Kikao cha ukoo kilivyokataa wosia wa mwisho wa Mengi (3)

Wednesday May 26 2021
mengipic
By Bernard James

Jana katika mapitio ya kesi ya mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, marehemu Reginald Mengi tuliona mmoja wa watoto wa tajiri huyo akiieleza mahakama kuwa hawakuwa tayari kuutambua wosia uliodaiwa kuandikwa na baba yao kwani ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwatupa nje ya urithi watoto wake wakubwa na kumpatia mali zake zote mke wake wa pili, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake pacha.

Tuliona pia Ntuyabaliwe akiunga mkono wosia ulioandikwa na mume wake, huku akiiomba mahakama iwathibitishe watu wanne ambao mpenzi wake huyo aliwateua kuwa wasimamizi wa mirathi.

Watu aliodai waliteuliwa na Mengi kuwa wasimamizi wa mirathi – Benson Benjamin Mengi, William Onesmo Mushi, Zoeb Hassuji na Sylvia Novatus Mushi – walifungua maombi Mahakama Kuu wakitaka wosia uthibitishwe na wao watambuliwe kama wasimamizi.

 Kufuatia maombi hayo, mtoto mmoja wa Mengi na Abdiel na kaka yake Mengi, Benjamin, walipeleka zuio la utekelezaji wa wosia huo hadi hapo hoja zao za kupinga zitakaposikilizwa na kuamuliwa.

Endelea ...

Baada ya kuwasikiliza mashahidi, mahakama iliwapa mawakili wa pande zote mbili kufanya majumuisho na ufafanuzi wa hoja zao.

Advertisement

Mawakili wa waleta maombi walijikita katika masuala makubwa mawili; uhalisi (validity) na usahihi (appropriateness) wa wosia wa Mengi.

Walianza kwa kujadili maana ya neno ‘validity’ kama lilivyotafsiriwa katika kamusi ya Black’s Law Dictionary ambayo kuwa ni ‘inayojitosheleza kisheria, inayofunga, na kwa upande mwingine, likimaanisha ‘sahihi’ au ‘inayojitosheleza’.

mengipiccccc

Pia walifanya marejeo katika kesi iliyowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufaani Tanzania kuhusu uhalali wa wosia katika kesi iliyofunguliwa na Mark Alexander Gaete na wengine wawili dhidi ya Grigitte Gaetje Defloor, ambapo mahakama ilitamka yafuatayo:-

 “…katika maombi ya kuthibitisha wosia mahakama hujikita katika kuthibitisha uhalali wa wosia. Maswali ambayo yatahitaji kujibiwa ni kama wosia ulisainiwa kwa usahihi ili uweze kutekelezwa kisheria; kama mtoa wosia alikuwa na uwezo wa kuandaa wosia; pale inapotokea mtoa wosia ana mapungufu au ulemavu fulani kama vile kipofu, kiziwi au kutojua kusoma wala kuandika (kama alijulishwa yaliyomo kwenye wosia au la na kadhalika na yeye akauridhia); kama kulikuwa na ushawishi usio halali au la; kama kulikuwa na kughushi au udanganPia waliangalia kama wosia huo ulikwishatenguliwa au la.

Kama wosia huo umekidhi vigezo vilivyotajwa hapo juu, basi wosia huo utachukuliwa kuwa umethibitishwa na mahakama itampa msimamizi wa mirathi nguvu/ruhusa ya kisheria kusimamia mirathi hiyo.

” Moja ya hoja walizotoa mtoto wa Mengi, Abdiel na kaka yake Mengi katika kutaka kusimamishwa utekelezwaji wa wosia wa tajiri huyo, ni kwamba wosia huo uliwatupa nje ya urithi watoto wakubwa wa marehemu bila kutoa sababu yoyote.

Wakili wa waleta maombi alipinga hoja hiyo kwa maelezo kuwa Gazeti la Serikali Namba 436 la mwaka 1963 chini ya jedwali la 3, sura ya 35 inatoa nafasi kwa watoto na wanufaika walionyimwa urithi kufungua maombi mahakamani ili iamue kama kubaguliwa kwao kulikuwa halali, jambo ambalo watoto wa Mengi hawakufanya.

Kuhusiana na wosia wa baba yao kuwa mikononi mwa mjane wa marehemu (Jacqueline) ambaye pia ni mnufaika, wakili wa waleta maombi alikiri kuwa wanufaika wa wosia wahatakiwi kuwa pia watunza wosia, akirejea kesi ya Shan Arshad Yusuf dhidi ya Zuberi Abdallah na wengine wawili.

Hata hivyo, alidai msimamo huo lazima utofautishwe na kesi iliyopo mbele yao kwa kuwa shahidi wao wa pili, mtunzaji nyaraka aliyeaminiwa, alitoa pia nakala ya wosia wa marehemu ambao ulilinganishwa na ule aliokuwa nao mjane na kuonekana kuwa sawa.

Aliongeza kuwa hoja kuwa wosia ule unaweza kuwa wa kughushi halikuthibitishwa kwa viwango vinavyotajwa katika vifungu vya 110 (1) (2) na 111 vya Sheria ya Ushahidi. Vifungu hivyo vinatamka kuwa mtu yeyote anayetaka mahakama iamini ukweli au jambo atalazimika kuthibitisha na si kuuachia upandemwingine wa kesi.

Kuhusu hoja kuwa afya ya akili ya marehemu alikuwa imetetereka (dementia) kutokana na umri na maradhi mengine wakati akiandika wosia, wakili wa waleta maombi alidai kuwa mtu sahihi kuthibitisha hilo ni Florence Msaki (katibu muhtasi wa Mengi) na Grace Maleto (mhudumu wa mapokezi wa IPP) ambao alidai walishuhudia wosia huo na kuusaini.

Sehemu ya mwisho upande wa waleta maombi ni kuhusu mashahidi waliosemekana kushuhudia wosia ule. Wakili wao alikubali kuwa wosia haukushuhudiwa sawasawa kwa kuwa mashahidi hawakuwa wanaukoo wa Mengi.

Akanukuu kanuni ya 19 ya Gazeti la Serikali Namba 436 la mwaka 1963 ambao jedwali la tatu la Sheria ya Tamko la Sheria za Kimila linalosema “wosia unaoandikwa hushuhudiwa na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika, yaani mashahidi wasiopungua wawili, (mmoja wa ukoona mmoja mtu baki) ikiwa mwenye wosia anajua kuandika.

Endapo mwenye wosia hajui kusoma wala kuandika patatakiwa kuwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na wawili wengine).

Alikiri wosia uliopo mahakamani haukuwa halali katika kipengele cha mashahidi waliousaini na si vinginevyo.

Watoto wa Mengi wajibu

Wakili wa waleta zuio alianza kwa kudai kuwa wosia unaodaiwa kuwa wa marehemu Mengi haukuwa halali kwa msingi kwamba mwenye wosia hakuwa na uwezo wa kuandika wosia na mashahidi pia hawakuwa na uweza wa kisheria kushuhudia na kusaini wosia ule.

Alidai pia wosia huo ulitoa kwa ajili ya urithi mali ambazo hazikumilikiwa na marehemu na kwamba marehemu alitupa nje watoto wake wa kuzaa katika wosia huo. Kuhusu uwezo wa marehemu kuandaa wosia, wakili huyo aliendelea kueleza kuwa mashahidi wanne walioletwa mahakamani walikuwepo wakati marehemu alipopatwa na kiharusi Oktoba, 2016 ambao uliathiri kumbukumbu yake na tangu wakati ule hakuwahi kupata nafuu hadi mauti yalipomfika.

Akanukuu Kanuni ya 7 ya jedwali la tatu la Sheria ya Tamko la Sheria za Kimila inayosema kuwa wosia hutenguliwa kama mwenye wosia atagundulika kuwa na tatizo la akili kwa sababu ya ugonjwa wa akili, ugonjwa na ulevi au hasira za ghafla, akirejea pia Sheria ya Urithi ya India, 1865 inayosema mtu yeyote mwenye akili timamu na si mtoto anaweza kugawa mali zake kwa kutumia wosia.

Kuhusu uwezo wa kisheria wa mashahidi wa wosia, wakili huyo aliikumbusha mahakama kuhusu ushahidi wa mashahidi walioshuhudia wosia ule—Florence Sawaya na Grace Maleta—ambao waliiambia mahakama kuwa hawakuwahi kuusoma wosia ule.

Aliongeza kuwa hata mkutano wa ukoo wa mengi uliukataa wosia ule kwa sababu mashahidi waliousaini hawakuwa ndugu wa damu wa marehemu kama sheria inavyotamka.

Zaidi ya hapo, alidai mke wa marehemu hakuwepo wakati wa kusainiwa kwa wosia ule, akirejea kesi ya Jackkson Reuben Maro dhidi ya Halima Shekigenda na ile ya Jackson Reuben Maro dhidi ya Hubert Sebastian ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania ilitengua wosia kwa kuwa mke wa marehemu hakuwepo wakati wosia ule ukiandaliwa.

Akifafanua kuhusu suala la marehemu kutoa urithi wa mali ambazo hakuzimiliki, wakili huyo alidai kuwa wosia wa marehemu ulihusisha mali ambazo hakuzimiliki kinyume na Kanuni ya I ya Jedwali la 3 la Local Customary Law (Declaration)

Namba 4. Kanuni hiyo imeweka wazi kuwa mwenye wosia haruhusiwi kurithisha mali asizomiliki. Aliongeza kuwa wosia wa Mengi ulihusisha mali ambazo zilikuwa chini ya mgawanyo katika kesi ya marehemu Mengi na mke wake wa kwanza, Mercy Anna Mengi, kitu ambacho marehemu alikijua.

Akihitimisha, wakili huyo alidai kuwa wosia huo uliwaweka kando watoto wa marehemu bila sababu, huku akinukuu Kanuni ya 38 ya Jedwali la 3 la Local Customary law (Declaration) (Namba 4) inayosema “kama itaonekana mtu amenyimwa urithi katika wosia pasipokuwa na sababu ya haki, wosia unavujwa na urithi utagawanywa kufuata mpango wa urithi usio wa wosia.

Aliongeza kuwa marehemu aliwanyima watoto aliozaa na mke wake wa kwanza, Abdiel na Regina, haki yao ya kurithi bila kutoa sababu yoyote. Wakili huyo akaendelea kueleza kuwa wosia unadaiwa kuandikwa na Mengi ulitokana na ushawishi usio halali (undue influence).

Hapa aliitaka mahakama kuzingatia mahusiana ya siri ambayo hutengeneza ushawishi kati ya mnufaika na mwenye wosia, kwa mfano, katika mazingira ambapo mwenye wosia anaumwa na anamtegemea mnufaika kwa uangalizi, matibabu au mahitaji mengine muhimu ya maisha.

Akadai pia kuwa hata mke wa Mengi, Ntuyabaliwe pia alijua kuhusu suala wa watoto wengine wa Mengi kuwekwa pembeni katika urithi.

Akasema hata Ntuyabaliwe alikiri kuwa siku ya kwanza walipowasili na mwili wa marehemu kutoka Dubai alifungua sefu ambamo wosia ulikuwa umehifadhiwa na kuuweka katika sefu nyingine katika chumba chake.

Kesho tutaangalia mahakama ikichambua mfumo wa maisha ya Mengi ili kupata sheria sahihi itakayotumika kufikia hukumu

Advertisement