Siri ya Mengi kuwekewa mashine kwenye moyo

Muktasari:

Marehemu Reginald Mengi, aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, aliwekewa kifaa maalumu cha kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker) wiki chache kabla ya kifo chake.

Dar es Salaam. Marehemu Reginald Mengi, aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, aliwekewa kifaa maalumu cha kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker) wiki chache kabla ya kifo chake.

Mengi alifariki Mei 2, 2019 katika hospitali moja ya Dubai, wiki chache baada ya kwenda huko kwa matembezi na kufanya vipimo vya afya yake akiwa na mkewe, Jacqueline Ntuyabaliwe.

Hayo yalielezwa na Ntuyabaliwe mbele ya Mahakama Kuu wakati akitoa ushahidi katika maombi yaliyofunguliwa kutaka mahakama imthibitishe kuwa mrithi wa mali za Mengi kupitia wosia aliodaiwa kuuandika Agosti 17, 2017.

Jumanne wiki hii, Mahakama Kuu imeyatupilia mbali maombi yaliyofunguliwa na Benson Benjamin Mengi (binamu wa Mengi), William Onesmo Mushi, Zoeb Hasujji na Sylvia Novatus Mushi (aliyekuwa katibu wa Kampuni ya IPP).

Watu hao walikuwa wakiiomba Mahakama imthibitishe rasmi mrithi aliyetamkwa kwenye wosia wa mwisho wa marehemu Mengi ili aweze kuyashughulikia yote aliyopewa.

Kisheria, maombi kama hayo yanapofunguliwa, waleta maombi hutakiwa kuwapa notisi watoto wote wa marehemu na wanufaika wa mali zake kuwajulisha uwepo wa maombi ya namna hiyo ili wahoji na kupinga wosia huo, kama wana nia ya kufanya hivyo.

Mahakama iliridhika na hoja zilizotolewa na mtoto na mdogo wa Mengi  waliopinga maombi hayo, Abdiel Mengi na Benjamin Mengi, waliodai kuwa Mengi alikuwa amepoteza uwezo wa kuandaa wosia huo kwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na matatizo makubwa ya afya.

Walidai kuwa wosia huo haukuwa sawa kwa kuwa uliwanyima watoto halali wa marehemu haki ya urithi bila kuzingatia mila za kabila la Wachaga au bila kumhusisha ndugu yake yeyote.

Walisema wosia huo ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwa uliwarithisha mali zote za marehemu mke wake mpya, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake pacha.

“Mwaka 2016 Mengi alipata tatizo la kiharusi cha muda mfupi (mini stroke). Alitembea kwa maumivu lakini aliweza kuongea kawaida tu. Baadaye tulikwenda Dubai kwa ajili ya mapumziko na tukiwa huko Mengi alifanya uchunguzi wa afya yake na kugundulika kuwa alihitaji kuwekewa pacemaker mwaka 2019,” alisema Ntuyabaliwe.

“Baada ya kuwekewa pacemaker alianza kupata maumivu ya kifua na baadaye alifariki dunia.”

Ntuyabaliwe hakuwa mmoja wa watu wanne waliofungua maombi ya kutaka wosia wa Mengi uthibitishwe na Mahakama, lakini Mahakama, kwa kutumia uwezo wake, iliamua kumwita yeye pamoja na daktari wa Mengi, Valentina Ochieng Khoja, watoe ushahidi utakaoisaidia kufikia uamuzi sahihi.

Dk Khoja aliiambia Mahakama kuwa amewahi kumhudumia Mengi kimatibabu zaidi ya mara kumi tangu 2015 hadi Desemba 2017 na kwamba tajiri huyo alikuwa akisumbuliwa na magonjwa matatu yaliyohitaji daktari mbobezi.

Aliyetaja magonjwa hayo kuwa ni shinikizo la damu, tezi dume pamoja na shinikizo la damu tata lililomsababishia kiharusi. Alisema Mengi alipatwa na kiharusi Oktoba, 2016.

Alisema Mengi alikuwa pia akisumbuliwa na ugonjwa wa gauti, lakini hakumbuki kama aliwahi kuwa na tatizo la kumbukumbu.

Usikose kusoma mfululizo wa uchambuzi wa kesi ya mirathi ya bilionea Reginald Mengi ambao gazeti lako la Mwananchi litakuwa likikuletea kila siku kuanzia kesho.