Upelelezi sakata la Hamza hadi nje ya nchi

Jeshi la Polisi laibuka na mapya ya Hamza

Muktasari:

  • Zikiwa zimepita siku 15 tangu Hamza Mohammed (30) auawe, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wa kina unaendelea kufanyika dhidi ya tukio hilo.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku 15 tangu Hamza Mohammed (30) auawe, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wa kina hadi nje ya nchi unaendelea kufanyika dhidi ya tukio hilo.

Hamza aliuawa Agosti 25 mwaka huu nje ya geti la Ubalozi wa Ufaransa katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, baada kufanya shambulio la kurusha risasi na kuua askari wanne, akiwamo mmoja wa kampuni ya ulinzi na kujeruhi wengine sita.

Muliro alisema upelelezi huo unafanyika ndani na nje ya familia.

Pia, alisema wanafanya upelelezi mwingine ndani na nje ya nchi, licha ya ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kudai kuwa upelelezi umebaini Hamza alikuwa ni gaidi wa kujitoa mhanga.

Kamanda Muliro alisema hayo alipozungumza na Mwananchi jana muda mfupi baada ya ndugu wa karibu wa Hamza kuiambia Mwananchi kuwa watu watano waliokuwa wanashikiliwa na polisi bado hawajaachiwa.

“Bado hawajaachiwa lakini acha tuone huenda leo watatoka, tutawafahamisha,” alisema ndugu huyo.

Alipoulizwa kuhusu watu hao, Muliro alisema polisi wanaendelea kufuatilia kwa kina tukio hilo kwa kuzingatia uzito wake.

“Kwa jinsi tulivyojaribu kuhoji watu mbalimbali niseme bado tunalifuatilia. Upelelezi wa tukio hili unaendelea na tunaliangalia kwa kina ndani na nje ya familia, ndani ya nchi na nje ya nchi,” alisema Muliro.

Alipoulizwa nchi zipi zinaangaliwa kwa ukaribu katika tukio hilo, alisema hilo ni suala la kiupelelezi, huku akigoma kubainisha upelelezi kwa sasa umefika asilimia ngapi.

“Upelelezi unaenda vizuri, lakini sidhani kama nipo katika nafasi nzuri ya kusema sasa upo kwenye asilimia hii, ila unakwenda vizuri,” alisema Muliro.

Wiki iliyopita, DCI Camilius Wambura alizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza na kudai baada ya kufanya uchunguzi wa kina, wamebaini kuwa Hamza alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga.

Alisema hilo limebainika kupitia uchunguzi wao uliofanyika kwa kuzingatia mambo matatu ambayo ni kutaka kutambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma kufanya tukio lile na kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.

“Na katika uchunguzi huu, polisi ilibaini Hamza alikuwa akiishi kisiri huku akiwa amegubikwa na viashiria vyote vya ugaidi,” alidai Wambura.

“Amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao inayoonyesha matendo hayo na magaidi wengi hujifunza kupitia mitandao hiyo.”

Hata hivyo, Wambura pia alikanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kwamba Hamza aliwashambulia askari hao kwa sababu walimdhulumu madini yake na kusema katika uchunguzi huo, wamebaini Hamza hakuwa na madini wala fedha.

“Hakuwa katika nafasi yoyote ya kumiliki madini wala pesa, mbali ya kwamba watu wengi wameongea kuwa alikuwa anamiliki migodi ya madini kule Chunya na maeneo ya Makongolosi.

Uchunguzi wetu umebaini hali hiyo ya maisha ilikwisha simama muda mrefu,” alisema.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Tatu Mohammed na Bakari Kiango