Mtoto wa Mengi: Baba asingeweza kuandika wosia kama huu bila kushawishiwa (2)

Tuesday May 25 2021
kikao pc
By Bernard James

Jana katika mapitio ya kesi ya mirathi ya Reginald Mengi, mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, Reginald Mengi tuliona jinsi watu wanne walivyofungua kesi wakiiomba Mahakama Kuu wakitaka kuthibitishwa kuwa wasimimizi wa mirathi ya tajiri huyo.

Tuliona pia mtoto na kaka yake Mengi wakiweka zuio ili watu hao wasithibitishwe kwa madai kuwa wosia wa baba yao haukuwa na uhalali wa kisheria kwa kuwa ulitokana na ushawishi usiokuwa halali, wakati baba yao akiwa amepoteza uweza wa kuandaa wosia.

Watoto hao walilalamika kuwa wosia huo ambao ulimtaja mke wa mwisho wa baba yao, Jacqueline Ntuyabaliwa na watoto wake mapacha kuwa ndio warithi pekee wa mali zote za tajiri huyo, ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwaweka kando watoto wengine wa marehemu. Endelea…


Baba alishawishiwa

Katika kulipa nguvu zuio walilofungua mahakamani, shahidi wa kwanza ambaye pia ni mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi, alianza kwa kuwasilisha mahakamani cheti chake cha kuzaliwa ili kuthibitisha kwamba alikuwa mtoto wa marehemu mengi.

Advertisement

Abdiel alitoa maelezo mafupi kuhusu maisha ya baba na mama yake (mke wa kwanza wa Mengi ambaye pia amefariki) yalivyokuwa, akilenga kuishawishi mahakama iamini kuwa baba yao alikuwa katika uhusiano mzuri na familia yake na kwamba hakuwa katika hali ya kutoelewana na watoto wake.

Aliieleza mahakama kuwa baba yake alianza kuishi na vimada kabla hata ya kuachana na mama yake na kwamba hata wadogo zake wawili mapacha ambao aliwazaa na mke wake wa pili, Jacqueline, walizaliwa kabla hajaachana rasmi na mama yake.

Akasisitiza kuwa marehemu aliheshimu mila na desturi za Kichaga na alizikwa Machame, Kilimanjaro.

Kuhusiana na wosia unaobishaniwa, Abdiel alisema baba yake aliandaa wosia ule wakati afya yake ikiwa imetetereka baada ya kupatwa na kiharusi Oktoba 2016, na tangu hapo hakuwahi kupata nafuu.

Mbali na matatizo ya kiafya, Abdiel alidai kuwa bahasha iliyokuwa imehifadhi wosia ulidaiwa kuandikwa na baba yao ilikuwa haikufungwa kwa rakili, hivyo kuacha uwezekano mkubwa wa kuchezewa.

“Wosia huo ulishuhudiwa na watu ambao hawakuwa ndugu wa marehemu na pia haukushuhudiwa hata na mke wa marehemu,” alidai shahidi huyo.

Aliongeza kwa wosia huo umezitoa kama urithi mali ambazo hazikuwa zikimilikiwa na marehemu, kwa mfano, mali alizochuma na kuzimiliki kwa pamoja na mke wake wa kwanza.

Abdiel alidai pia baba yake aliheshimu na kuishi maisha ya kimila kama inavyothibitishwa kwa kuwapa watoto wake majina ya Kichaga, na kuongeza kuwa ingawa baba yake alikuwa na ndoa ya Kikristu alikuwa na mahusiano ya waziwazi ya kimapenzi nje ya ndoa.

“Baba asingeweza kuandika wosia kama si kulazimishwa na mke wake wa pili kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kupata ushauri wa wataalamu wengi wa sheria.Ni kwa sababu ya ugonjwa, ndio maana alifanya hivyo. Kama marehemu alikuwa na nia ya kutunyima mali zake angesema,” alidai shahidi huyo.

Ushahidi uliotolewa na shahidi wa pili Benjamin Mengi (kaka wa marehemu) na shahidi wa tatu Regina Mengi (mtoto wa marehemu) ulifanana kwa kiasi kikubwa na ule wa Abdiel, huku Benjamin akifunga ushahidi wake kwa kueleza nini atafanya endapo mahakama itamteua kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu.

Benjamin alisema endapo mahakama ingemteua kuwa msimamizi wa mirathi atahakikisha kuwa mjane na watoto wake wanapata mgao halali wanaostahili.

Pia aliahidi kuwaongoza watoto wakubwa wa marehemu pamoja na mama yao kwa kuwashauri kuwatunza watoto wadogo wa marehemu ambao wana miaka minane tu na kuwasaidia kukua kitaaluma na kimaadili.

Akaahidi pia kuhakikisha uhusiano mzuri kati ya watoto wakubwa wa marehemu na wale wadogo ili waishi pamoja kama familia moja ya Reginald Abraham Mengi. Mwisho aliahidi kuwaandaa kiakili wajue nao ni warithi wa mali za baba yao.


Ushahidi wa Jacqueline, daktari

Jacqueline na daktari wa Mengi, Valentina Ochieng Khoja hawakuwa sehemu ya maombi yaliyofunguliwa mahakamani lakini mahakama iliamua kuwaita kama mashahidi wake muhimu ili waisaidie kufikia uamuzi sahihi.

Jacqueline alianza kwa kuieleza mahakama kuwa uhusiano wake na Mengi ulianza mwaka 2011 na baadaye kufunga ndoa ya kiserikali mwaka 2015. Aliongeza kuwa alizaa watoto na marehemu kabla ya kufunga ndoa.

Katika ushahidi wake Jacqueline alisema mwake 2016 Mengi alipata tatizo la kiharusi cha muda mfupi (mini-stroke). Alitembea kwa maumivu lakini aliweza kuongea kawaida tu. Baadaye tulienda Dubai kwa ajili ya mapumziko na tukiwa huko Mengi alifanya uchunguzi wa afya yake na kugundulika alihitaji kuwekewa pacemaker (betri ya moyo) mwaka 2019,” alisema Ntuyabaliwe na kuongeza:

“Baada ya kuwekewa pacemaker alianza kupata maumivu ya kifua na baadaye alifariki dunia.”

Ntuyabaliwe aliuunga mkono wosia wa mume wake na uteuzi wa waleta maombi wanne kama wasimamizi wa mirathi ya mume wake kwa kuwa walitajwa kwenye wosia huku akipinga zuio lililowasilishwa mahakamani.

Kwa upande wake, daktari aliyekuwa akimtibu Mengi kwa zaidi ya mara kumi tangu 2015 hadi Desemba 2017, Valentina Khoja alidai kuwa mteja wake alikuwa na magonjwa matatu yaliyohitaji uangalizi wa daktari mbobezi.

Aliyetaja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, tezi dume pamoja na shinikizo la damu lililomsababishia kiharusi. Alidai kuwa Mengi alipatwa na kiharusi Oktoba, 2016.

“Marehemu alipatwa na kiharusi ambacho kiliathiri sehemu ya ubongo wake inayodhibiti mwenendo wa misuli,” alisema daktari huyo.

Aliongeza kuwa Mengi alikuwa pia akisumbuliwa na ugonjwa wa gauti lakini hakumbuki kama aliwahi kuwa na tatizo la kumbukumbu.

kikao pcc

Majumuisho ya mawakili

Baada ya mahakama kusikiliza mashahidi, mawakili wa pande zote waliwasilisha mahakamani hoja zao za majumuishio ya mwisho.

Katika moja ya malalamiko yao, waliofungua zuio la kuthibitishwa kwa wosia wa Mengi, walihoji uhalali wa wosia huo kuwanyima urithi watoto wakubwa wa marehemu bila kutoa sababu yoyote.

Mawakili wa waleta maombi waliipinga hoja hiyo huku wakinukuu Gazeti la Serikali (GN) Namba 436 ya mwaka 1963, chini ya jedwali la tatu, ambayo inatoa mwanya kwa wanufaika walionyimwa urithi kuhoji mahakamani kama kunyimwa kwao kulikuwa halali, jambo ambalo walidai watoto wa Mengi hawakulifanya.

Kuhusu hoja kwa nini wosia wa baba yao ulikuwa mikononi mwa mjane wa marehemu ambaye pia ni mnufaika, mawakili wa waleta maombi walidai ni kweli wanufaika wa wosia hawatakiwi kuwa watunzaji wa wosia.

Hata hivyo, alidai katika shauri lao, shahidi wa pili ambaye pia alikuwa msaidizi binafsi wa Mengi, Florence Msaki, aliyeaminiwa na marehemu kutunza wosia huo alitoa nakala ya wosia huo na kulinganishwa na ule aliokuwanao mke wa marehemu na kuonekana ililingana kwa kila kitu.

Walisema suala la kuwa wosia ule ulikuwa wa kughushi halikuweza kuthibitishwa kama inavyotakiwa na sheria ya ushahidi.

Kuhusu hoja kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la afya ya akili (dementia) wakati akiandika wosia huo, wakili wa waleta maombi walidai kuwa mtu sahihi wa kuthibitisha madai hayo ni Florence na Grace Maloto (mhudumu wa mapokezi IPP) ambao walikuwa mashahidi wa wosia huo.

Suala la mwisho katika sehemu hii ni kuhusu mashahidi waliodai kushuhudia wosia ule. Katika hili, wakili wa waleta maombi alikubali kuwa wosia ule haukushuhudiwa kwa usahihi kwa kuwa washuhudiaji hawakuwa wana ukoo.

Kanuni ya 19 ya Gazeti ya Serikali Namba 436 ya mwaka 1963 na jedwali la tatu la Sheria ya Tamko la Sheria za Kimila ya mwaka 1963 imeweka wazi kuwa “wosia ulioandikwa ushuhudiwe na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika.

Inataka wosia ushuhudiwe na mashahidi wasiopungua wawili, (mmoja wa ukoo na mwingine mtu baki) ikiwa mwenye wosia anajua kuandika na wasiopungua wanne (wawili wa ukoo wawili watu baki) ikiwa mwenyewe hajui kusoma wala kuandika.

Wakili huyo alikiri kuwa wosia ulikuwa na mapungufu kuhusiana na kipengele cha mashahidi waliousaini.


Itaendeleo kesho

Advertisement