Hospital ya rufaa Amana yazindua kitengo cha figo

Kaimu mganga mkuu hospital ya Rufaa ya Amana Dk Fatuma Kibao.
Muktasari:
- Siku ya Figo duniani huadhimishwa kila mwaka siku ya Alhamisi ya pili ya mwezi Machi, tangu mwaka 2006.
Dar es Salaam. Hospital ya rufaa ya Manispaa ya Ilala (Amana), imezindua kitengo maalumu kwa ajili ya kusafisha figo ikiwa ni siku ya maadhimisho ya figo duniani ambao mpaka sasa zaidi ya watu milioni 900 wameripotiwa kuugua kote ulimwenguni.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Kaimu mganga mkuu hospital hiyo Dk Fatuma Kibao, amesema kwa sasa wanaweza kufanya usafishaji wa figo kufuatia kupata machine maalumu kutoka serikalini.
"Napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuwa na utaratibu wa kufanya vipimo vya angalau Mara moja kwa mwaka kwani hii itasaidia kujua magonjwa nyemelezi yakiwemo magonjwa ya Figo," amesema Dk Kibao.
Akizungumzia dalili za ugonjwa wa Figo Daktari bingwa wa Figo, Dk Vincent Mboya, alisema dalili hizo ni pamoja na Kichefuchefu kisichokoma, kuvimba sehemu mbalimbali za mwili na kwikwi ya muda mrefu.
"Hatua za awali za kujinga na ugonjwa huu ni kujua afya yako kwa kufanya vipimo Mara kwa Mara hospitalini, pia kukaa mbali na bihatarishi kama vile Shinikizo la damu lisilotibiwa vizuri pamoja na kisukari.
"Kuna utaratibu wa kawaida wa kila siku ambao unaweza ukafanyika ili kujikinga na magonjwa ya Figo kama vile Kupunguza matumizi ya chumvi mbichi, lakini pia kufanya mazoezi walau Mara tatu kwa wiki," amesema Dk Mboya.
Aidha Dk Mboya amesema kwa asilimia 8 mpaka 16 ya Watanzania wanaugua magonjwa ya figo huku asimilia 10 ya watu wote duniani wakiugua maradhi ya figo.
Naye Ghazal Masudy ambaye ni mmoja kati ya waliojitokeza katika zoezi la kufanya vipimo vya afya katika hospitali hiyo, ameshukuru utaratibu huo kwani alipata fursa ya kuijua afya yake.
"Kujua afya ni jambo la msingi sana, kwani ukipata ugonjwa ni rahisi pia kwa familia na watu wa karibu kupata Matatizo kama hayo," alisema Masudy.
Pia hospital ya Amana ilifanya upimaji wa magonjwa ya Figo kwa siku mbili Machi 8 na 9 ikiwa ni pamoja na kupima magonjwa mengine kama vile shinikizo la damu, Kupima Ini, Macho, Masikio, Pua, saratani na zoezi la uchangiaji damu.
Siku ya Figo duniani ni kampeni ya kimataifa ya uhamasishaji wa afya inayozingatia umuhinmu wa figo na kupunguza athari za ugonjwa ya figo na matatizo yanayohusiana na afya duniani kote.
Siku hii ni mpango wa pamoja wa Jumuiya ya Kimataifa inayohusisha magojwa ya figo (ISN) na Shirikisho la Kimataifa la Figo (IFKF) yenye kusudı la kuongeza ufahamu kuhusu figo.