Huu ndio uchaguzi uliobeba taswira mbaya tangu Uhuru

Mgombea ubunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema, Halima Mdee akiwa na wafuasi wa chama hicho wakionyesha wakionyesha begi waliodai lina kura feki walizozikamata wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2022. Picha na maktaba

Muktasari:

Uchaguzi Mkuu wa 2020 ndio unatajwa kuwa mbaya kuliko chaguzi zote tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kutokana na idadi kubwa ya wapinzani kuondolewa, kunyimwa fomu na matokeo kutangazwa tofauti

Kama kuna uchaguzi ambao umepewa kila sifa ya ubaya tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1992, ni ule wa mwaka 2020, huku kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akisema ulikuwa na mazingira yaleyale ya mwishoni mwa miaka ya tisini.

Wagombea walijikuta katika mazingira magumu ya kurejesha fomu, na waliofanikiwa walikatwa majina yao kutokana na kasoro, baadhi ya mikutano kudhibitiwa, mawakala kutoruhusiwa kuingia vituoni, pia taasisi za kiraia kuwekewa mazingira magumu ya kufanya kazi.

Kifungu cha 2(b) cha sheria hiyo mpya, Sura 337, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 3 (2019), inakataza asasi za kidini kujishughulisha na shughuli za kisiasa. Hali hii iliinyima REDET/TEMCO michango ya watazamaji hawa wazoefu kutoka asasi za kidini.

Hali kadhalika, mitandao ya kijamii ambayo imekuwa nyenzo kuu ya mawasiliano, haikuwa ikifanya kazi vizuri kipindi cha uchaguzi. Kulikuwa na madai kuwa kuanzia Oktoba 27, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifunga tovuti kadhaa maarufu za mitandao ya kijamii ili kudhibiti mawasiliano.

Mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alikuwa amekwenda Ubelgiji kutibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, alirudi nchini kugombea urais lakini akalazimika kukimbia nchi mara tu baada ya matokeo, akifuatiwa na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Mafanikio ya upinzani katika chaguzi tano zilizotangulia kabla ya 2020 yaliwapa matumaini kuwa wangeongeza idadi yao bungeni na hivyo kuwa na nguvu zaidi katika utungaji sheria, lakini matokeo yakawa tofauti na matarajio yao baada ya kufanya vibaya kuliko wakati mwingine wowote.

“Ulikuwa ni uchaguzi wenye mazingira sawa na kabla ya mwaka 1990,” alisema Zitto katika mahojiano na Mwananchi kuhusu miaka 30 ya demokrasia, akimaanisha kabla ya nchi kuamua kurudisha mfumo wa vyama vingi.

“Haki zote za msingi zilizokuwa zimepatikana, ziliondolewa. Kisheria tulikuwa na mfumo wa vyama vingi, lakini practically ilikuwa chama kimoja.”

Zitto alisema uchaguzi huo ulitanguliwa na matukio ya dola kuamua kuichukua demokrasia kama kugeuza wakurugenzi wa wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati ni makada wa CCM na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara.

Kadhia ya mawakala pia ilimkuta, Lema, ambaye aliongoza jimbo la Arusha Mjini kwa vipindi viwili akiwa na Chadema.

“Mimi sikuwa na mawakala vituoni. Mawakala wangu wote walikataliwa kuingia vituoni,” alisema Lema, mmoja wa wabunge waliokuwa wakishinda kwa kura nyingi.

Hata kabla ya uchaguzi, zilishaanza kampeni za kuonyesha hakukuwa na umuhimu wa uchaguzi wa rais kwa madai kuwa John Magufuli alikuwa anakubalika.

Wagombea 15 wa urais walijitokeza mwaka 2020 kupambana na Rais Magufuli ambaye alikuwa akiwania kipindi cha pili. Hii ni idadi kubwa kuwahi kutokea katika historia ya uchaguzi katika Tanzania.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kulikuwa na wagombea wanane pekee, 2010 walikuwa saba na ule wa mwaka 2005 ulikuwa na wagombea 10 wa urais.

Mbali na Dk Magufuli na Tundu Lissu, wengine waliogombea kiti hicho cha rais ni pamoja na Bernard Membe wa ACT (kura 81,129), Leopord Mahona wa NRA (kura 80,787), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (72,885), John Shibuda wa TDA (33,086), Hashim Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma (32,878) na Yeremia Maganja wa NCCR–Mageuzi (19,969).

Wengine ni Muttamwega Mgaywa (Sauti ya Umma), Cecilia Mwanga (ADP), Philipo Fumbo (DP), Queen Sendiga (ADC), Twalib Kadege (UPDP), Seif Maalim Seif (Alliance for African Farmers Party) na Khalfan Mohammed Mazrui (UMD) ambaye alipata kura 3,721.

Wakati wa kampeni, kulikuwa na changamoto kadhaa, lakini baadaye zikatatuliwa na kuendelea bila ya matatizo.

Rais Magufuli alikuwa akimaliza kampeni zake mapema, huku akitumia muda mwingi kuelezea atakayotekeleza katika ilani ya uchaguzi ya CCM iliyokuwa na kurasa 303.

Hali ilikuwa tofauti kwa mgombea urais wa Chadema. Lissu alishindwa kutumia helikopta ambayo Chadema ilipanga aitumie baada ya mamlaka ya usafiri wa anga kuizuia kampuni inayokodisha ndege kutokana na matakwa ya kikanuni.

Hata hivyo, mwanasheria huyo alimudu kwenda sehemu kadhaa nchini, akiungwa mkono na ACT-Wazalendo, ambayo mgombea wake wa urais, Bernard Membe aliishia njiani baada ya kuonekana mara chache kwenye kampeni.

Chadema na ACT-Wazalendo pia waligawana baadhi ya majimbo.

Rais Magufuli alitetea nafasi yake baada ya kushinda kwa kishindo uchaguzi huo kwa kupata kura milioni 12.5 ambayo ni asilimia 84 ya kura zote, wakati Lissu alishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 1.9.

Kabla na baada ya matokeo kutangazwa, kulikuwa na manung’uniko mengi dhidi ya mwenendo wa uchaguzi.

Manung’uniko haya yalitoka ndani na ya nje ya nchi. Vyama vikubwa vya upinzani vilikataa matokeo, vikisema uchaguzi ulivurugwa, haukuwa huru na wa haki.

Hadi sasa Chadema imekataa kutambua matokeo hayo na hivyo haichukui hata ruzuku zinazotokana na ushiriki wao katika uchaguzi, huku kikiwa na mzozo wa wanachama 19 walioenda bungeni kwa madai kuwa wameidhinishwa kuwa wabunge wa viti maalumu, suala ambalo hadi sasa liko mahakamani baada ya chama hicho kukana kupeleka barua.

Jumla ya watu milioni 15.0 walipiga kura wakati waliojiandikisha walikuwa milioni 29.75 kwa mujibu wa NEC.

“Voters turnout (kujitokeza kwa wapigakura) ilishuka mwaka 2020. Hata vijana waliojitokeza walikuwa wachache. Ni asilimia 12 tu ya vijana ndio waliojitokeza,” alisema Zitto.

“Hii inatia wasiwasi wa kurejea katika hali iliyokuwepo kabla ya 1990.”

ACT-Wazalendo ilikwenda mbali zaidi baada ya kupeleka malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).

Chama cha wananchi CUF, pamoja na kunung’unikia mchakato wa Uchaguzi na matokeo, kilijiapiza kutoshiriki tena uchaguzi wowote wa nchi hiyo, mpaka pale itakapoundwa tume huru ya Uchaguzi.

Mwenendo na matokeo ya uchaguzi huo yanaonekana kuamsha kilio cha tume huru ya uchaguzi, na hasa katiba mpya, kitu ambacho CCM imesharidhia lakini haijatoa mwelekeo wa jinsi mchakato huo utakavyofanyika.

Wako wanaotaka mchakato uendelee ulipoishia, yaani kupiga kura ya maoni kuridhia Katiba Iliyopendekezwa, na wako wanaotaka mchakato uanzie katika Rasimu ya Katiba, wakiamini iliwekwa kando katika mjadala wa Bunge la Katiba.

Nyongeza na Angetile Osiah