Prime
Hoja tano za Serikali kati ya 10 zakataliwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo akiwasilisha bungeni maoni ya kamati hiyo kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imesema kati ya hoja 10 zilizohusu utolewaji wa fedha za maendeleo, wamekubaliana na Serikali kwa hoja tano pekee.
Hoja hizo ni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2022/23 zilizopokelewa kutoka kwenye kamati za kisekta.
Kwa mujibu wa kanuni, Kamati ya Bajeti hukutana na Kamati ya Uongozi na Serikali, kujadili hoja zilizojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo akisoma taarifa ya kamati bungeni jana, alisema baada ya mashauriano baina ya Kamati ya Uongozi na Serikali kati ya hoja 10 zilizopokelewa, kamati ilikubaliana na Serikali kwa hoja tano na zilizosalia Serikali iliomba muda zaidi ili kuzifanyia kazi.
Sillo alizitaja hoja zinazoendelea kufanyiwa kazi na Serikali ni utolewaji wa barua ya muamana kwa Kampuni ya Mbolea ya Taifa, ili iweze kuagiza mbolea kwa wakati kuendana na msimu wa kilimo.
Alisema pia walikubaliana kupitia upya muundo wa kitengo cha kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu pamoja kufanya mabadiliko ya Sheria ya Utakatishaji wa fedha haramu ili kuendana na miundo ya kimataifa.
“Kuongeza fedha za dharura kwa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) ili uweze kufanya ukarabati wa barabara zilizoharibika kutokana na mvua na kupitia upya mgawanyo wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 ili kuongeza fedha kwa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ili kuweza kupima vijiji vingi zaidi,” alisema.
Pia, Sillo alisema kwa kuwa Serikali iliomba muda wa ziada ili kuzifanyia kazi hoja hizo, Kamati ya Bajeti itafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha Serikali inatimiza ahadi zake kwa Kamati ya Uongozi.
Sillo alisema pia kamati ilipokea jumla ya hoja 12 zilizohitaji nyongeza ya fedha ya Sh97.7 bilioni.
“Baada ya mashauriano baina ya Kamati ya Uongozi na Serikali, Kamati ilikubaliana na majibu ya Serikali katika hoja tisa na hoja tatu zilihitaji ufuatiliaji zaidi,” alisema.
Alisema hoja zilizohitaji ufuatiliaji zaidi ni kuongeza fedha kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA).
Nyingine ni mahitaji ya fedha za mishahara kwa watumishi wa Hospitali ya CCBRT na fedha za dharura kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura).
Alisema Kamati ya Bajeti itaendelea kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya mafungu haya na kutoa ushauri kwa Serikali na Bunge kadri itakavyokuwa inawezekana.
Hoja zilizopokelewa
Kuhusu hoja zinazotokana na majadiliano ya Bunge kwenye utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2022/23 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, alisema hoja zilizopelekwa zilikuwa tano.
Sillo alisema hoja hizo zilihhusu uagizaji wa mafuta ghafi ya mchikichi kutoka nje pamoja na uzalishaji wa mafuta ya kula ndani ya nchi.
Alisema hoja nyingine zilikuwa kuongeza fedha za maendeleo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ili kununua helikopta kwa ajili ya kufukuza wanyama pori wakali na waharibifu.
Pia, kufanya mapitio ya mkopo wa mradi wa uboreshaji wa milki ya Ardhi (LTP) wa Dola za Marekani milioni 150 ili kupata fedha zaidi kwa ajili ya upimaji wa ardhi na mipaka ya vijiji.
“Utozaji wa ushuru wa forodha kwa bidhaa ya kitenge pamoja na thamani ya bidhaa hiyo inapofika Bandari ya Dar es Salaam na upungufu wa fedha za kigeni nchini,” alisema.
Kuhusu fedha za kigeni
Katika hatua nyingie kamati hiyo ilipendekeza mambo matano ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo kufanya mapitio ya kodi, ada na tozo ambazo ni kikwazo katika kuongeza mauzo nje ya bidhaa na huduma.
Sillo alisema hilo itasaidia katika kuchochea ukuaji na utolewaji wa huduma zitakazoliingizia Taifa fedha za kigeni.
Alipendekeza pia kuanzisha utaratibu wa kutumia wabia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwenye ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji ili kuchochea skimu za umwagiliaji.
“Hivi sasa mabonde yote ya umwagilia yaliyopo chini ya Tume ya Umwagiliaji yanategemea bajeti ya Serikali. Hatua hii itasaidia kuwa na kilimo cha uhakika kisichotegemea mvua,”alisema.
Alitaja kingine kuwa ni kuimarisha miundombinu ya utalii katika hifadhi za Taifa, mapori tengefu pamoja na malikale ili kuwezesha watalii kufika na kuzuru maeneo hayo.
“Kuchochea mauzo ya dhahabu na makaa ya mawe nje ya nchi na kudhibiti uagizwaji wa bidhaa zisizo za msingi ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni,”alisema huku akiongeza kuwa kamati inaamini mapendekezo hayo yakifanyiwa kazi, tatizo la upungufu wa fedha za kigeni nchini litapungua kwa kiasi kikubwa.