Jaji Mkuu aomba bei ya mitandao ishuke

Muktasari:

  • Aeleza  umuhimu wa Tehama katika utendaji haki na kuomba Serikali kupunguza bei ya mitandao.  Pia, aeleza chanzo cha majaji kuvaa kanzu nyekundu.

Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameomba bei ya mitandao iendelee kushuka ili kuwezesha watumiaji wa mifumo ya mahakama kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), waweze kusomana.

 Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Februari Mosi, 2024 wakati akihutubia kwenye kilele cha Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini na maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu.

 “Ili taasisi za haki jinai ziweze kusomana, haina budi vile vile kusomana ndani ya taasisi, hamna maana kusomana na taasisi za nje wakati ndani hatusomani,” amesema.

Jaji Mkuu amesema uwekezaji wa mkongo wa Taifa umewezesha mahakama zikiwamo Mahakama za Mwanzo zaidi ya 900, Mahakama Kuu, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi kusomana na kubadilishana taarifa.

“Tumeweza hivyo kwa sababu ya uwekezaji ambao upo na tunachoomba zaidi ni bei ya mitandao iendelee kushika chini ili tuweze kusomana kwa uzuri zaidi,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema wasingeweza kutumia Tehama kama kusingekuwa na mkongo wa mawasiliano uliowezesha kuwa na Serikali mtandao kwa ajili ya mawasiliano ndani ya Serikali.

Joho jekundu la majaji

Jaji Mkuu pia amesema zaidi ya miaka 100 iliyopita kuna jaji mmoja wa kwanza kuja Tanganyika, alifungua Mahakama Kuu na alikuwa amevaa joho jekundu.

Amesema jaji huyo kutoka Ulaya, alifungua Mahakama Kuu Dodoma na alipofika alikuwa amevaa joho jekundu, wananchi walijua ni kanzu kwa hiyo wakamwita ni jaji mwenye kanzu nyekundu na ndio maana hadi leo majaji bado wanavaa kanzu nyekundu.

Jaji Mkuu amesema jaji huyo alileta haki Dodoma kwa njia ya reli iliyojengwa na Mjerumani. “Yeye alileta haki Dodoma kwa kutumia reli au uwekezaji wa reli uliofanywa na Mjerumani, alifika hapa, lakini karne ya 21 uwezeshaji wa haki unafanywa na Tehama na ndio maana tunaishukuru Serikali kwa uwekezaji ambao umeufanya katika hii miaka ya hivi karibuni katika mifumo ya Tehama,” amesema.