Jamii yahimizwa kusaidia watoto wanaoishi mazingira magumu
Muktasari:
- Jamii imeshauriwa kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ili kukabiliana na wimbi la watoto kuzurura mitaani ovyo ambapo baadhi yao hujikuta wakijiingiza kwenye makundi ya kihalifu hali ambayo inahatarisha usalama wao.
Moshi. Jamii imeshauriwa kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ili kukabiliana na wimbi la watoto kuzurura mitaani ovyo ambapo baadhi yao hujikuta wakijiingiza kwenye makundi ya kihalifu hali ambayo inahatarisha usalama wao.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kata ya Bondeni iliyopo Manispaa ya Moshi, John Hamaro wakati akikabidhi misaada mbalimbali ya vyakula na mavazi katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Selengia.
Amesema kwa sasa kuna wimbi kubwa la watoto wa mitaani kutokana na baadhi ya wazazi na walezi kuwatelekeza kutokana na ugumu wa maisha na kusababisha baadhi yao kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya na wengine wakifanyiwa vitendo vya ukatili.
"Sisi kama jamii tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha hawa watoto wanasaidika, watoke huko walipo ili tuweze kuokoa kizazi kijacho,hivyo katika kutekeleza hilo nimeungana na wananchi wa kata hii, tumeguswa kuwasaidia hawa watoto ambapo wapo katika vitu hivi,ambapo leo tumewaletea vyakula pamoja na mavazi." Amesema Hamaro na kuongeza.
"Tumefanya hivyo ili na wao wasione kwamba wamesahaulika, hawa ni watoto wetu tuwasaidie na hiki ambacho tunakifanya leo ni kwamba tunamsaidia Rais wetu Samia Suluhu Hassan katika kuisaidia jamii."
"Kwa umoja wetu wa chama cha Mapinduzi kata ya Bondeni tunaendelea kutekeleza ahadi za chama pamoja na kuunga mkono jitihada zinzazofanywa na Rais Samia za kuisaidia jamii hasa zinazoishi katika maizngira magumu." amesema Hamaro.
Mwenyekiti huyo ameiomba jamii ndugu jamaa na marafiki kuendelea kushirikiana kusaidia watoto kama hawa ambao wengi wao wameachwa yatima kutokana na sababu mbalimbali na wengine hawana uwezo wa kuwasaidia watoto wao na kuwatelekeza.
Akishukuru kwa misaada hiyo Mkurugenzi wa kituo hicho, Swalehe Mkilindi amesema baada ya kuona watoto wengi wako mtaani na hawana msaada wowote aliamua kuanzisha kituo hicho ili kuwasaidia kwa kushirikiana na wadau.
"Tunashukuru misaada hii ambayo tumeletewa leo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wetu hii ni zawadi kubwa, tunamshukuru Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi kata ya Bondeni kwa kuja hapa na kuona tunaouhitaji mkubwa wa chakula na mavazi kwa hawa watoto wetu tunaowalea hapa." Amesema Mkilindi.
Amesema uwepo wa kituo hicho cha kulelea watoto hao ni kwa ajili ya kupunguza hatari za watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima za kufanyiwa matukio hatari ya kikatili pamoja na kujiingiza kwenye makundi hatarishi.