IGP Wambura aagiza ukaguzi vyuo vya udereva

Muktasari:
- Makosa ya kibinadamu yakiwemo mwendo kasi, ulevi, kutofunga mikanda na kutovaa kofia ngumu yanachangia ajali kwa zaidi ya asilimia 80, vyuo vya udereva vimetajwa kama sababu mpya ya ajali za barabarani.
Mwanza. Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura ametoa maagizo kwa wakuu wa vikosi vya usalama barabarani vya mikoa (RTO’s) kufanya ukaguzi na uhakiki wa shule zote za udereva nchini ili kujua kama zinakidhi ubora.
Hilo linafanyika ikiwa ni baada ya Jeshi la Polisi kugundua mfumo mbovu wa upatikanaji wa madereva kuwa ni chanzo kingine cha ajali nchini zinazogharimu maisha ya wananchi.
Ameyasema hayo leo Jumanne, Machi 14, 2023 wakati wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayofanyika kitaifa viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.
IGP Wambura amesema baadhi ya vyuo vya udereva vimekua vikitumika kama madaraja ya kurasimisha vyeti feki.
“Tumeshatoa maagizo kwa RTO’s (Wakuu wa kikosi cha usalama barabarani) ambao wapo hapa wote wafanye ukaguzi na uhakiki wa shule za udereva zote nchini kujua kama zinakidhi ubora wa kufundisha madereva na kama bado kweli zina sifa ya wale ambao ndiyo walimu wa madereva hao,” amesema Wambura.
Hilo litaenda sambamba na operesheni mbalimbali za kuhakiki leseni na vyeti vya madereva ambao hawajapatikana kwa njia halali nchi nzima na kuwachukulia hatua za kisheria wanaomiliki leseni kinyume cha utaratibu.
Amesema baadhi ya vyuo vimekuwa vikikosa weredi na sifa za kutoa mafunzo hivyo kutumika kama madaraja ya kurasimisha vyeti feki.
“Na pia baadhi ya watahiri wa madereva na wakaguzi wa magari kwenda kinyume na utaratibu wa utoaji wa leseni hizo bila kuzingatia miiko yao ya kazi,” amesema IGP Wambura.
Amesema mbali na jeshi hilo kutoa elimu mara kwa mara iliwalazimu kufanya uchunguzi wa kina ili kung’amua kiini na kisababishi cha matukio ya ajali.
Alidai kuwa awali malalamiko ya wananchi na baadhi ya watafiti yalidai ubovu wa miundombinu ya barabara kuwa ni moja wapo ya chanzo cha ajali za barabarani.
“Serikali ya awamu ya sita kwa kiasi kikubwa imeendelea na jitihada ya kutatua changamoto hiyo na wote tu mashuhuda wa miradi ya barabara inayoendelea nchini ya kuunganisha barabara za mikoa na zile za wilaya kwa kiwango cha lami kwa kiasi kikubwa zimepunguza matukio ya ajali nchini.
“Viahatarishi na visababishi vya ajali vilivyosalia kwa sasa ni uzembe wa madereva unaosababishwa na ulevi, mwendo kasi, mihemuko, ubovu wa magari, ujazaji wa abiria na mizigo,” amesema Wambura.
Amesema hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kudhibiti kadhia hiyo inayopelekea ajali ikiwemo kukaguana na kusimamiana kwenye utendaji wao eneo la usalama barabarani kwa kuhakikisha usimamizi wa sheria unazingatiwa.
Amesema jeshi hilo limejipanga kudhibiti ajali za barabarani kwa kubadilishana taarifa kwa njia za kielektroniki lengo likiwa ni kuwabaini madereva wanaokiuka sheria za barabarani na kuwachukulia hatua stahiki ili kunusuru maisha ya wananchi.