Jaji Mkuu azungumzia udhaifu mfumo sheria nchini
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma
Muktasari:
- Wadau wa sheria nchini wamebainisha changamoto zinazokwamisha mafanikio ya kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi
Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema mfumo wa sheria nchini unahitaji kuangaliwa na kufanyiwa maboresho akisema una tatizo kubwa, kutokana na kuwa na kona kona za michakato na mlolongo mrefu.
Profesa Juma amesema hayo katika hafla ya utoaji tuzo kwa wadau wa usuluhishi, waliofanikisha mashauri mengi kumalizika kwa njia ya usuluhishi mwaka 2023.
Tuzo hizo zilizoandaliwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Usuluhishi, zimetolewa kwa mara ya kwanza jana jioni, Jumanne, Januari 16, 2024, katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Hafla hiyo ya utoaji wa tuzo hizo pia imekwenda sambamba na uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa utatuzi migogoro kwa njia mbadala na mjadala wa wadau kuhusiana na sheria na changamoto za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Profesa Juma amesema moja ya maboresho muhimu katika karne ya 21 ni matumizi ya usuluhishi kutatua migogoro kwa kuwa ni sheria za jinai na hata za madai zilitungwa tangu karne ya 19.
Amesema sheria hizo zina kona nyingi kwa kuwa kesi inaweza kukamilika lakini mtu mwingine akarudi tena mahakamani kuweka mapingamizi.
"Kuna tatizo kubwa sana katika mifumo ya sheria zetu kwa kuwa ina michakato na konakona nyingi na kwamba bahati mbaya taaluma ya sheria imejengwa katika hizo kona maana ndizo zinawapatia mawakili chakula," amesema Profesa Juma.
"Hivyo, kuna haja ya kuangalia sheria zetu zote. Tuna maeneo mengi ya kuangalia mfumo wetu wa sheria. Wenzetu wa elimu wameangalia mfumo wa elimu sisi mfumo wa sheria hatujafanya. Hata marekebisho ya sheria tunayoyafanya tunafanya vipandevipande."
Awali, Mkufunzi Mkuu wa Shule ya Sheria kwa Vitendo (LST), Profesa Clement Mashamba amesema kuna aina 10 za sheria zinazoanzisha usuluhishi na kanuni mbalimbali lakini tatizo hazina umoja.
Pia, amesema kuna tasisi nyingine zinafanya usuluhishi huohuo lakini kwa namna tofauti hivyo, kuna haja ya kuzirekebisha.
Amesema ingawa usuluhishi ni suala la kisheria na ni njia rahisi ya kutatua migogoro, bado mawakili wengi hawaitumii kwa sababu mara nyingi hawafundishwi vyuoni na pia bado mawakili wana hofu ya kukosa mapato.
Hivyo, ameshauri vyuo vianzishe hilo somo katika mitalaa yake.
Profesa Mashamba amesema pia bado kuna tatizo la wataalamu wa usuluhishi huku akishauri Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Jaji Mkuu na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuangalia namna ya kuwajengea uwezo.
"Ofisi ya Mwanaheria Mkuu wa Serikali na ya Wakili Mkuu wa Serikali mna jukumu la kuisaidia Serikali kumaliza migogoro kwa njia mbadala maana hawa tunaogombana nao bado tunahitajiana," amesisitiza Profesa Mashamba.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, George Mandepo amesema kuna taasisi zinazotajwa kwenye Sheria ya Usuluhishi kwamba kuna vyombo vimeanzishwa lakini havina wataalamu.
Rais wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Madeline Kimei amesema kuwa licha ya kuwepo kwa sheria, pengo lililopo ni kutokuwepo kwa sera ya usuluhishi.
Pia, amesema aina ya mafunzo wanayopewa wanasheria kazi yao ni kuwawakilisha wateja wao mahakamani tu jambo ambalo amesema ni moja ya tatizo.
"Hivyo sheria inapaswa irekebishwe ili pamoja na mambo mengine iweze kujibu swali la kwanini siyo upatanishi," amesema Kimei.
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Serikali, Lukas Makumde amesema hata waliopewa jukumu la kusaidia kupatikana kwa suluhu wakiwamo mawakili wa kujitegemea na hata wasuluhishi wakati mwingine wanachangia suluhu isipatikane.
Amesema kuna kazi ya kufanya kuwarejeshea imani wananchi waliokuwa wamekata tamaa kuhusiana na usuluhishi na hata wasuluhishi wanahitaji kupatiwa mafunzo.
Rais wa TLS, Harold Sungusia amesema mawakili licha ya kusimama haki kama maofisa wa Mahakama lakini pia ni wafanyabiashara.
Amesema kwa jinsi walivyofundishwa utaalamu wa kutumia sheria, wakili anapopambana kwa hoja za kisheria mahakamani ndipo anaonesha umahiri na umwamba wake na hivyo kuaminika kwa mteja.
"Hivyo, kuna dhana kwamba kama wakijifungia tu katika chumba kupata usuluhishi umaarufu wake utapotea na hata kipato," amesema Sungusia.
Pia, amesema kuna wateja wengine hawataki kabisa kusikia habari ya usuluhishi wakisema kama wanaona wakienda mahakamani wanauhakika wa kushinda kwa nini aende kwenye usuluhishi.
Sungusia amesema kuna haja ya kutoa elimu ya kubadili moyo kwa kuwa usuluhishi unategemea na moyo wa mtu na kwamba mitalaa ya mafunzo inabidi iwafundishe watu kuwa si aina moja tu ya kutatua migogoro yaani kupambana kwa hoja za kisheria bali kuna usuluhishi.
Sungusia amesema wamekuwa wakishauri hata migogoro mingine ya kibiashara badala ya kuikimbiza mahakamani ni vema ikaenda kwenye usuluhishi kwa kuwa inakuwa na athari kubwa hata kwa uchumi wa nchi.
"Tume ya kurekebisha sheria ina jukumu kubwa sana kufanya hata utafiti kuona taratibu mbalimbali zinazoweza kutumika katika kutatua aina fulani ya migogoro kwa usuluhishi," amesema Sungusia.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi amesema mawakili ndio watu wa kwanza kuwajenga wateja wao kwa kuwashauri kwenda kwenye usuluhishi.