Ibada ya hija yafutwa kwa sababu ya corona
Muktasari:
- Serikali ya Saudi Arabia imefuta ibada ya hija kwa mwaka 2021 kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Dar es Salaam. Serikali ya Saudi Arabia imefuta ibada ya hija kwa mwaka 2021 kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Hii ni mara ya pili kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutotekeleza ibada hiyo kutokana na gonjwa huo ulioanza kutikisa mwishoni mwa mwaka 2019.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatano Juni 16, 2021
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi amesema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaimu Balozi wa Saudi Arabia, Abdul Aziz Hamad, hija itatekelezwa kwa raia wa Saudi Arabia pekee na si wananchi kutoka mataifa mengine duniani.
"Kutokana na taarifa niliyopata hakutakuwa na hija mwaka huu, isipokuwa itatekelezwa na wenyeji Saudi Arabia ambao ni wakazi wa palepale kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.”
"Serikali ya Saudi Arabia wameona waifute kwa maana ya raia kutoka nchi nyingine kutoingia Saudi Arabia na watakaoshiriki ni wenyeji peke yao kwa idadi ndogo isiyozidi mahujaji 60,000," amesema.
Huku akiwataka Watanzania kujiandaa kwa hija mwaka 2022 amesema, “mwenyezi Mungu atupe subira juu ya jambo hili, huu ni mwaka wa pili kutokwenda hija, hii inatokana na ucha Mungu katika ibada.”