Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu ndio mzizi tatizo la nguvu za kiume

Muktasari:

  • Msongo wa mawazo, kutofanya mazoezi, matumizi ya vyakula visivyo na virutubisho ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia upungufu wa nguvu za kiume.

Msongo wa mawazo, kutofanya mazoezi, matumizi ya vyakula visivyo na virutubisho ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia upungufu wa nguvu za kiume.

Tatizo hilo hivi sasa limekuwa gumzo katika jamii kutokana na athari zinazojitokeza kila kukicha, ikiwemo wanandoa, wapenzi na familia kuparaganyika.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya na saikolojia, tatizo hilo miaka ya nyuma halikuwa gumzo kwa kile kinachodaiwa watu walikuwa wakitumia vyakula vya asili vilivyoimarisha miili yao.

Hata hivyo katika siku za hivi karibuni biashara ya virutubisho na vyakula vinavyodaiwa kuongeza nguvu za kiume zimeshamiri na baadhi ya watu wanaozifanya au kutengeneza virutubisho hivyo hawana taaluma ya utabibu.

Kwenye baa, vijiwe vya kahawa, barabarani na maeneo tofauti tofauti baadhi ya watu wamejizolea umaarufu kwa kuuza au kuelezea ufanisi wa virutubisho na vyakula husika.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo upungufu wa nguvu za kiume ulitajwa kuathiri watu wenye umri mkubwa, hivi sasa tatizo hilo linawakabili vijana.

Baadhi ya vijana wanakabiliana na tatizo hilo kwa kusaka tiba tofauti mitaani badala ya kwenda kwa wataalamu wa afya kujua chanzo na njia za kutatua tatizo hilo.

Wapo wanaojikita kula na kunywa mchuzi wa pweza, alkasusu, mihogo mibichi, karanga mbichi na nazi, huku wengine wamezama kwenye tiba asili ili kukabiliana na tatizo hilo.

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili anasema vyakula hivyo na baadhi ya samaki wa baharini husaidia kuongeza homoni za kiume lakini si nguvu za kiume.

“Ni vizuri kutumia vyakula kama mihogo, nazi na karanga mbichi endapo mtu anakuwa na afya njema… hivyo vinasaidia, lakini ukishakuwa na tatizo ambalo linakutokea mara kwa mara, hata ukila mihogo haiwezi kusaidia. Ni vema kwenda hospitali kubaini chanzo cha tatizo,” anasema.

Pia anasema vyakula vya baharini kama pweza, ngisi huwa na virutubisho ambavyo husaidia kutanua mishipa ya damu, hivyo kuongeza mzunguko wa damu.

Alipoulizwa kuhusu matumizi ya vinywaji vikali kuchanganya na baadhi ya vile vyenye cafein, Dk Mashili anasema haisaidii kama inavyoelezwa bali huongeza nguvu kwa ujumla wake.

Hata hivyo, kwa baadhi ya wanaume wanaotumia dawa za kupaka ikiwemo vumbi la ‘mkongo’ na nyingine maarufu viksi wanatoa sababu anuai kama asemavyo Herman Julius.

“Vumbi la mkongo au viksi wengi tunanunua kwa malengo ya kuondoa hisia ili ufanye tendo kwa muda mrefu kwa maana wengi tunamaliza haraka.

“Wanawake wanatudharau na hiyo inatufanya wengi tuingie kwenye alkasusu, viagra na dawa nyingine ili tuweze kudumu katika tendo kwa muda mrefu.”

Katika hili Dk Mashili anasema, “Sina uhakika kama anayetumia atapata madhara, lakini sidhani kama anapata hisia vizuri kwa sababu zile dawa zinamfanya anapata ganzi, inamfanya asifikie mshindo mapema kuna uwezekano mkubwa hawezi kufurahia. Pia wataalamu tuna wasiwasi na afya ya mwanamke.”

Mtaalamu huyo wa afya anasema tatizo la nguvu za kiume linachangiwa na sababu kuu mbili; za kiafvya na kisaikolojia na kwamba halitokei kwa siku moja.

Anasema tatizo hilo hutokana na mtiririko wa mtindo wa maisha ambao mwanaume anao tangu akiwa kijana mdogo.

Anasema ili nguvu za kiume zipatikane, mwanaume anatakiwa kutokuwa na hitilafu yoyote katika mfumo wake wa damu, pamoja na magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu.

Dk Mashili anasema ubongo unahusika katika tendo hilo, lakini kikubwa ni vichocheo ‘homoni ya kiume’ ambazo huongezeka zaidi nyakati za asubuhi.

“Kwenye uume kuna mishipa mikubwa ya damu, halafu wenyewe upo kama sponji, hivyo mwanaume anavyojengeka kisaikojia kuwa tayari kwa lile tendo, damu hutoka katika maeneo mengine ya mwili na kushuka chini, damu ikienda katika uume hushibisha ile mishipa inatanuka, uume hurefuka na kunenepa na ndipo nguvu za kiume hutokea,” anasema.

Anasema wanaume wenye magonjwa kama kisukari, presha ya kupanda na mengine hupunguza uwezo wa nguvu za kiume na kupunguza uwezo wa kuzalisha mbegu za kiume zenye nguvu na afya.

Anaeleza kuwa madhara hayo hayaishii katika nguvu za kiume pekee, bali huweza kusababisha hitilafu katika uwezo wa mbegu za kiume kuzalisha.

“Upungufu wa mbegu za kiume kitaalamu tunaita ‘Oligospermia’ na mbegu kutokuwepo kabisa inaitwa ‘azoospermia’.

Suala la kutengeneza mbegu za kiume huratibiwa na mfumo wa fahamu, mfumo wa homoni na mfumo wa uzazi kwa ujumla, ili mwanaume azalishe mbegu zinazofaa, ni lazima mifumo hiyo ifanye kazi kwa karibu,” anasema.

Mtaalamu huyo wa afya anasema ikiwa moja ya mfumo huo utaathiriwa kwa namna yoyote ile, uzalishaji wa mbegu za kiume huweza kupungua au kutokuwapo kabisa.

Anasema kukosa nguvu za kiume na kuathiri uzalishaji wa mbegu kwa wingi, pia husababishwa na unene na vitambi, msongo wa mawazo, joto kali hasa sehemu za uume.


Madhara ya dawa

Matumizi ya dawa mbalimbali za kutibu tatizo la nguvu za kiume bila ushauri wa daktari, zimeelezwa kuchochea zaidi tatizo hilo tofauti na matarajio ya watumiaji.

Daktari kutoka Kituo cha Elimu na Tiba, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Shindo Kilawa anasema tabia ya unywaji wa dawa kama viagra na kuvamia kila kitu kinachodaiwa kuongeza nguvu hizo, ni kichocheo cha kuongezeka kwake.

Anasema matumizi hayo yamewafanya wanaume wengi kupoteza kwa kiwango kikubwa uwezo wao, licha ya kuwa lingetibika kirahisi kama angekwenda hospitali au kwa wataalamu wa afya.

“Wanotumia dawa bila ushauri wanaongeza tatizo badala ya kupunguza kwa sababu chanzo cha tatizo wanakuwa hawajakiondoa,” anasema Dk Kilawa.

Akizungumzia viagra, anasema kabla mtu hajatumia anatakiwa kupata ushauri wa daktari na kueleza kuwa mara nyingi hutolewa kwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea kwasababu ukishaanza kutumia kuna uwezekano hutaweza kuwa na nguvu mpaka uzitumie.

Anasema wataalamu waliweka umri huo kwa kuwa kawaida mwanaume mwenye umri mkubwa kiwango cha homoni ya kiume hupungua mwilini.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Dk Kilawa anasema, “Wanaume wanapaswa kuacha matumizi ya pombe, sigara na kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika. Wajiepushe na tabia hatarishi zinazoweza kumletea magonjwa ya zinaa na mengine yanayoweza kuathiri mifumo hiyo ya uzalishaji.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba, Mloganzila (MAMC), Deogratius Mahenda anasema, “Wanaume wengi akiona jogoo hapandi mtungi anakimbilia viagra, dawa za mitishamba anabugia bila kupima, hilo limewafanya wengi hata nguvu za awali kupotea kabisa.”

Anasema tatizo hilo linaweza kuisha baada ya uchunguzi wa maabara na mgonjwa kupatiwa tiba. “Tunatoa vipimo vya aina mbalimbali lakini pia tiba ya saikolojia na wengi wanapata usaidizi, kwani asilimia 90 ya wanaokuja ni tatizo la kisaikolojia.”

Anasema pia wanatoa dawa za kusisimua misuli kulingana na tatizo la mgonjwa na kwamba zipo za vidonge na sindano. “Mgonjwa anashauriwa namna ya kutumia na sindano anaelekezwa namna ya kujichoma na inachomwa kwenye uume,” anaeleza.

Dk Mahenda anaeleza matumizi ya dawa asili wapo ambao haisaidii, wakiwemo wenye ugonjwa wa U.T.I, pingili za mgongo na selimundu.


Tiba lishe

Kuna makundi ya vyakula ambavyo mwanaume anapaswa kula tangu akiwa mdogo ili kulinda nguvu zake na vipo vya kuepukwa kama wanavyoshauri wataalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Theresia Thomas na Job Mbwilo.

Ofisa Lishe, Theresia anasema ulaji wa protini, matunda na mlo kamili ndiyo dawa pekee ya kuhimili nguvu kwa mwanaume yeyote.

“Ulaji wa samaki, kuku na nyama kiasi husaidia, kwani kuna chembechembe za asidi ambazo husaidia utendaji kazi wa mwili na kuimarisha mishipa ya damu, ila isizidi sana ikaleta mafuta mwilini. Mazao ya samaki, ikiwemo pweza, ngisi na mengineyo husaidia pia.”

Anayataja matunda kama tikiti maji na parachichi ambayo yana folic asid na nishati mwilini na berries ambazo huwezesha msukumo wa damu mwilini.

Pia anataja mbogamboga kama broccoli, spinach na kabichi pamoja na nafaka za karanga, korosho ambazo huleta pia nishati mwilini na mbegu za maboga, bila kusahau viungo kama vitunguu swaumu, pilipili, kungu na mdalasini ambazo hufanya kazi ya kuamsha hisia.

Ofisa Lishe, Job Mbwilo anaitaja chocolate nyeusi kuwa husaidia kuamsha hisia za mtu katika kufanya tendo na husaidia pia kusukuma damu kwenda maeneo husika, lakini mwanaume anatakiwa kula vizuri na kushiba kabla ya tendo.