Japan, UNFPA kushirikiana kuzuia vifo vya uzazi kambi za wakimbizi

Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) wakitiliana saini makubaliano ya ufadhili wa mradi wa kuwasaidia wakimbizi huduma za uzazi mkoani Kigoma . Hafla hiyo imefanyika leo nyumbani kwa Balozi Misawa, Dar es Salaam. Picha na Peter Elias

Muktasari:

Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Schreiner katika mradi huo wa miezi 12 unaotarajiwa kuwanufaisha watu 113,000 wakiwamo wanawake, wenye walemavu na rika balehe kwenye kambi za wakimbizi

Dar es Salaam. Ubalozi wa Japan nchini Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu linaloshughulikia Afya ya Uzazi (UNFPA) zimetiliana saini makubaliano ya ufadhili wa kuwasaidia wakimbizi wenye thamani ya Sh921 milioni.

Ufadhili huo utahusisha kusaidia shughuli za kuokoa maisha ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi katika kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta wilaya za Kasulu na Kibondo pamoja na wenyeji waishio karibu na kambi hizo mkoani Kigoma.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Januari 31, 2024 kati ya Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Schreiner katika mradi huo wa miezi 12 unaotarajiwa kuwanufaisha watu 113,000 wakiwamo wanawake, wenye walemavu na rika balehe kwenye kambi hizo.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Balozi Misawa amesema Japan imejitolea kuboresha afya za watu duniani kote.

Amesema Serikali yao imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuzingatia afya ili kuhakikisha mazingira bora ya maisha pamoja na ukuaji wa Afrika.

“Nchini  Tanzania, Japan inashirikiana kikamilifu kuimarisha huduma ya afya kupitia misaada mbalimbali. Chini ya Shirika la Jica kwa huduma za uzazi na watoto wachanga, tunalenga kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa na wataalamu wa afya,” amesema Balozi Misawa.

Ameipongeza UNFPA kwa kuhakikisha vifo vya uzazi katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu vinapungua na kwa takwimu za mwaka 2022, shirika hilo limepata vifo sifuri katika kambi hiyo yenye wakimbizi 130,000.

“Haya ni mafanikio makubwa, hata hivyo, wimbi la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) lililoanza mwaka 2023 lilileta changamoto kwa huduma bora za afya katika kambi za wakimbizi,” amesema Balozi Misawa.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Tanzania, Schreiner ameishukuru Japan kwa ufadhili huo akisema watakuwa tayari kutoa huduma kwa wanawake na wasichana mkoani Kigoma.

“Tunashukuru Japan kwa kufadhili jitihada hizi, UNFPA inatoa huduma ya kuokoa maisha kwa wanawake na wasichana katika kambi za Nyarugusu na Nduta zinazosimamiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Schreiner.

Amesema kwa wastani, kambi za Nyarugusu na Nduta hushuhudia takriban mimba 2,004 kila mwezi, huku wanawake 201 wakikumbana na matatizo ya afya ya uzazi na mimba kuharibika.

UNFPA inashirikiana na washirika wake wa utekelezaji wa jamii inayozunguka kambi za wakimbizi Kigoma ambao ni Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma (Ras Kigoma) na Kampuni ya Borderless Japan Corporation.

Mtendaji Mkuu wa Borderless Tanzania Limited, Moana Kikuchi amesema alijitolea kufanya kazi Tanzania ili kusaidia jamii na katika mradi huo watatoa taulo za kike kwa wakimbizi 3,000 na wanawake 3,000 wengine wanaoishi karibu na kambi kwa mwaka mzima.

“Ninatambua changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu. Nilikutana na msichana mmoja ambaye alipata mimba akiwa bado shule, alipata shida sana, nilimsaidia akaendelea na masomo, sasa anafanya kazi kwangu,” amesema Kikuchi.