Jaji kesi ya Mbowe ateuliwa kuwa Jaji Kiongozi

Jaji kesi ya Mbowe ateuliwa kuwa Jaji Kiongozi

Muktasari:

  •  Rais Samia Suluhu Hassan ameteua viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameteua viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 8, 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Jaffar Haniu imesema uteuzi huo umeanza jana Oktoba 7, 2021.

Jaji Siyani ndiye aliyekuwa akisimamia kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya kigaidi.

Kesi hiyo inayosikilizwa  katika Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, ilianza kwa kesi ndogo ambayo nayo ilifikia hatua ya uhukumu kabla ya kuendelea na kesi ya msingi.

Jaji Siyani alipewa jukumu hilo baada ya Mbowe na wenzake kumkataa Jaji Elinaza Luvanda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo awali. 

Kabla ya uteuzi wa sasa Jaji Siyani alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na anachukua nafasi iliyoachwa na Jaji Elieza Feleshi aliyeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mbali na Jaji Siyani, taarifa ya Ikulu pia imemtaja aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu aliyeteuliwa kuwa Jaji katika Mahakama ya Rufani Tanzania.

Taarifa ya Ikulu pia imemtaja aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sofia Mjema anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akichukua nafasi ya Dk Philemon Sengati ambaye uteuzi wake umetenguliwa.