Prime
Jambo jipya laanzishwa WhatsApp
Muktasari:
- Kuanzia jana Jumatatu Juni 29, 2026 watumiaji wameanza kupewa fursa ya kuhifadhi majina yao (username) na kuyatumia rasmi badala ya namba.
Dar es Salaam. Ni rasmi watumiaji wa mtandao wa WhatsApp wameanza kusajili na kuhifadhi utambulisho wa majina yao ‘Username’ kuanzia Juni 29, 2026 ili kuyatumia badala ya namba zilizozoeleka.
Hatua hiyo inafuatia baada ya kampuni ya Meta inayomiliki WhatsApp kutangaza mfumo huo unaolenga kuongeza faragha na usalama wa mawasiliano.
Hivyo si lazima mtu awe na namba yako ili akupate WhatsApp, bali akiwa na ‘username’ yako tu ataweza kukufikia kama ilivyo katika mitandao kama Telegram.
Mabadiliko hayo moja ya maboresho makubwa ya faragha kuwahi kufanywa na WhatsApp tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2009, ambapo kwa sasa inasubiriwa huduma kuanza kusambazwa baada watumiaji kusajili majina yao.
Meta inasema uamuzi wa kuanzisha mfumo huo umetokana na uhitaji wa watumiaji wengi, ambao wamekuwa wakitaka kuwasiliana na watu wapya bila kulazimika kufichua namba zao za simu, hususan wanapojiunga kwenye makundi sogozi ya shule, kazi, michezo au shughuli nyingine za kijamii.
"Kutoa namba ya simu wakati mwingine ni hatua kubwa kwa sababu namba hiyo imeunganishwa na maeneo mengi ya maisha ya mtu. Wakati mwingine unahitaji kuzungumza na mtu bila kutoa namba yako," imeeleza kampuni hiyo katika tovuti yake rasmi.
WhatsApp yenye zaidi ya watumiaji bilioni tatu duniani, imesema mfumo wa username ni hatua mpya ya kuimarisha faragha ya watumiaji wake.
Tofauti na mitandao mingine ya kijamii, WhatsApp haitakuwa na orodha ya kutafuta majina ya watumiaji. Hii ina maana kuwa mtu atalazimika kujua ‘username’ sahihi, ndipo aweze kuanzisha mawasiliano kwa mara ya kwanza.
Username haipatikani kirahisi
Katika kuboresha zaidi faragha, kampuni hiyo imeweka chaguo la ziada la usalama litakalowaruhusu watumiaji kuweka "ufunguo wa username" (username key), ambao mtu mwingine atalazimika kuujua kabla ya kutuma ujumbe.
Meta imesema mara mfumo huo utakapoanza kufanya kazi, mtu au biashara utakayowasiliana nayo kwa mara ya kwanza haitaona tena namba yako ya simu iwapo utakuwa umewezesha matumizi ya username.
Kwa watumiaji wa kawaida, kampuni imewashauri kuchagua majina yatakayojulikana na watu wanaotaka tu kuwasiliana nao. Pia imeweka huduma ya kutengeneza mapendekezo ya username kwa wale watakaoshindwa kupata jina linalofaa.
Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo, watengeneza maudhui na taasisi, Meta imesema wamepewa nafasi ya kudai (claim) majina yaleyale wanayotumia kwenye Instagram au Facebook, ili kudumisha utambulisho mmoja katika majukwaa yote ya kampuni hiyo.
Watumiaji wenye akaunti za Instagram au Facebook wataweza kupewa kipaumbele cha kuhifadhi majina yanayofanana ili kupunguza uwezekano wa kuigwa na matapeli.
Watumiaji wanaotaka kuhifadhi username wanapaswa kupakua toleo jipya la WhatsApp, kisha waingie kwenye settings, wafungue sehemu ya account, halafu wachague username.
Meta imesema usambazaji wa huduma hiyo utafanyika hatua kwa hatua kuanzia sasa na watumiaji watapokea taarifa ndani ya WhatsApp pindi huduma hiyo itakapopatikana katika nchi zao.