Huyu ndiye Machumu mkurugenzi mtendaji MCL

Huyu ndiye Machumu mkurugenzi mtendaji MCL

Muktasari:

  • Baada ya kudumu kwa miaka 17 ndani ya kampuni, Bakari Machumu ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miezi sita tangu alipoondoka Francis Nanai.


Dar es Salaam. Baada ya kudumu kwa miaka 17 ndani ya kampuni, Bakari Machumu ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miezi sita tangu alipoondoka Francis Nanai.

Uteuzi wa Machumu, ambaye alikuwa akiikaimu nafasi hiyo kwa kipindi chote hicho baada ya kuondoka Nanai ulitangazwa jana na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Nation Media Group (NMG), Stephen Gitagama.

Katika taarifa hiyo ya uteuzi, Gitagama alisema majukumu hayo mapya kwa Machumu yanaanza kesho, Mei mosi na atakuwa akiripoti kwake.

“Machumu amekuwa ndani ya kampuni tangu mwaka 2004 alipojiunga na MCL kama mhariri wa biashara wa gazeti la The Citizen na miaka miwili baadaye akawa mhariri mtendaji wa gazeti hilo na mwaka 2012 aliteuliwa kuwa mhariri mtendaji mkuu wa MCL,” inasema taarifa hiyo.

Gitagama aliongeza kuwa “katika kipindi hicho alikuwa kiungo muhimu katika kufanikisha mapinduzi ya kidijitali ndani ya MCL na kuifanya kuwa chumba cha habari cha kwanza Tanzania kuwa na muunganiko wa magazeti na vyombo vya kidijitali (convergence) mwaka 2017.”

Akiwa mkurugenzi mtendaji, alisema atakuwa na jukumu la kuiongoza MCL kwa ujumla, kuandaa mikakati ya ajenda na jitihada za kuendeleza mapinduzi ya dijitali na ukuaji wa biashara ya sasa sanjari na maeneo mapya yenye manufaa kwa siku zijazo.

Wasifu wa Machumu

Kabla ya uteuzi huo, Machumu alikuwa kaimu mkurugenzi mtendaji na mhariri mtendaji mkuu wa MCL ambayo ni kampuni ya habari inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti pamoja na majukwaa ya mtandaoni.

Kabla ya nafasi hiyo, alikuwa mhariri mtendaji wa The Citizen kwa miaka saba. Kabla ya kujiunga MCL mwaka 2004 kama mhariri wa biashara, Machumu alifanya kazi katika kampuni ya Business Times Ltd iliyokuwa inachapisha magazeti ya Majira, Business Times, Daily Times na Dar Leo kwa miaka sita na katika kipindi hicho alikuwa mwandishi wa habari za biashara na mhariri wa makala. Vilevile, amewahi kuwa mhariri wa habari wa gazeti la Daily Times.

Kitaaluma, Machumu ana shahada ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) alikohitimu mwaka 1998 na miaka 20 baadaye akahitimu shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA) kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uongozi cha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) na kwa sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nairobi akisoma shahada ya uzamili katika uongozi wa vyombo vya habari na ubunifu.

Uzoefu mwingine

Mbali na uzoefu wake katika masuala ya habari, Machumu ni Mjumbe wa Bodi ya Kikanda ya Mtandao wa Uchumi (IREN) nchini Kenya, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Uongozi la Baraza la Habari Tanzania na mwanachama mwanzilishi wa Taasisi ya Habari ya Kimataifa (IPI) nchini.

Pia, ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Wazazi na Walimu wa Shule ya Sekondari ya Barbro Johannson na mwenyekiti wa kamati ya sekta ya mawasiliano na uchukuzi ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Vilevile, ni mshindi wa ndani wa tuzo ya Titans Outstanding Media Leadership mwaka 2014 na mshindi wa ukanda wa Afrika Mashariki na mshiriki wa tuzo hiyo katika fainali Afrika.