Jafo aishukia Suma JKT ujenzi Ofisi Makamu wa Rais

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo.

Muktasari:

  • Waziri Jafo ameipa wiki mbili kampuni ya Suma JKT inayojenga Ofisi ya Makamu wa Rais mkoani Dodoma kukamilisha kazi ndani ya muda, kabla hajaifutia mkataba.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo amempa wiki mbili mkandarasi wa kampuni ya Suma JKT pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linalosimamia kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa ofisi ya Makamu wa Rais kwa muda waliopewa.

Ofisi ya Makamu wa Rais ilisaini mkataba wa Sh18.8 bilioni na Kampuni ya Suma JKT Oktoba 13, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi iliyopaswa kukamilika Novemba 09, 2022.

Kwa mujibu wa mpango kazi uliowekwa, kazi ya ujenzi huo kwa ujumla uko nyuma hali inayotokana na kasi ndogo ya ujenzi wa jengo hilo kutoridhisha.

Akiwa ameambatana na viongozi na wataalamu kutoka Ofisi hiyo katika ujenzi unaoendelea eneo la Mtumba jijini Dodoma leo Februari 1, 2023, Waziri Jafo ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo hilo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi.

“Hapa mko nyuma sana, wenzenu kule wako mbali kuliko ninyi na mara ya mwisho tulipokutana mkaniambia kazi itakwenda kwa kasi, lakini ndio mkaamua kabisa kusimama na mmeanza tena kufanya baada ya kusikia ninakuja kukagua,” amesema Jafo.

Amesema Serikali haitavumilia kuona kazi hiyo inakwama na kama hawataonesha maendeleo ya kuridhisha, mkataba utavunjwa ili apewe mkandarasi mwingine.

Katika ziara hiyo, Waziri Jafo pia ametembelea majengo mengine yanayojengwa na Suma JKT na kubaini ujenzi wake unakwenda kwa kasi hivyo akaonya kuchukua hatua ya kuvunja mkataba.