Hoja tatu za DC Makilagi akipinga kukaidi amri ya Mahakama
Muktasari:
- Watuma maombi wanataka mahakama imuite Mkuu wa Wilaya Amina Makilagi aeleze kwa nini amekaidi amri halali iliyotolewa na mahakama.
Mwanza. Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imewasilisha hoja tatu za pingamizi katika shauri linalomkabili Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Amina Makilagi, la kukaidi amri iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuhusu mgogoro wa kanisa.
Hoja hizo za pingamizi katika shauri hilo la kugombea jengo la kanisa, zimewasilishwa leo Ijumaa Januari 26, 2024 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lameck Merumba akisaidiana na wakili, Felician Msethi.
Akisoma hoja hizo mbele ya Jaji Wilbert Chuma, Wakili Melumba amesema kiapo cha mleta maombi hakijitoshelezi kutokana na kutotaja bayana iwapo anayeshtakiwa ni Amina Makilagi au Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana.
“Anayeshtakiwa hafahamiki kisheria alipaswa kusomeka Mkuu wa Wilaya Nyamagana na si Amina N Makilagi kama inavyosomeka kwenye kiapo cha mleta maombi. Hivyo, anayeshtakiwa hatambuliki,” amesema Wakili Melumba.
Wakili huyo ametaja udhaifu mwingine kuwa ni kutooana kwa taarifa zilizoko kwenye wito wa Mahakama na kiapo cha mleta maombi na kuwa uamuzi unaotolewa na DC si utashi binafsi, bali wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kama ilivyoanzishwa na Baraza la Usalama la Taifa.
“Kwa hoja hizo upande wa mjibu maombi tunaona kabisa hakuna ushahidi kwamba DC Nyamagana amekaidi amri ya mahakama, hivyo maombi ya mleta maombi hayana mashiko na tunaomba Mahakama kutoyazingatia,” amesema.
Hata hivyo, Wakili Gibson Ishengoma anayemwakilisha mleta maombi Benson Kitonka, ameieleza mahakama hiyo kuwa kiapo kusomeka ‘Amina N. Makilagi ‘DC Nyamagana,’ ni kosa la kiundishi ambalo Mahakama ina mamlaka ya kutoa nafasi lirekebishwe na kuandikwa jina halisi la mhusika ambaye ni DC Nyamagana.
Kuhusu hoja ya taarifa zilizopo kwenye kiapo cha mleta maombi kutooana na amri ya mahakama, Ishengoma amesema misingi ya kisheria inaruhusu maelezo mengine kufafanuliwa kwa vifungu kama ilivyofanyika katika kiapo cha mteja wake.
“Kiapo cha mleta maombi na samansi haviwezi kutenganishwa, hivyo si lazima samansi kusomeka kama kilivyo kiapo cha mleta maombi, kama inavyoelezwa kwenye Kifungu namba 95 (3) (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, tukiweka hivi vifungu maana yake ni sehemu ya maombi yetu,” amesema Ishengoma.
Wakili huyo ameenda mbali akisema pamoja na kuwa DC Nyamagana ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, mleta maombi anaiomba mahakama imuite kueleza sababu za kukaidi amri halali ya mahakama, bila kujali iwapo uamuzi huo ulitolewa na kamati.
“Amri ya Mahakama haipaswi kudharauliwa na mtu au kamati yoyote, hivyo tunaendelea kuiomba Mahakama yako tukufu itupilie mbali hoja zilizowasilishwa na wakili wa mjibu maombi badala yake DC Nyamagana aitwe mahakamani kujieleza, ikibainika ameidharau Mahakama basi achukuliwe hatua kama mfungwa wa madai,” amesisitiza.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Chuma ameahirisha shauri hilo hadi Februari 5, 2024 litakapoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
“Kwa kawaida huwa tunasikiliza kwanza pingamizi kisha tunatoa uamuzi iwapo pingamizi hilo lina mashiko, kama hoja za pingamizi zina mashiko ina maana zinaenda kumaliza maombi mama (msingi), lakini kama mapingamizi hayamalizi, maana yake tunaendelea kusikiliza maombi mama,” amesema Jaji Chuma.
Maombi ya msingi kwenye shauri hilo, mleta maombi anaiomba mahakama imuite DC Nyamagana ili aeleze kwa nini amekaidi amri halali iliyotolewa na Mahakama ikimtaka kusitisha uamuzi wa kumuondoa mchungaji Kitonka na waumini wake kanisani.
Chanzo cha mgogoro
Katika shauri la msingi, mdai Benson Kitonka, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God Gospel Church International (AGGCI), anaiomba Mahakama kulipatia kanisa hilo haki ya kumiliki jengo la Kanisa lililoko eneo Bugando jijini Mwanza, ambalo kwa sasa linamilikiwa na Kanisa la Evangelical Assemblies of God in Tanzania (EAGT).
Kabla ya kujitenga na kuanzisha Kanisa jipya la AGGCI, Mchungaji Kitonka na baadhi ya waumini wake walikuwa waumini wa Kanisa la EAGT na walikuwa wakifanya ibada zao katika jengo linalogombaniwa sasa.
Baada ya mgogoro na hatimaye baadhi ya wachungaji na waumini kujitenga kwa kuanzisha kanisa jipya, mali na fedha ziliamuliwa kubaki chini ya mamlaka na umiliki wa EAGT, uamuzi unaoungwa mkono na taasisi na ofisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, lakini unaopingwa na upande wa Kanisa la AGGCI kupitia kwa mchungaji Kitonka kupitia shauri hilo mahakamani.
Mchungaji Kitonka anayedai kuwa mmiliki halali wa jengo la kanisa linalogombaniwa, anaiomba Mahakama kutoa amri ya kumruhusu yeye na waumini wake kuendelea kufanya ibada katika jengo hilo hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.
Desemba 20, 2023, Jaji Stanley Kamana wa Mahakama Kuu alitoa amri ya kuitaka Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kutengua uamuzi wa kuwazuia waumini wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo hilo.
Kutokana na amri ya awali kutotekelezwa, waleta maombi kupitia kwa Wakili Gibson Ishengoma wamerejea mahakamani kuomba Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi atengue zuio dhidi ya waumini na viongozi wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo la eneo la Bugando jijini Mwanza.