Jela mwaka mmoja kumchoma mwanaye kwa kudokoa dagaa

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Somoe Mohamed (34) kwa kosa la kumjeruhi mtoto wake wa miaka mitano kwa kumchoma moto viganja vya mikono yake baada ya kuiba dagaa.

Mtwara. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Somoe Mohamed (34) kwa kosa la kumjeruhi mtoto wake wa miaka mitano kwa kumchoma moto viganja vya mikono yake baada ya kuiba dagaa.

Shtaka hilo lilosomwa na Wakili wa Serikali Gidion Magesa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mtwara, Lucas Jang’andu na mwanamke huyo amekutwa na hatia.

Somoe ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Namanjele, Kata ya Dihimba Wilaya ya Mtwara Vijijini, amehukumiwa kosa hilo kinyume na kifungu cha 225 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, mahakama ingeweza kumfunga hadi miaka saba jela ambapo hakimu huyo amempunguzia adhabu mpaka mwaka mmoja baada ya kujutia kufanya kosa hilo.