Jacqueline Mengi aruka kiunzi cha kwanza Mahakama ya Rufani

Muktasari:

  • Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi amevuka kihunzi cha kwanza katika mapambano ya kisheria ya mirathi baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali pingamizi dhidi ya maombi yake kuhusu wosia.


Dar es Salaam. Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi amevuka kihunzi cha kwanza katika mapambano ya kisheria ya mirathi baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali pingamizi dhidi ya maombi yake kuhusu wosia.

Jacqueline amefungua maombi ya mapitio ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 18, 2021 na Jaji Yose Mlyambina iliyobatilisha wosia uliokuwa unadaiwa kuandikwa na marehemu Mengi wakati wa uhai wake, ambapo anaiomba Mahakama ya Rufani ifanye mapitio ya hukumu hiyo na hatimaye ibadilishe.

Kufuatia maombi hayo wajibu maombi wa kwanza Abdiel Reginald Mengi, ambaye ni mtoto wa marehemu Mengi wa mke mkubwa na Benjamin Abraham Mengi (mdogo wake na marehemu Mengi) walimwekea Jacqueline pingamizi la awali la hoja za kisheria wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali maombi yake bila kuyasikiliza.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ambao Mwananchi limeona nakala yake iliyotolewa na mahakama hiyo kwa matumizi ya umma, leo Jumatano, Oktoba 13, 2021, imetupilia mbali hoja zote za pingamizi dhidi ya maombi hayo ya Jacqueline na badala yake imekubali kuyasikiliza maombi hayo.

Jacqueline pamoja na mambo mengine ikieleza kuwa haukidhi matakwa ya kisheria ili kuwa wosia halali.

Awali, Jaji Yose Mlyambina alitoa uamuzi huo kufuatia shauri la mirathi lililokuwa limefunguliwa na watu wanne waliokuwa wameandikwa kwenye wosia huo kuwa wasimamizi wa mirathi wakiwemo ndugu wa marehemu Mengi, wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo.

Jaji Mlyambina alifikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na mmoja wa watoto wakubwa wa marehemu Mengi pamoja na ndugu yake marehemu Mengi, waliokuwa wakipinga uhalali wa wosia huo.

Shauri hilo la mirathi namba 39 la mwaka 2019 lilifunguliwa na Benson Benjamin Mengi, William Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi mirathi hiyo kwa mujibu wa wosia huo.

Hata hivyo, mtoto wa Mengi, Abdiel na ndugu wa marehemu, Benjamin, waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo wakipinga uhalali wake huku wakiwasilisha sababu nne za kuupinga.

Sababu hizo ni pamoja na kwamba haukuwa umepigwa muhuri na saini iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti na iliyokuwa ikitumiwa na Mengi na kuwa haukushuhudiwa na ndugu au mke wa marehemu.

Pia walikuwa wakidai marehemu hakuwa na uwezo wa kuandaa wosia kwa kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya tangu mwaka 2016 na kwamba, unaondoa katika urithi watoto bila kuzingatia mila za Kichaga au kuhusisha ndugu.

Jaji Mlyambina alikubaliana na sababu hizo za pingamizi na pamoja na mambo mengine alisema unawanyima urithi wanaye bila kutoa sababu, na kwamba ziliiingizwa mali za mke mkubwa na nakala yake alikuwa nayo mke mdogo, Jacqueline ambaye alikuwa mnufaika.

Kwa uamuzi huo Jaji Mlyambina hakuwateua waombaji hao kuwa wasimamizi wa mirathi na badala yake aliwateua Abdiel na Benjamin kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza mali za marehemu zigawiwe warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa mtu ambaye hakuacha wosia.

Awali, Jacqueline alijaribu kuingia katika shauri hilo bila mafanikio baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yake mara tatu.