Jela mwaka mmoja, wizi wa kuku 15
Muktasari:
- Mahakama ya Mwanzo Chato imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja Thomas Kitunga baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuiba kuku 15 wenye thamani ya Sh290,000 mali ya Mkuu wa upelelezi wa Polisi Chato, Daniel Mkoma.
Chato. Mkazi wa kijiji cha Kalema Wilaya ya Chato mkoani Geita, Thomas Kitunga (38) amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuiba kuku 15 wenye thamani ya Sh290,000 mali ya Daniel Mkoma, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilayani humo.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Chato, Yahaya Yassin baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Akitoa hukumu hiyo hakimu Yassin ameeleza kuridhishwa na ushahidi wa mlalamikaji Daniel Mkoma pamoja na wa mshItakiwa ambaYe alikiri mwenyewe kwa kinywa chake kutenda kosa hilo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Januari 29,2024 saa tisa usiku huko kwenye kijiji cha Mkuyuni kata ya Chato, mshitakiwa aliiba kuku 15 baada ya kuvunja banda na alipokamatwa alikua na kuku 14 walioko hai na mmoja alikua amekufa.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa kinyume na kifungu cha 265 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Akitoa hukumu hiyo hakimu Yassin amedai imezingatia historia ya mshitakiwa ambaye amekuwa na rekodi ya makosa ya uhalifu wa mara kwa mara .
Alipopewa nafasi ya ungamo mshitakiwa aliiomba Mahakama kumsamehe kwa kuwa ana familia inayomtegemea .
Hakimu Yassin alidai ametoa hukumu ya mwaka mmoja kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za wizi .