Hoja ya kusitisha mafao ya kustaafu ya Kenyatta yawasilishwa bungeni

Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Nairobi. Bunge la Kitaifa la Kenya linahitaji kura za walio wengi kusitisha mafao ya kila mwezi na marupurupu mengine ambayo Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta anapata kwa kinachoelezwa kuwa anajihusisha na siasa baada ya kustaafu.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe amewasilisha hoja katika Bunge la Kitaifa leo Jumanne Aprili akitaka Kenyatta anyimwe marupurupu yake ya kustaafu.

Hoja hiyo pia inalenga kusitisha mafao na marupurupu mengine ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga na aliyekuwa Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka.

Hoja hiyo inaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wabunge wanaounga mkono Muungano wa Kenya Kwanza wa Rais William Ruto.

Uamuzi wa kusitisha mafao ya Odinga na Musyoka utaamuliwa na si chini ya nusu ya wabunge, kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Kustaafu (Naibu Rais na Maofisa Walioteuliwa).

Kagombe pia anataka Hazina ya Taifa kurejesha angalau Sh844 milioni ambazo zimelipwa kwa maofisa watatu wa zamani baada ya kuondoka ofisini.

Mbunge huyo wa awamu ya kwanza anawatuhumu watatu hao kwa kujihusisha na siasa kali huku wakiendelea kupokea mafao yao ya kustaafu, jambo ambalo anasema ni kinyume na vifungu vya Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais ya mwaka 2003 na Sheria ya Mafao ya Kustaafu (Naibu Rais na Maofisa Wateule) ya mwaka 2015.

Sheria hizo mbili zinawalazimisha maofisa kama hao wa serikali kuacha siasa ili kuwa na sifa za kupata mafao na marupurupu ya baada ya kustaafu.

“Bunge linaweza kwa hoja iliyoungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili kuazimia kwamba Rais mstaafu au mke wake, kwa kadri itakavyokuwa, hatastahili mafao yoyote au sehemu ya mafao anayostahili kwa mujibu wa sheria hii,” kinaeleza kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais ya mwaka 2003.

Sheria hizo mbili zinaweka misingi sawa ya kukomesha marupurupu hayo.

Bunge la Kitaifa lina wabunge 349, maana yake ni kwamba ili mafao ya Kenyatta yasitishwe, hoja hiyo inahitaji kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya wabunge wote, yaani wabunge 233.

Kwa upande wa Odinga na Musyoka, angalau nusu ya wabunge, yaani wabunge 175 wanalazimika kuunga mkono hoja hiyo.

“Endapo Bunge litapitisha azimio, Rais mstaafu au mwenza wake, hatastahili mafao yoyote chini ya Sheria hii au haki yao ya kupata mafao hayo itapunguzwa kwa mujibu wa azimio hilo," inasomeka sheria hiyo.