Prime
Jeshi la Polisi ladai mwanafunzi alitolewa mahari ng’ombe 15

Shinyanga. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amedai kuwa mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne mwaka jana ambaye wazazi wake waliamua kumuoza alilipiwa mahari ya ng’ombe 15.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mwanafunzi huyo aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na wazazi wake kuamua kumuozesha, kamanda Magomi alisema: “Baada ya mahojiano na baadhi ya wanaoshikiliwa, tumebaini kuwa wazazi wa mwanafunzi yule walipokea mahari ya kati ya ng’ombe 14 hadi 15 kutoka familia ya kijana aliyekuwa anamuoa binti yao”.
Kamanda alisema hadi jana, mume mtarajiwa, mshenga na ndugu mmoja walikuwa wanashikiliwa na polisi huku mwanafunzi huyo akiwa chini ya uangalizi maalumu.
“Hadi sasa, wazazi waliopokea mahari na kukubali kumuozesha binti yao ambaye bado ni mwanafunzi hawajajisalimisha polisi kama alivyoagiza mkuu wa mkoa, tunaendelea kuwatafuta,’’ alisema Kamanda Magomi.
Hata hivyo, ndoa ya mwanafunzi huyo iliyopangwa kufungwa Juni 17 mwaka huu ilizuiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme kuingilia kati kwa kuagiza maharusi na wasimamizi wao kutiwa mbaroni.
Mndeme akiongoza wajumbe wa kamati ya usalama na wataalamu wa sheria, alizuia ndoa ya mwanafunzi huyo wakati sherehe zikiwa zinaendelea katika Kijiji cha Mwawaza, huku umati wa watu ukibaki na butwaa.
Kiongozi huyo na ujumbe wake, walikuwa kijijini hapo kutekeleza kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, ndipo walipopata taarifa za siri za ndoa hiyo na kuingilia kati.
Mwanafunzi huyo alihitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Mwawaza.