Mbowe na wenzake wafikishwa Mahakamani, mbele ya jaji mpya

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe  amefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.

  

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.

Mbowe na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa Septemba 10, 2021, saa 3:30 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja katika mahabusu ndogo iliyopo katika Mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Hata hivyo muda mfupi baadae, washtakiwa hao wamepelekwa Mahakama ya wazi, maalumu kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.


Washtakiwa hao wanatarajia kuendelea kusikiliza kesi yao mbele ya Jaji Mustapha Siyani, baada ya Jaji Elinaza Luvanda kujitoa kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo ilisimama kwa siku nne kutokana na Jaju Luvanda kujitoa kuisikiliza baada ya washtakiwa kutokuwa na imani naye kwamba hawaamini kama atawatendea haki baada ya kutupilia mbali mapingamizi waliyoweka.

Mbowe anashtakiwa pamoja na Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.


Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5, 2020.