Huu ndio mwelekeo mpya wa Bajeti

Tuesday February 09 2021
bajetipic

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango maelezo kuhusu mapendekezo ya mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022-2025/26) na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/2022 pamoja na mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 Dodoma jana. Picha na Jonathana Mussa

By Mwandishi Wetu

Dodoma. Serikali imewasilisha bungeni mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 kwamba inatarajia kukusanya na kutumia Sh36.26 trilioni ikiwa na vipaumbele vya ukuaji uchumi, utawala bora na maendeleo ya watu.

Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21 ya Sh34.88 trilioni 34.88.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ambaye hakuwapo bungeni.

Dk Mwigulu alisema ongezeko la asilimia 4 linatokana na mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha malipo ya deni la Serikali.

“Mahitaji ya upandishwaji wa madaraja ya watumishi na ajira mpya; na mahitaji ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks Authority -Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority -Tawa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority -NCAA),” alisema.

Dk Mwigulu alisema mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kuongezeka hadi Sh26.03 trilioni mwaka 2021/22 kutoka makadirio ya Sh24.07 trilioni mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 8.6 katika muda wa kati.

Advertisement

Alisema uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 71.8 ya bajeti ya mwaka 2021/22 hadi asilimia 76.7 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24. Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka hadi Sh21.47 trilioni mwaka 2021/22 kutoka Sh20.14 trilioni mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 7.1 katika muda wa kati.

“Mapato yasiyo ya kodi (yakijumuisha mapato ya halmashauri, mapato ya utalii na mapato mengine yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania) yanakadiriwa kuwa Sh4.56 trilioni mwaka 2021/22 na kuongezeka kufikia Sh5.60 trilioni mwaka 2023/24,” alisema.

Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh2.89 trilioni sawa na asilimia 7.9 ya bajeti yote.

Dk Mwigulu alisema katika kipindi hicho, Serikali inatarajia kukopa Sh4.99 trilioni kutoka soko la ndani.

Alisema kati ya kiasi hicho Sh3.15 trilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Sh1.84 trilioni sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

“Mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa Sh2.35 trilioni mwaka 2021/22. Matumizi ya Serikali yanakadiriwa kufikia Sh36.26 trilioni ambapo Sh23.0 trilioni 23.0 ni matumizi ya kawaida na Sh13.26 trilioni ni matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.

“Matumizi ya kawaida yanajumuisha mishahara Sh8.15 trilioni (sawa na asilimia 31.3 ya makadirio ya mapato ya ndani), malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje Sh8.88 trilioni na matumizi mengineyo Sh5.97 trilioni.

“Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha Sh10.37 trilioni fedha za ndani na Sh2.89 trilioni fedha za nje,” alisema.

Alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo yamezingatia kukamilika kwa miradi mbalimbali kama vile maboma ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya ambayo yanahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji.

Dk Mwigulu alisema mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22 umeainisha maelekezo mbalimbali ambayo maofisa masuuli watatakiwa kuyazingatia wakati wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa.

Alisema maofisa masuuli watatakiwa kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye mwongozo na kusimamia Sheria ya Bajeti, Sura 439 na kanuni zake.

Dk Mwigulu alisema shabaha na malengo ya uchumi yatakayozingatiwa katika muda wa kati ni kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2021 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.3 ifikapo mwaka 2023.

Alisema pia kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 -5.0 katika muda wa kati.

Maoni ya kamati

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Sillo Baran alitoa maoni ya kamati yake kuwa Serikali iendelee kutoa kipaumbele stahiki katika nishati mbadala kama vile joto ardhi, umeme wa upepo na umeme wa juaili ili kuboresha uzalishaji na usambazaji wa nishati nchini.

Alisema pia Serikali itatue haraka changamoto ya bei na kuchelewa kufika kwa pembejeo za kilimo katika maeneo mbalimbali, upatikanaji wa mbegu bora za mazao nchini na kuandaa ramani itakayoonyesha ni mazao yanayoweza kustawi katika kila wilaya nchini.

“Serikali iainishe mkakati wa kutafuta masoko ya mazao nje ya nchi kwa kuingia mikataba na wanunuzi au nchi ili ziweze kununua mazao yetu. Balozi zetu ziongeze kasi katika utafutaji wa masoko ya mazao yanayolimwa hapa nchini na kuuzwa nchi za nje.

Imeandikwa na Noor Shija, Mwananchi

[email protected]

Advertisement