Ivory Costa yatumia Sh3 trilioni kuandaa Afcon

Muktasari:
- Uwekezaji wa zaidi ya Sh3.7 trilioni umefanywa na nchi ya Ivory Coast katika miundombinu kwa ajili ya kuwa mwenyeji Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon). Michuano hiyo inaanza leo Jumamosi Januari 13 hadi Februari 11, 2024.
Ivory Coast. Macho na masikio ya wapenzi wa soka Afrika na duniani kote yakielekezwa katika ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), nchini Ivory Coast, imetajwa Sh3.767 trilioni zimetumika kuboresha miundombinu ya maeneo yatakapofanyika ya mashindano hayo vikiwamo viwanja.
Pia nchi hiyo imeweka bayana askari na wanajeshi 17,000 wanatarajiwa kutumika kuhakikisha usalama wakati mashindano hayo.
Hilo linafanyika wakati kiu kuu ya waandaaji wa ndani na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiwa ni kuhakikisha mashindano hayo yanakamilika bila kuwapo kwa matukio kama yale yalitokea msimu uliopita nchini Cameroon.
“Nimeridhika na hatua zilizochukuliwa kuhakikisha tutaepukana na vitu vya kuumiza kama vilivyotokea Cameroon,” amesema Rais wa CAF, Patrice Motsepe alipozungumza na Daily Monitor.
Michuano hiyo inafunguliwa leo Jumamosi, Januari 13, 2024 ambapo wenyeji hao wataumana na Guinea-Bissau katika uwanja mpya uliopewa jina la Rais wa Ivory Coast, Alasane Aouttara.
Maboresho hayo yaliyofanyika yatawezesha mechi kuchezwa katika miji mitano tofauti na mji mkuu Yamoussoukro, Bouake, eneo la pwani la San Pedro na mji wa kaskazini Korhogo na Abijan.
Katika mji mkuu wa nchi hiyo, viwanja vikuu viwili vinatarajiwa kutumika ambavyo ni Felic Houphouet Boingny uliopo katikati pamoja na uwanja wa Ebimpe.
Ivory Coast inaandaa mashindano haya ikiwa imewahi kutwaa taji hilo mara mbili na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2015 wakati timu hiyo ikiwa chini ya nahodha wa zamani, Yaya Toure huku wakiwa na matumaini ya kufanya vyema zaidi kwa sababu michuano hiyo inafanyika katika ardhi yao.
Wenyeji hao wako kundi A na timu za Nigeria, Guinea-Bussau na Equatorial Guinea.
Ivory Coast inapokea kijiti cha kuandaa mashindano hayo kutoka kwa Cameroon iliyokuwa mwenyeji mwaka 2021.
Jumla ya timu 24 zinashiriki michuano hiyo ikiwemo Tanzania inayoshikiri kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo 1980, 2019 huku nyingine zikiwa ni Morocco, Algeria, Afrika Kusini, Senegal, Burkina Faso, Tunisia, Misri, Zambia, Equatorial Guinea, Nigeria, Cape Verde, Mali, Guinea, Ghana, Angola, Zimbabwe, DR Congo, Mauritania, Gambia, Cameroon na Namibia.