Jicho letu mahakamani: Jina la Zombe kwenye vielelezo lazua mvutano (50)

Jicho letu mahakamani: Jina la Zombe kwenye vielelezo lazua mvutano (50)

Muktasari:

  • Jana katika mfululizo wa simulizi kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi tuliona shahidi wa Jamhuri akitoa majibu tata kuhusu matokeo ya sampuli ya damu iliyochukuliwa sehemu yalipofanyika mauaji na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.

Jana katika mfululizo wa simulizi kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi tuliona shahidi wa Jamhuri akitoa majibu tata kuhusu matokeo ya sampuli ya damu iliyochukuliwa sehemu yalipofanyika mauaji na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.

Leo tunaendelea na shahidi wa 34 katika kesi hiyo ambayo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na askari wenzake 12 walishtakiwa kwa mauaji ya makusudi ya Sabinus Chigumbi na mdogo wake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha, Juma Ndugu.

Walidaiwa kuwapiga risasi shingoni na sehemu nyingine za miili yao baada ya kuwakamata na kuwapeleka katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam usiku wa Januari 14, 2006, saa chache baada ya kuwakamata eneo la Sinza Palestina, wakiwahusisha na uporaji wa pesa katika gari la kampuni ya Bidco. Endelea…

Mvutano mkali wa kisheria uliibuka katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Septemba 22, 2008, na kuvuta hisia za wasikilizaji wa kesi hiyo baada ya shahidi wa 34 wa Jamhuri, Sajenti Ally Nkya kuiomba mahakama ipokee mkanda wa picha jongefu (CD) alioupa jina la Zombe ili uwe kielelezo katika kesi hiyo.

Sajenti Nkya alitoka Makao Makuu ya Upelelezi (CID-HQs) na alikuwa mpigapicha za video, za mnato na mtaalamu wa alama za vidole.

Ndiye aliyepiga picha hizo katika maeneo mbalimbali yaliyotajwa kuhusishwa katika matukio ya uhalifu uliosababisha kesi hiyo, Januari 22, 2006.

Wakili wa Zombe, Jerome Msemwa ndiye aliyeibua mvutano huo baada ya kuweka pingamizi la kupokelewa picha hizo mahakamani akidai upande wa utetezi walikuwa hawajui kilichokuwamo ndani ya CD hiyo.

Pia alihoji sababu ya shahidi kuiita CD hiyo kwa jina la mteja wake baada ya kuzipiga Februari 22, 2006 wakati Zombe alikuwa bado hajashitakiwa katika kesi hiyo.

Msemwa alidai kuwa Zombe alihusishwa na kesi hiyo mwezi Juni, 2006 hivyo akahoji ilikuwaje shahidi akaziandika kwa jina la raia huru na ofisa wa polisi.

Wakati mvutano huo ukiendelea, Zombe alimwita wakili wake (Msemwa) na kumnong’oneza jambo.

Baada ya kunong’onezwa na mteja wake, Msemwa akaendelea: “Kwa hiyo inaonekana huko mwanzo kulikuwa na mbinu kwamba ni lazima Zombe ashtakiwe.”

Msemwa aliieleza mahakama kuwa picha hizo hazikuwahi kuoneshwa katika hatua ya uchunguzi wa awali wa kesi hiyo (Preliminary Inquiry) katika mahakama ya chini (Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu).

Hivyo aliiomba mahakama hiyo isizipokee picha hizo na akaungwa mkono na mawakili wengine wa utetezi.

Kwa upande wake, wakili Gaudioz Ishengoma aliiomba mahakama iamuru CD hiyo ioneshwe kuona kilichomo, akidai kuwa hakuwahi kupewa mkanda huo katika hatua ya ufungaji na uhamishaji wa kesi hiyo kutoka mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.

Ishengoma alidai kuwa inawezekana picha hizo zilitajwa katika hatua hiyo, lakini akasisitiza kuwa ni vema waone kilichomo kama ni sahihi.

Wakili Majura Magafu naye alisisitiza kuwa CD hizo hazikuoneshwa ili kujua kilichomo ndani wala kuzizungumzia tu katika hatua ya usikilizwaji wa awali.

“Kwa hiyo kwa matakwa ya kisheria si sahihi kuleta CD hiyo hapa na kusema ipokelewe iwe sehemu ya ushahidi,” alisisitiza Magafu.

Naye wakili Rongino Myovela alisisitiza kuwa hawajui kilichomo ndani ya CD hiyo na kwamba upande wa mashtaka ulipaswa kuandaa na kuzionesha ili kuona kilichomo na haitakuwa sahihi kwa mahakama kuzipokea kwani hazikuwahi hata kutajwa tu kwenye uchunguzi wa awali.

Wakili Denis Msafiri alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi ni lazima nyaraka yoyote inayowasilishwa mahakamani itajwe na kuangaliwa wakati wa uchunguzi wa awali.

“Hii CD haikuorodheshwa kwenye commital. Hata siku ya preliminary hearing (usikilizwaji wa awali) haikuzungumziwa. Kwa hiyo, tunaomba uamuzi wa mahakama uliotumika kukataa picha za still (mnato) kwa shahidi wa 32 kuamua hili,” alidai Msafiri.

Akijibu mapingamizi hayo, mwendesha mashtaka, Angaza Mwipopo, alidai kuwa upande wa mashtaka wako tayari kuionesha mahakama hiyo.

Kuhusu hoja ya CD hiyo kupewa jina la Zombe, Mwipopo alisema CD hiyo haikuandikwa mtuhumiwa bali iliandikwa ‘Zombe, AM’ na kwamba yeye mwenyewe anajua sababu zake, huku akisema kuwa labda ni kwa sababu (Zombe) alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum).

Mwipopo alikiri kuwa kweli picha hizo hazikutajwa kwenye PI (Kisutu) na kwenye PH (usikilizwaji wa awali Mahakama Kuu), lakini akasema kuwa kwenye PI maelezo ya shahidi huyo yalisomwa ambamo yalieleza kuwa alipiga picha hizo za video.

Aliongeza kuwa ilikuwa ni vigumu kuwapa upande wa utetezi nakala ya picha jongefu na hata kuzionesha mahakamani na kuongeza kuwa maelezo ya shahidi huyo yaliyosomwa mahakamani yalitosha kuaminisha kuwa zipo.

Maelezo hayo ya Mwipopo hayakuwaridhisha mawakili wa utetezi ambao waliendelea kuipinga CD hiyo na wakaiomba mahakama izingatie kifungu cha 246 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kuamua mvutano huo.

Kwa upande wake, Msemwa alisisitiza kuwa bado wanapinga kupokelewa picha hizo kwa kuwa kwenye hatua ya usikilizwaji wa awali hazikuzungumzwa, akisema hata kama isingewezekana kuzichezesha kuona kilichomo, basi zingeorodheshwa.

“Hii ndio mara ya kwanza kuziona na kutajwa. Kama awali zilifanywa siri basi iendelee kuwa siri,” alisisitiza Msemwa.

Kwa mara nyingine Zombe alimwita wakili wake. Zamu hii alimpa kipande cha karatasi kilichoandikwa ujumbe.

Haikuweza kufahamika Zombe alikuwa ameandika ujumbe gani, lakini baada ya kumkabidhi wakili wake kikaratasi hicho na wakili wake kurudi kwenye nafasi yake, Zombe alionekana kumshinikiza kwa ishara wakili wake afanye jambo kuhusu ujumbe huo.

Msemwa aliendelea kuhoji kwa nini shahidi atumie jina la Zombe kwenye kielelezo hicho wakati Zombe alikuwa hajakamatwa, akidai ‘ni dhahiri kuwa kulikuwa na mpango kuwa Zombe ni lazima tu aingie kwenye kesi hii.’

Wakili Ishengoma naye aliomba CD hiyo isipokewe kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutilia maanani matakwa ya kifungu hicho cha 246 cha CPA.

Alieleza kuwa kifungu hicho kinataka mshitakiwa aelezwe aina ya kesi/shitaka analoshitakiwa nalo na kinataka pia apewe taarifa zote (vikiwamo vielelezo) vitakavyotumika na Jamhuri ili kumpa nafasi ya kuandaa utetezi wake.

“Kutajwa tu kwenye statement (maelezo) ya shahidi haitoshi. Najua kuna amendment (marekebisho) kwenye kipengele cha electronic evidence (ushahidi wa kielektroniki), lakini haituzuii kujua in advance (mapema) na kuandaa utetezi wetu,” alisema Ishengoma.

Naye Magafu alipinga hoja ya Mwipopo kuhusu ugumu wa kuwapatia nakala ya CD hiyo akisema kuwa nakala hiyo inaweza kuzalisha nakala nyingine nyingi tu na kwamba katika maelezo ya shahidi huyo hizo picha zenyewe zimetajwa kwenye mstari mmoja tu.

“Walikuwa na nafasi ya kuleta TV (televisheni) tukaiona. Hata wewe Mheshimiwa Jaji ukiikubali utaomba walete TV kuangalia kilichomo. Kwa hiyo Mheshimwa Jaji bado tuna-maintain (sisitiza) kuwa si sahihi kielelezo hiki kupokewa,” alisisitiza.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Massati alikubaliana na upande wa utetezi, akisema kuwa CD hiyo haiwezi kupokewa mahakamani kama kielelezo kwa kuwa haijakidhi masharti ya kisheria.

Kufuatia uamuzi huo ambao hata upande wa mashtaka ulikubaliana nao, Jaji Massati aliahirisha kesi hiyo hadi siku iliyofuata ambapo shahidi wa 34 alihojiwa na upande wa utetezi.

Nini atakisema shahidi huyo? kesho usikose kupata nakala ya gazeti la Mwananchi kujua kesi ilivyoendelea.