Jeshi la Polisi lahimiza ushirikiano na kampuni za ulinzi binafsi
Muktasari:
- Kampuni za ulinzi binafsi zimetakiwa kuongeza ufanisi na kuwekeza zaidi katika teknolojia, mafunzo kwa watumishi wao, kufuata sheria na kuzingatia haki za binadamu ili kupunguza malalamiko wakati wa utoaji wa huduma
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetoa wito wa ushirikiano wa karibu kati ya polisi na kampuni binafsi za ulinzi kwa lengo la kupunguza matukio ya uhalifu pamoja na kudumisha amani nchini.
Wito huo umetolewa na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Ulrich Matei wakati wa hafla maalumu iliyoandaliwa na Kampuni ya Ulinzi ya SGA Tanzania iliyolenga kuwaaga watumishi wa kampuni hiyo waliostaafu na kuwatambua wafanyakazi walioitumikia kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 20 kupitia programu inayojulikana kama Club 20.
Hafla hiyo ilifanyikia katika Bustani ya Hekima jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuhudhuriwa na wawakilishi mbalimbali kutoka Jeshi la Polisi, Baraza la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), uongozi na wafanyakazi wa SGA pamoja na wageni wengine waalikwa.
Naibu Kamishna wa Polisi, Ulrich Matei (wa pili kushoto) akisaidiana na wanachama wa Club 20 wa SGA kukata keki wakati wa shughuli ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu na kuwatambua wafanyakazi walihudumia kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 20.
Matei amesema sekta binafsi katika ulinzi pia ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa salama huku akitoa wito kwa wastaafu walioagwa kuendelea kutoa michango na uzoefu wao ili amani iliyoko hapa nchini iendelee kutamalaki.
Ameupongeza uongozi wa SGA kwa kuendelea kuthamini michango inayotolewa na wafanyakazi wake sambamba na kuhakikisha ustawi wa watumishi wa kampuni hiyo.
“Kampuni nyingi huwa hazizingatii maagizo yanayoelekeza kampuni binafsi za ulinzi kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kiutendaji watumishi wao kupitia mafunzo, uhakiki, usimamizi na maboresho ya mishahara; kwa SGA niwapongeze kwa kujitahidi kutekeleza maagizo haya, ninyi ni mfano mzuri wa kuigwa na makampuni mengine,” amesema.
Pia, amepongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kuwa na utaratibu wa kuwapongeza wafanyakazi waliofanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 na kuongeza kuwa, watumishi 95 kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 ni jambo linalostahili kusherehekewa na kupongezwa.
Ametoa wito kwa kampuni za ulinzi binafsi kuongeza ufanisi na kuwekeza zaidi katika teknolojia, mafunzo kwa watumishi wao, kufuata sheria na kuzingatia haki za binadamu ili kupunguza malalamiko wakati wa utoaji wa huduma.
Matei ameahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ushirikiano wake wa dhati kwa kampuni binafsi akisema ni muendelezo wa ushirikiano huo kwa miaka mingi iliyopita.
Akizungumza kwa niaba ya SGA Tanzania, Mkuu wa kitengo cha fedha cha kampuni hiyo, Jonathan Geleta ameushukuru uongozi wa Jeshi la Polisi kwa ushirikiano ambao jeshi hilo limetoa kwa kampuni binafsi za ulinzi hapa nchini.
"Nichukue fursa hii kwa niaba ya uongozi wa SGA kuahidi kuwa kampuni yetu itaendelea kufuata miongozo na kanuni zote kama zinavyotolewa na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha ufanisi katika kutoa huduma zetu ndani ya jamii,” amesema Geleta.
Amewapongeza wastaafu kwa huduma yao bora waliyotoa wakati wakiitumikia kampuni hiyo.