Imani potofu zachangia kupaa maambukizi ya malaria Tabora

Muktasari:
- Takwimu zinaonyesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kimeongezeka kutoka asilimia 11.7 mwaka 2016/2017 hadi asilimia 23.4 mwaka 2022 wakati kiwango cha maambukidhi ya malaria kitaifa ni asilimia 8.1.
Tabora. Mkoa wa Tabora umetajwa kuwa wa kwanza kitaifa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria hali inayotokana na imani potofu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa kuwa vinapunguza nguvu za kiume.
Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kimeongezeka kutoka asilimia 11.7 mwaka 2016/2017 hadi kufikia asilimia 23.4 mwaka 2022, wakati kiwango cha maambukidhi kitaifa ni asilimia 8.1.
Kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imetia kambi mkoani humo na kusambaza vyandarua vyenye dawa.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 25, 2023, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Luis Bura amesema hali ya ugonjwa huo ni mbaya kwa sasa kwa kuwa unaongoza kwa maambukizi nchini.
“Tafiti zinaonyesha kiwango cha maambukizi ugonjwa wa malaria kwa mwaka 2016/2017 kwa watoro wa umri wa miezi sita hadi miaka 5 ni asilimia 20 na mwaka 2018 yameongezeka kufikia asilimia 23,” amesema Bura.
Amesema ikitazamwa kitaifa, takwimu zinaonyesha maambukizi ya ugonjwa huo imefikia asilimia 8.1, hivyo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 11.7 hali inayosababisha mkoa huo kuongoza.
Kaimu mkuu huyo wa mkoa amesema hali hiyo haikubaliki hivyo ni lazima kuwa na nguvu ya pamoja kwa watendaji na jamii kuhakikisha maambukizi hayo yanapungua.
Bura amesisitiza makundi ambayo yako hatarini ndio yatanufaika na vyandurua hivyo wakiwemo watoto chini ya miezi tisa na miaka mitano, wajawazito, wanafunzi, wazee wa miaka 60 na watu wanaoishi na VVU.
Amesema zaidi ya kaya 300,000 kati ya 400,000 ambazo zitapewa vyandarua hivyo, ni zaidi ya milioni 1.8.
Naye Kaimu Meneja wa MSD mkoani Tabora Adonizedeck Tefurukwa ameshukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini na kuwahakikishia wananchi wa Tabora kuwa, kila mnufaika wa vyandarua hivyo atafikiwa.
Amesema katika usambazaji huo, wamejipanga ipasavyo na wanayo timu ya kutosha kufika katika kila maeneo.
Nan ili kulifanikisha hilo, Tefurukwa amesema wamekodisha maghala mawili ya ziada eneo la Nzega na Igunga kwa ajili ya kuhifadhia vyandarua hivyo kusudi wavigawe kwa haraka.
“Katika usambazaji huo tumepokea zaidi ya vyandarua milioni 1.8 ambavyo vitasambazwa katika vituo 2,673 sawa na kaya zaidi ya 400,000,” amesema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Honoratha Rutatinisibwa amesema takwimu hizo zimechangiwa na imani potofu wanazozikumbatia baadhi ya wananchi mkoani humo.
Amesema wengi wao wanadai kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa vinapunguza nguvu za kiume.
Pia, usafi wa mazingira usioridhisha huku halmashauri nazo zikishishindwa kutenga bajeti ya ununuzi wa viuadudu, wananchi kutokuwa na mwamko wa kupima na mkoa huo kutoingizwa katika mpango wa taifa wa kupulizia dawa za ukoko.
“Bila kusahau ongezeko la mazali ya mbu yanayotokana na kilimo, jiografia ya mkoa huu una maeneo mengi yenye madimbwi ya maji yaliyotuama, na hauna wadau wanaotoa misaada ya afua za kupambana na ugonjwa huu,” amesema Dk Rutatinisibwa.