Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaji Mkuu Tanzania ataja alama za haki alizoziacha Jaji Kisanga

Jaji Mkuu wa Tanzania,Profesa Ibrahim Juma (kulia) akizindua kitabu cha hayati Jaji Robert Kisanga jijini Dar es Salaam leo Januari 23, 2024. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mahakama imezindua kitabu cha historia ya maisha ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Robert Kisanga, huku wadau wakibainisha mchango wake katika nyanja ya sheria na alama alizoziacha.

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amemuelezea marehemu Jaji wa Mahakama ya Rufani, Robert Kisanga kuwa alikuwa mwalimu wa utawala wa sheria na haki za binadamu, huku akieleza mchango wake katika nyanja ya sheria kwa ujumla.

 Profesa Juma amebainisha mchango huo wa marehemu Jaji Kisanga wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachoelezea historia ya maisha ya jaji huyo na utumishi wake, kiitwacho" Ndoto iliyotimia; Maisha ya Jaji Robert Kisanga, leo Jumanne, Januari 23, 2024.

Hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho iliyokwenda sambamba na kumbukizi ya kifo cha Jaji Kisanga imeandaliwa na Taasisi ya Uongozi wa Mahakama (IJA) ambayo pia ndio iliyotayarisha kitabu hicho, imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Jaji Kisanga alizaliwa katika Kijiji cha Fukeni katika Halmashauri ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, Juni 20, 1933, alifariki dunia Januari 23, 2018 katika Hospitali ya Regency, jijini Dar es Salaam.

Kitabu chake hicho kilichozinduliwa leo, chenye kurasa 378 kinaelezea maisha ya jaji huyo tangu alipozaliwa, maisha ya shule, kazi zake za uanasheria wa Serikali, ujaji na mchango wake katika tasnia nzima ya sheria na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Katika hotuba yake, Profesa Juma amesema kitabu hicho kina umuhimu kwa sababu kinabeba historia ya taasisi muhimu kama Mahakama, Kamisheni ya Haki za Binadamu na Tume ya  Haki za Binadamu na Utawala Bora na kwamba mahakama ina mengi ya kujifunza.

"Jaji Robert Habesh Kisanga ameacha alama isiyofutika, zaidi kwenye mchango wa haki, ameacha alama yenye wino isiyofutika katika Katiba ya Tanzania hususan katika mchango wake kwenye mabadiliko ya 13 na ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2004," amesema Profesa Juma.

Amefafanua kuwa mabadiliko hayo yaliyotokana na maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na Kamati ya Jaji Kisanga kuhusu hoja 19, kupitia waraka wa Serikali namba 1 wa mwaka 1998 yaani White paper.

Amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji wa maoni hayo ilianza na mabadiliko ya 13 ya Katiba yaliyopitishwa na Bunge mwaka 2000, yaliyolenga kuimarisha demokrasia hasa mchakato wa uchaguzi.

Profesa Juma amesema awamu ya pili ya utekelezwaji wa maombi hayo ilihusisha mabadiliko ya 14 ya Katiba yaliyokuwa na shabaha ya kuhakikisha kwamba Ibara za Katiba zinazohusu haki za binadamu na wajibu ulioainishwa katika Katiba zinaandikwa vizuri, ili kulinda na kuhifadhi haki hizo kwa kuzingatia maoni ya wananchi.

"Moja ya alama kubwa zilizoletwa na Jaji Kisanga kupitia mabadiliko ya 13 ni kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ilianzishwa chini ya Ibara ya 129", amesema Profesa Juma na kuongeza;

"Na Jaji Kisanga ameacha alama nyingine baada ya Rais Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) kumteua mwaka 2002 kuanzisha taasisi mpya kabisa Tanzania kama Mwenyekiti wa kwanza wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.”

Pia Jaji Mkuu amesema kuwa ripoti ya Tume ya Jaji Kisanga kuhusu ajali ya MV Bukoba, pia ilileta mabadiliko mengi katika usalama wa vyombo vya usafiri majini.

"Nyayo za Jaji Robert Habesh Kisanga zimetapakaa katika michango ya aina nyingi ambayo ilileta mabadiliko na maboresho katika maisha ya Watanzania," amesisitiza Jaji Mkuu.

Amesema kuwa wa kusoma kitabu hicho ni wazi Jaji Kisanga alikuwa akiishi maisha yenye malengo na kwamba alilenga sheria na ndio maana hata alipopata nafasi ya kufanya kazi yenye maslahi makubwa Benki Kuu ya Tanzania, aliacha na kwenda kuwa Wakili wa Serikali na kuitumikia sekta ya sheria.

"Sisi tunamshukru kuja huku maana tumeona mchango wake umekuwa mkubwa sana kuliko kama angekwenda Benki Kuu," amesema Profesa Juma.

Hukumu zilizoacha historia

Kwa upande wake, mjumbe wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Dk Fauz Twaib ambaye pia ni mmoja wa wahariri wa kitabu hicho, amebainisha kuwa hukumu za Jaji Kisanga katika kesi mbalimbali zimesababisha marekebisho ya sheria mbalimbali.

Miongoni mwa hukumu hizo akiwa ama Mwenyekiti wa jopo au sehemu ya jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani ni pamoja na kesi ya Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (Juwata) dhidi ya Kiwanda cha Uchapaji Tanzania (Kiuta).

Amesema kuwa katika hukumu hiyo, Mahakama ya Rufani iliamua uwezekano wa Mahakama kuondoka katika uamuzi wake ya awali kwa kuangalia upya uamuzi huo kama kuna kosa ililolifanya.

Amesema kuwa katika hukumu hiyo, Mahakama hiyo katika jopo la majaji akiwemo Jaji Kisanga ilikubaliana na hoja za kina Profesa Issa Shivj kuwa kama kuna makosa katika uamuzi wa awali, kuna haja kubadilisha uamuzi wa awali.

Hukumu hiyo iliibua marekebisho ya sheria ili kuiruhusu Mahakama pale inapobaini kosa, iweze kubadilika na kuchukua msimamo tofauti.

Kwa mujibu wa Dk Twaib, kesi nyingine ni ile ya ubunge baina ya Jaji Joseph Sinde Warioba dhidi ya Steven Wasira, ambayo Jaji Kisanga ndio alikuwa mwenyekiti wa jopo la majaji.

"Hii kesi iliifanya Mahakama ya Rufani iangalie uwezo wake wa kuweka maneno ndani ya sheria ambayo yalionekana yalipaswa kuwekwa, lakini Bunge halikuyaweka," amesema Dk Twaib.

Dk Twaib amezitaja kesi nyingine kuwa ni ile ya Kukutia Mohamed dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambayo ilihusu masuala ya haki za binadamu na kwamba mahakama hiyo katika jopo la kina Jaji Kisanga ilisema Mahakama ina wajibu kutafsiri sheria hizo kwa namna ya kulinda haki za binadamu.

Vilevile Jaji Dk Twaib amezitaja hukumu ya kesi ya Julius Isengoma Ndyanabo dhidi ya AG, kuhusu dhamana ya Sh5 milioni anayopaswa kuweka kwanza kabla mgombea au mtu kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge mahakamani.

Katika hukumu hiyo, DkTwaib amesema  Mahakama ya Rufani katika jopo la kina Jaji Kisanga ilikubaliana na Ndyanabo kuwa ni kinyume cha sheria na matokeo yake sheria hiyo imebadilishwa na kutoa fursa anayefungua kesi anaweza kuomba kupunguziwa kiwango hicho au kuondolewa kabisa kama mahakama ikijiridhisha kuwa hana uwezo wa kuipata.

Kauli ya mjane

Kwa upande wake, mjane wa marehemu Jaji Kisanga, Maria Ezra Kisanga amesema wanamkumbuka Jaji Kisanga kwa mengi yakiwemo upendo, uvumilivu, huruma, uadilifu uchapakazi na kupenda watu.

"Alikuwa mtu wa msimamo aliyejali umoja na kuzingatia utaratibu, tunamshukru Mungu kwa karama alizompa," amesema Mama Kisanga.

Pia amemshukru Jaji Mkuu kwa kukubali wazo la familia la kuandikwa kitabu cha maisha yake.

"Kwa kuwa marehemu alitumia muda mwingi mahakamami, niliamini Mahakama ndio itakuwa chombo sahihi kufanya kazi hiyo ndipo niliwasiliana na jaji mkuu kuhusu kufanya kazi hiyo naye aliafiki na kuahidi kufanya kazi hiyo," amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa IJA, Jaji Dk Gerald Ndika amesema mbali na historia ya maisha ya Jaji Kisanga, pia kitabu hicho kinatoa historia ya Mahakama na taasisi nyingine ambazo Jaji Kisanga alihudumu.

"Kitabu hiki kitakuwa nyenzo kwa wanafunzi wa sheria, wanasheria na wananchi kwa jumla", amesema Dk. Ndika.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya sheria wakiwemo majaji na majaji wakuu wastaafu, majaji walioko katika utumishi akiwemo Jaji Mkuu wa Zanzibar, mawakili wa Serikali, mawakali wa kujitegemea na wadau wengine kutoka taasisi mbalimbali.