Jafo ataka kiwanda cha saruji kuchukuliwa hatua

Jafo ataka kiwanda cha saruji kuchukuliwa hatua

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kiwanda cha saruji cha Fortune kwa kuzalisha vumbi kwenye makazi ya wananchi.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kiwanda cha saruji cha Fortune kwa kuzalisha vumbi kwenye makazi ya wananchi.

Waziri Jafo amekitembelea kiwanda hicho leo Jumanne Mei 4, 2021 Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ambapo viongozi wa kiwanda hicho hawakuwepo licha ya kuelezwa kuwa walipewa taarifa.

Jafo amesema licha ya kuvihitaji viwanda kwa ajili ya kukuza uchumi, hatakubali kuona viwanda hivyo vinachafua mazingira na kusababisha adha kwa wananchi waishio maeneo ya jirani.

"Nimepokea malalamiko ya wananchi kwamba kiwanda hiki kinapeleka vumbi kwenye maeneo yao. Nimekuja hapa kujionea hali halisi, wenye kiwanda wamekimbia na mitambo wamezima. Kuna tatizo hapa.”

"Nemc chukueni hatua mara moja kwa mujibu wa sheria. Hatuwezi kuruhusu uchafuzi wa mazingira, afya za wananchi ziwe matatani kwa sababu ya viwanda. Haiwezekani," amesisitiza Jafo.

Kabla ya ziara ya Jafo, kiwanda hicho kilipewa notisi na Nemc kushughulikia suala la vumbi zinazoelekea kwenye makazi ya wananchi na leo walitakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo hayo lakini hawakuwepo.

Wakati huohuo, Waziri Jafo ametembelea kiwanda cha chuma cha Lodhia na kuridhishwa na jinsi kinavyozingatia uhifadhi wa mazingira.

Amewataka wananchi kutoharibu miundombinu na kwenda kuuza kwa sababu ni kosa kisheria na kuwataka kutoa taarifa wanapoona watu wanahujumu miundombinu ya Serikali.