Mahakama yawaita akina Mbowe kesi yao iendelee leo

Mahakama yawaita akina Mbowe kesi yao iendelee leo

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetoa hati kumwita Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kuendelea kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.


Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetoa hati kumwita Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kuendelea kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Mbowe na wenzake wanatakiwa kuwa mahakamani hapo leo baada ya kesi yao kusimama kwa siku nne kutokana na Jaji Elinaza Luvanda kujitoa kuisikiliza. Jaji huyo alijitoa Jumatatu baada ya washtakiwa kutokuwa na imani naye kwamba hawaamini kama atawatendea haki baada ya kutupilia mbali mapingamizi waliyoweka.

Mahakama sasa imemteua Jaji Mustapha Siyani kusikiliza kesi hiyo. Kwa mujibu wa hati ya wito, kesi itaendelea leo mahakamani hapo kuanzia saa 3:00.

Jaji Siyani, aliyezaliwa Februari 25 mwaka 1977 ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amewahi kufanya kazi katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na akaapishwa kuwa jaji na Rais John Magufuli Aprili 2018.

Miongoni mwa kesi alizoamua akiwa jaji ni ya mauaji ya wanafamilia 17 wa Mgaranjabo huko Musoma mkoani Mara. Katika hukumu hiyo aliwatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa washtakiwa sita na kuwaachia huru watatu.

Jamhuri inatarajiwa kuwasilisha hati mpya ya mashtaka baada ya kufanya marekebisho yaliyoelekezwa na mahakama kutokana na kasoro zilizobainika, kisha washtakiwa wasomewe tuhuma zao kwa mara ya kwanza.

Mbowe anashtakiwa pamoja na Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya ambao wote ni makomandoo waliofukuzwa kazi jeshini kutokana na sababu mbalimbali. Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka jana.

Vilevile wanatuhumiwa kupanga vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko na kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.