.

Alisema katiba iliyopo inampa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kumteua mwenyekiti, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wengine wanaosimamia uchaguzi, jambo linalofanya uwanja wa siasa kutokuwa sawa.

“Sisi tunataka ama Katiba mpya au mabadiliko makubwa ya Katiba ya kuondoa kasoro zote zinazofanya chaguzi zetu zisiwe huru,’’ alisema Mtendaji mkuu huyo wa Chadema, huku akiwasihi Watanzania kuungana kudai Katiba mpya bila kujali itikadi, imani wala maeneo yao ya kijiografia.

Hoja ya Katiba mpya iliungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Chadema - Bara, Tundu Lissu aliyesema Taifa linahitaji Katiba ambayo siyo tu itawadhibiti na kuwawajibisha viongozi, bali pia kulinda mali na rasilimali za Taifa kwa faida na maslahi ya umma bila kujali viongozi walioko madarakani wanatoka chama gani.

Lissu, ambaye ni mwanasheria kitaaluma alisema Katiba iliyopo inawafanya viongozi kugeuka miungu watu kwa kujiwekea kinga inayowalinda wasiwajibishwe na mamlaka yoyote hata kwa makosa ya wazi.

“Kwa hiyo ndugu zangu wana Kagera na Watanzania kwa ujumla, ni jukumu letu kujipanga na kuungana kuzungumza Katiba mpya kila mahali, hata majumbani mwetu,” alisema Lissu.


Mkataba wa Bandari

Huku akionyesha kushangazwa na kitendo cha viongozi wa CCM kutawanyika nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara kuutetea mkataba wa uwekezaji bandarini, Lissu aliwataka viongozi wa Serikali na CCM kuueleza umma namna Taifa itakavyonufaika na mkataba huo badala ya kuwashambulia wanaoukosoa na kutoa mawazo kinzani kuuboresha.

“Taifa letu limeshaingia mikataba kadhaa ya uwekezaji tangu enzi ya uongozi wa Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli, lakini hatujawahi kushuhudia viongozi wa CCM na Serikali wakitawanyika kote nchini kuitetea mikataba hiyo; watueleze huu una nini hadi wanahaha hivyo,” alisema na kuhoji Lissu.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki alikuwa akirejea ziara na mikutano ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu Mkuu, Daniel Chongolo katika mikoa mbalimbali kueleza umma mambo mbalimbali, ikiwemo suala la mkataba wa uwekezaji bandarini.

Hoja ya mkataba wa bandari pia iliibuliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akionya kuwa bila kurekebishwa, mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai utaathiri siyo tu uchumi wa Taifa, bali pia uhuru na ulinzi wa rasilimali za Taifa.

Hali ngumu ya uchumi

Kiongozi huyo upinzani aliushawishi umma wa Watanzania kutumia sanduku la kura kuiwajibisha CCM kwa kushindwa kuboresha uchumi miaka zaidi ya 60 ya uhuru, licha ya wingi wa rasilimali zilizopo.

“Tuna ardhi kubwa yenye rutuba na watu, lakini tumekosa siasa safi na uongozi bora. Tuiwajibishe CCM kwa kuiondoa madarakani,’’ alisema Mbowe.

(Imeandikwa na Saada Amir, Mgongo Kaitira na Damian Masyenene)