Jaji Luvanda ajitoa kesi ya Mbowe na wenzake, atoa maelekezo

Muktasari:

  • Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, amejitoa kusikikiza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Dar es Salaam. Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, amejitoa kusikikiza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi hapo mahakama hiyo itakapopangiwa Jaji mwingine na washtakiwa wataendelea kubaki rumande.

Jaji Luvanda ametoa maelekezo kuwa jalada la kesi hiyo lipelekwe kwa msajili kwa ajili ya kupangiwa Jaji mwingine.
Mbowe na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi.

Uamuzi wa kujitoa Jaji Luvanda kusikikiza kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 16/2021, umetokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, Freeman Mbowe kwa niaba ya wenzake kuwa hawana imani na Jaji huyo katika kutenda haki dhidi ya kesi yao.

Mbowe ametoa madai hayo leo Jumatatu Septemba 6, 2021 muda mfupi baada ya Jaji Luvanda kutupilia mbali mapingamizi mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa hao.


Jaji Luvanda ajitoa kesi ya Mbowe na wenzake, sasa kupangiwa jaji mwingine


Madai ya Mbowe

Mbowe amedai kuwa wanavyoona mwenendo wa kesi yao hawatatendewa haki, hivyo wanaomba Jaji ajiondoe kusikiliza shauri hilo.


"Nikizungumzia pingamizi la kwanza, ni ukweli usiopingika kuwa kesi hii inavuta hisia nyingi ndani ya jamii na itakuwa njema zaidi kama hatua zote za usikilizwaji wa kesi hii zitaonekana na kubaki kuwa vitafanyika kwa haki na weledi bila hisia zozote za uonevu," ameeleza Mbowe na kuongeza.

"Mheshimiwa Jaji hisia mbalimbali za jamii katika suala hili zinaweza kuthibitishwa katika mjadala mbalimbali inayoendelea katika mtandao wa kijamii Wikileaks ambayo kwa urahisi ningependa kuisoma mbele ya mahakama yako," ameeleza Mbowe na kisha kuisoma taarifa hiyo.


“Mheshimiwa Jaji naomba kunukuu taarifa hiyo...... 'Jaji Elinaza Luvanda ni Mserikali na Tiss, yupo Mahakama ya Mafisadi kimkakati, anaelekezwa kumfunga Mbowe huku msajili akishughulika na Chadema, Rais atamuachia baada ya muda kila pingamizi atalitupilia mbali, haijalishi uhalali wake,” mwisho wa kunukuu....alidai Mbowe.


Amedai kuwa maneno yaliyopo katika mtandao huo yanazungumzwa katika jamii, hivyo hayawezi kupuuzwa.
"Hivyo ni ombi langu ikikupendeza Jaji ujitoe kusikiliza kesi hii kwa ajili ya kulinda heshima yako na heshima ya mahakama na usibebeshwe lawama pengine usizosistahili," Mbowe alitoa ombi hilo.

Mbowe baada ya kutoa ombi hilo, Wakili wa Serikali  Mwandamizi, Robert  Kidanda alimshauri Jaji Luvanda kuzingati kanuni za kisheria katika hoja ya kina Mbowe kumtaka ajitoe, akisema kuwa Jaji hawezi kujitoa kwa hofu ya mshtakiwa/ washtakiwa.


Jaji Luvanda baada ya kupitia ombi la Mbowe na maelezo ya upande wa mashtaka, ametoa uamuzi kwa kusema kuwa amejitoa kusikiliza kesi hiyo.


"Nimesikiliza ombi la mshtakiwa wanne katika kesi hii( Mbowe) na mawakili wa upande wa mashtaka niseme tu ombi la Mbowe ni la msingi na lina maslahi mapana kwa umma licha ya kuwa malalamiko yake ni ya kudhani..hivyo nichukue fursa hii kukaa pembeni ili nimpishe Jaji mwingine aje achukue nafasi ya kuendelea na shauri hili, niwashukuru wote kwa ushirikiano na nawatakia kila la heri Insha'Allah," amesema Jaji Luvanda.


Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Luvanda aliahirisha kesi hiyo hadi hapo kesi hiyo itakapopangiwa Jaji mwingine na ameelekeza washtakiwa hao kurudishwa rumande.


Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, wa pili ni Adamu Hassan Kasekwa, wa tatu Mohamed Abdillahi Ling'wenya na wa nne Freeman Aikael Mbowe.


Washtakiwa hao wanatetewa na jopo la mawakili 14, likiongozwa na Peter Kibatala, huku upande wa mashtaka ukiwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.