Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Idadi watoto wanaozaliwa na matatizo ya kiafya yaongezeka Tanzania

Wadau mbalimbali wa kampeni ya kusaidia watoto wanaozaliwa na changamoto za kiafya wakizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 3, 2024 katika ukumbi wa Kituo cha Habari cha EFM jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Tafiti zilizofanywa na madaktari saba wa nchi za Afrika, zimeonyesha kiwango cha vifo vya watoto wachanga kuwa juu tofauti na mataifa mengine

Dar es Salaam. Idadi ya watoto wanaozaliwa na tatizo la utumbo kuwa nje na wanaopata changamoto kwenye njia ya haja kubwa imetajwa kuongezeka nchini, huku kanda ya ziwa ikiongoza.

Imeelezwa kuwa, takwimu za afya zinaonesha kuwa, kila wiki watoto watano mpaka saba huzaliwa na utumbo ukiwa nje kitaalamu ‘Gastroschisis’ na wanane wanazaliwa na changamoto ya kukosa sehemu ya kutolea haja kubwa.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 3, 2024 na daktari bingwa mbobezi wa upasuaji kwa watoto kutoka  Hospitali ya Taifa Muhimbili,  Zaitun Bokhary katika uzinduzi wa mbio za watoto zinazojulikana kama "Mtoto Day Out Fun Run" zenye lengo la kukusanya zaidi ya Sh200 milioni kusaidia watoto wanaozaliwa na changamoto hizo.

Kufuatia hilo, ameitaka jamii kuungana kuwasaidia watoto wenye changamoto hizo ili kupunguza idadi ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Dk Zaitun amesema tafiti zilizofanywa na madaktari saba kutoka nchi za Afrika, zimeonyesha kiwango cha vifo vya watoto wachanga kuwa juu ni tofauti na mataifa mengine.

Miongoni mwa sababu za vifo hivyo kwa watoto ni kuzaliwa na tatizo la utumbo nje na kukosa njia ya haja kubwa.

“Tatizo la utumbo nje hutokea katika sehemu ya kitovu, hivyo huhitajika mfuko maalumu kuwezesha kurudisha utumbo ndani ya tumbo, bila kufanyika upasuaji tofauti na tatizo la haja kubwa ambalo huhitajika mtoto kufanyiwa upasuaji ili kumwezesha kutoa haja,” amesema.

“Licha ya tafiti kufanyika, lakini sababu hazijabainishwa zinazochochea changamoto hizo kwa watoto lakini baadhi zinazosadikika ni unywaji wa pombe uliopitiliza kwa mjamzito pia baadhi ya madini kuwa sumu katika maeneo ya kanda ya ziwa.”

Ametaja maeneo yanayoonekana kuathiriwa na changamoto hiyo ni kanda ya ziwa ikilinganishwa na maeneo ya mashariki.

Mkuu wa Idara ya Watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Monica Appollo amesema mtoto anayezaliwa na changamoto hizo huhitaji vifaa maalumu kuokoa uhai wake.

Amesema vifaa hivyo huwa na gharama, hivyo kuwaomba Watanzania kuunga juhudi za Serikali kusaidia kuokoa maisha ya watoto.

Mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi kutoka Redio ya EFM, Dina Marious amesema amekuwa akiandaa matamasha ya mbio za watoto kwa zaidi ya miaka saba.

Amesema kutokana na changamoto aliyoiona katika sekta ya afya, wameona ni vyema kuwalenga watoto wanaohitaji kupata msaada ili siku zijazo waungane na watoto wenzao katika matamasha ya michezo wakiwa na afya njema.

"Bei ya vifaatiba vya watoto wenye matatizo hayo ni kubwa, hivyo tumeandaa kampeni kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa na lengo la kupata fedha zitakazowezesha kugharamia matibabu ya watoto wanaozaliwa na changamoto hizo na kuwarudishia tabasamu," amesema Dina.