Kesi ya urithi wa Mengi hatua kwa hatua-1

Kesi ya urithi wa Mengi hatua kwa hatua-1

Muktasari:

  • Haijawahi kuwa rahisi kwa familia nyingi kumaliza mashauri ya mirathi kwa amani, hata pale inapotokea marehemu alionesha mgawanyo wa mali zake katika wosia aliouacha.

Haijawahi kuwa rahisi kwa familia nyingi kumaliza mashauri ya mirathi kwa amani, hata pale inapotokea marehemu alionesha mgawanyo wa mali zake katika wosia aliouacha.

Tafrani na hali ya kutoelewana huwa kubwa zaidi kama aliyefariki na kuacha ama kutoacha wosia alikuwa tajiri aliyemiliki mali nyingi.

Moja ya familia za kitajiri zilizotumbukia katika mgogoro mkubwa wa mirathi ni ile ya marehemu Reginald Mengi, mfanyabiashara bilionea na mmiliki wa kampuni za IPP ambaye alipenda kujibainisha kama mtu mkarimu na mwenye kusaidia wahitaji.

Wiki chache baada ya kifo cha tajiri huyo kilichotokea Mei 2, 2019 katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Dubai, watu wanne walifungua maombi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiitaka iwathibitishe kuwa wasimamizi wa mirathi ya tajiri huyo kupitia wosia aliouacha.

Katika wosia wake aliouandika Agosti 17 2017, Mengi amemtaja mke wake, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake mapacha kuwa wamiliki wa mali zote pindi atakapoaga dunia, huku ukiwaweka kando watoto wengine aliozaa na mke wake wa kwanza.

Mengi alifunga ndoa na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2000, Ntuyabaliwe na kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na tofauti ya umri.

Mtoto wa Mengi, Abdiel na mdogo wake Mengi, Benjamin, walishitushwa na taarifa za kuwepo kwa maombi hayo mahakamani.

Haraka haraka walipeleka zuio la kisheria kutaka mahakama kusitisha uthibitishwaji wa wasimamizi wa mirathi waliotajwa kwenye wosia wa baba yao hadi hapo malalamiko yao yatakaposikilizwa.

Waliweka zuio hilo chini ya kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Urithi na Usimamizi wa Mirathi ambacho kinatamka kuwa mtu yeyote ambaye anadai kuwa mnufaika wa mali za marehemu anaweza kuweka zuio la kuthibitishwa msimamizi wa mirathi au mrithi hadi pale mahakama itakaposikiliza hoja zake.

Hoja za watoto wa Mengi

Abdiel na mdogo wake Mengi, Benjamin walidai katika moja ya hoja tano walizowasilisha mahakamani kuwa wosia uliodaiwa kuandaliwa na baba yao haukuwa halali kisheria, kwa kuwa alikwishapoteza uwezo wa kuandaa wosia kutokana na matatizo makubwa ya afya yaliyomsumbua tangu mwaka 2016.

Pia walitaka mahakama isiuthibitishe wosia huo kwa kuwa ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwaweka kando watoto wake halali na kumpa mali zote Ntuyabaliwe na watoto wake mapacha.

Katika hoja nyingine watoto hao walidai kuwa wosia wa baba yao haukuwa umefungwa lakiri (seal) na kwamba sain zilizopo katika wosia huo zilikuwa tofauti na saini halisi ya baba yao.

Walidai pia kuwa wosia huo haukushuhudiwa na ndugu yeyote au mke wa baba yao, wakihofia kuwa kitendo hicho kitaleta mkanganyiko na ugumu kwa walionyimwa urithi kulienzi jina la familia yao na urithi wa baba yao.

Kwa mujibu wa watoto hao, wosia huo ulikiuka sheria inayohusu uandaaji wa wosia, wakidai ulikuwa wa kibaguzi na ulifanywa kwa ushawishi mbaya wakati baba yao akiwa amepoteza uwezo wa kutumia dhamira yake kwa uhuru kamili.

Walipinga pendekezo lolote kuwapa waleta maombi haki ya urithi na usimamizi wa mirathi hawakuwa na nasaba wala kuhusika katika mali za marehemu, wakidai wote walikuwa ni ‘wageni’ kwa mali ya baba yao, hivyo wangesababisha ugumu na mashaka katika usimamizi wake.

Waliiambia mahakama kuwa wao ndio walioteuliwa na ukoo wao kusimamia mali za marehemu Reginald Mengi.

Majibu ya waleta maombi

Waliofungua maombi ya usimamizi wa mirathi waliiambia mahakama kuwa wao wanaamini kuwa wosia unaobishaniwa ni halali, huku wakiiomba mahakama kutamka hivyo.

Katika hatua hii ya kesi, mahakama iliamua kuligeuza shauri na kulisikiliza kwa mfumo wa kesi kamili ya madai kwa mujibu wa kifungu cha 52 (b) cha Sheria ya Urithi na Usimamizi wa Mirathi.

Katika kesi hiyo, waleta maombi waliwakilishwa na wakili Elisa Abel Msuya, Regina Kiumba na Irene Mchau wakati waleta zuio waliwakilishwa na wakili mwandamizi, Nakazael Lukio Tenga na mawakili Roman Masumbuko, Hamis Mfinanga na Grayson Laizer.

Masuala kuamuliwa na mahakama

Baada ya kusikiliza hoja za awali za pande zote, mahakama pamoja na pande zote walikubaliana masuala manne ambayo mahakama itatakiwa iyaamue ili haki itendeke.

Suala la kwanza lililowekwa mbele ya mahakama kuamua lilikuwa ni kama wosia wa Dk Mengi wa Agosti 17, 2017 uliandaliwa kukiwa na sababu thabiti na halali.

Mahakama ilitakiwa pia kuamua kama wosia huo uliandaliwa kwa usahihi na kama mahakama iwakubalie waleta maombi au kutoa hati ya usimamizi wa mirathi kwa waleta zuio.

Pia ilitakiwa kuamua ni nafuu gani wa kisheria kila upande unastahili.

Mashahidi wa waleta maombi

Katika usikilizwaji wa kesi hiyo, waleta maombi walileta mashahidi wanne ambao ni Sylivia Novatus Mushi (Katibu wa kampuni za IPP), Florence Sawaya Msaki (katibu/msaidizi binafsi wa marehemu Mengi), Grace Delicia Maleto (mhudumu wa mapokezi) na Benson Benjamin Mengi aliyedai kuwa mpwa wa Mengi.

Mashahidi wa utetezi

Upande wa utetezi ulileta mashahidi watatu ambao ni watoto wa marehemu, Abdiel Alese Mengi na Regina Anchelita pamoja na kaka yake Mengi, Benjamin Abraham Mengi.

Pia mahakama kwa kutumia busara yake na nguvu ya kisheria iliyonayo iliamua kuita mashahidi wake ambao ni mke wa Mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe pamona na aliyekuwa daktari wa Mengi, Valentina Ochieng Khoja kutoa ushahidi ili waisaidie mahakama kutenda haki.

Akitumia kesi ya John Magendo dhidi ya N.E. Govani, iliyowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani kufafanua kwa nini mahakama iliamua kuita mashahidi wake, jaji aliyesikiliza shauri hilo, Yose Mlyambina alisema ili kufikia uamuzi wa haki, Sheria ya Mwenendo wa Madai inampa jaji au hakimu, si tu nguvu za kuita mashahidi anaoamini wataisaidia mahakama kutenda haki, bali ni lazima kwa wao kufanya hivyo, endapo itaonekana kufanya hivyo kutasaidia kufikia uamuzi wa haki.

Mahakama yapokea ushahidi

Shahidi wa kwanza wa waleta maombi, Sylivia Novatus Mushi aliieleza mahakama kuwa amekuwa akifanya kazi na marehemu tangu mwaka 2007 na kwamba, alikuwepo wakati marehemu Mengi akisaini wosia wake wa mwisho ambao ulimteua yeye pamoja na wengine kama wasimamizi wa mirathi.

Katika hali iliyoishangaza mahakama, Mushi aliongeza kuwa hakuwahi kujua kilichoandikwa kwenye wosia huo kwa kuwa haukusomwa kwao siku ulipoandikwa.

Aliendelea kueleza kuwa Oktoba 2016, marehemu alipatwa na tatizo la kiharusi, hali ambayo iliathiri uwezo wake wa kutembea na kufanya kazi.

Alidai hali hiyo pia iliathiri kumbukumbu zake hadi hatimaye kufikwa na mauti.

 Si wosia wa kwanza kwa Mengi

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa Mengi aliwahi pia kuandaa na kusaini wosia nyingine ambamo aligawanya mali zake zote kwa wote waliostahili kurithi, wakiwemo watoto wake Regina na Abdiel, wa mwisho ukiwa ule aliouandaa mwaka 2014.

Alidai kuwa wosia wa mwisho wa Mengi ulitayarishwa na Sabas Kiwango ambaye alitoa nyaraka za wosia huo kutoka kwenye kompyuta yake ya mkononi kwa kutumia diski mweko (flash disk) na kuzileta ofisini kwa marehemu kwa ajili ya kudurufiwa na baadaye alizisaini.

Sylivia aliendelea kuieleza mahakama kuwa baadhi ya mali zilizoorodheshwa katika wosia huo hazikumilikiwa na marehemu wala marehemu hakuwa na hisa katika kampuni hizo.

 Akasema, kwa mfano, kampuni inayoitwa Tanzania Diamonds Limited, Tanzania Oil & Gas Limited na ile ya Oil & Gas Resources East Africa Limited hazikuwa zikifanya kazi kwa muda mrefu.

Alieleza pia kuwa baadhi ya kampuni zilizotajwa zilikuwa zilizomilikiwa na familia ambapo Abdiel na Regina walikuwa pia wakurugenzi.

Kwa upande wake, shahidi wa pili wa waleta maombi, Florence Sawaya Msaki naye alidai kuwa alishuhudia wosia huo wa Mengi.

Ushahidi wake haukutofautiana na ule wa shahidi wa kwanza, Sylivia kuwa hawakupewa fursa ya kujua kilichoandikwa ndani ya wosia ule mbali na kuitwa kama mashahidi. Shahidi wa tatu, Grace Delicia Maleto pia alieleza kushuhudia wosia huo na kuongeza kuwa hakuwahi kujua kilichoandikwa hadi mauti yalipomfika Dk Mengi.

Alisema hakujua hata kama marehemu aliwatoa kwenye urithi hata watoto aliowazaa. Hata hivyo, Grace alikiri wakati akihojiwa na wakili wa waleta zuio kuwa hakuna ndugu yeyote wa marehemu aliyekuwepo wala kushuhudia wakati wa kusainiwa kwa wosia ule, akiongeza kuwa marehemu alipatwa na ugonjwa wa kiharusi na kupoteza nguvu.

Shahidi wa mwisho wa waleta maombi alikuwa ni Benson Benjamin Mengi, aliyedai kuwa marehemu alikuwa baba yake mdogo na alikuwa na uhusiano naye mzuri. Benson alidai ndiye alimsaidi marehemu kumalizia uchapishwaji wa kitabu chake cha “I Can, I Must, I Will”.

Alidai kuwa marehemu hakuwa na afya nzuri tangu alipopatwa kiharusi Oktoba 2016 na kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.

Kwa mujibu wa Benson, watoto wakubwa wa marehemu walikuwa na ugumu kumtembelea baba yao kwa kuwa mke wake, Jacqueline aliwazuia kufanya hivyo.

Kesho tutaangalia watoto wa marehemu Mengi wakitoa ushahidi wao na kufafanua kwa nini wanapinga kutekelezwa kwa unaodaiwa kuwa wosia wa mwisho wa baba yao.