Jicho letu mahakamani: Wakili alivyowapambania washtakiwa waliotoboa siri ya mauaji-58

Jicho letu mahakamani: Wakili alivyowapambania washtakiwa waliotoboa siri ya mauaji-58

Muktasari:

  • Katika sehemu ya 57 ya simulizi ya Kesi ya Zombe, tuliona jinsi wakili Majura Magafu alivyochambua udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka akidai kuwa ni wa kutunga umeacha utata ambao unawafanya washtakiwa washindwe kujua wanajitetea kwa lipi.

Katika sehemu ya 57 ya simulizi ya Kesi ya Zombe, tuliona jinsi wakili Majura Magafu alivyochambua udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka akidai kuwa ni wa kutunga umeacha utata ambao unawafanya washtakiwa washindwe kujua wanajitetea kwa lipi.

Hayo yote yalikuwa ni katika namna ya kuishawishi Mahakama ione kuwa wateja wake (washtakiwa aliokuwa akiwatetea) hawakuwa na kesi ya kujibu akidai upande wa mashtaka ulikuwa umeshindwa kuwasilisha ushahidi uliokuwa ukiwagusa kiasi cha kulazimika kujitetea, na kwa sababu hiyo akaiomba Mahakama iwaachie huru.

Ingawa alikuwa akiwatetea washtakiwa wanane, lakini hoja zake na hasa katika hitimisho ziliwajumuisha washtakiwa wote.

Hii ni Simulizi ya kina kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na askari polisi 11.

Washtakiwa hao walidaiwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini watatu kutoka Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, Sabinus Sabinu Chigumbi maarufu kama Jongo, mdogo wake Ephraim Chigumbi na Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi wa Manzese Dar es Salama, aliyekuwa akiwaendesha.

Walidaiwa kuwapiga risasi katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2006, baada ya kuwatia mbaroni Sinza Palestina, nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, walipokuwa wamempelekea mkewe pesa, wakihusishwa na uporaji wa pesa katika gari la kampuni ya Bidco.

Baada ya kusikiliza hoja za wakili Magafu kwa niaba ya washtakiwa wanane, leo tunaendelea na hoja za mawakili wa washtakiwa watatu wa mwisho. Endelea...


Washtakiwa hawa ni pamoja washtakiwa wawili waliojisalimisha na kufichua ukweli wa mauaji hayo, Koplo Rashid Lema mshtakiwa wa 11 na Koplo Rajabu Bakari, mshtakiwa wa 12, waliokuwa wakitetewa na Wakili Denis Msafiri.

Lakini pia tutasikliza hoja za mshtakiwa wa 13, Koplo Festus Gwabisabi kupitia kwa wakili wake Rongino Myovela. Je, katika hoja zao mawakili hao walisema nini katika kujaribu kuwanusuru wateja wao?

Katika hoja zake kwa niaba ya washtakiwa wa 11 na wa 12, Wakili Denis Msafiri kama ilivyokuwa kwa mawakili wa washtakiwa wengine, naye alidai wateja wake hao hawakuwa na kesi ya kujibu akidai upande wa mashtaka haukuweza kuleta ushahidi uliothibitisha bila kuacha mashaka tuhuma dhidi yao.

Akirejea ushahidi wa upande wa mashtaka, Wakili Msafiri alisema kwa msisitizo: “Kwa ushahidi huu sioni kama upande wa mashaka umeweza kuthibitisha bila kuacha mashaka tuhuma dhidi ya mshtakiwa wa 11 na wa 12.”, alidai Wakili Msafiri.

Alidai ingawa upande wa mashtaka umetumia maelezo yao, yaani maelezo ya onyo waliyoyatoa na kuandikwa mbele ya askari polisi na maelezo ya ungano mbele ya mlinzi wa amani, lakini bado wameshindwa kuthibitika kama kweli walikiri kuhusika katika mauaji hayo.

Huku akinukuu kifungu cha 203 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code – PC), wakili Msafiri alisisitiza upande wa mashtaka kupitia kwa mashahidi wake wote 37, haukuweza kuthibitisha washtakiwa hao wawili ndo waliotenda kitendo kilichosbabisha kifo cha mmoja wa watu hao au wote.

Hivyo, wakili Msafiri alidai jambo pekee ambao washtakiwa hao katika maelezo yao ni kwamba walifika msitu wa Pande mahali mauaji hayo yalikofanyika na kuona kilichotendeka, huku akihoji kama kuona kwao hicho kilichotendeka ndio kosa lao.

“Katika sheria zetu (za nchi) hakuna sheria inayosema mtu akiona kosa linatendeka lazima naye anakuwa ametenda kosa hilo. Lingekuwa kosa kama wajibu wao ungekuwa ni kukaa kimya, ili kosa litendeke, lakini hakuna hakuna ushahidi kama huo,” alisema Wakili Msafiri na kuongeza:

“Ushahidi uliopo (mahakamani) ni kwamba aliyepiga risasi ni Ditekvitu Koplo Saad ambaye hayupo hapa mahakamani kwenye kesi na ndiye angekuwa principal offender (mhalifu mkuu). Kwa kuwa hayupo upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha mashtaka.”

Alidai shahidi wa 30, 31, 35 na 36 wa upande wa mashtaka katika ushahidi wao hakuna mahali wanaposema mshtakiwa wa 11 na wa 12 walikiri kutenda kosa hilo.

Wakili Msafiri alidai kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa 31 lilikuwa ni agizo la Rais, (kupitia tume aliyoiunda kuchunguza ukweli wa mauaji hayo iliyoongozwa na Jaji Mussa Kipenka) kuwa washtakiwe na kwamba hiyo hata kama kusingekuwa na ushahidi wasingepinga maana lilikuwa ni agizo la mkuu wa nchi.

“Maelezo yao hauafikii kiwango cha kusema walikiri kosa kama sheria inavyosema. Prosecution (upande wa mashtaka) walileta ushahidi mkanganyiko kama silaha ya mshtakiwa wa 11 ilitumika (siku hiyo ya tukio) au la,” alidai wakili Msafiri.

Alifafanua shahidi wa 15 alieleza mshtakiwa huyo alipewa bunduki na risasi 30 na akazirejesha zote kamili na kwamba baadaye shahidi huyo alidai alifanya marekebisho kwenye taarifa ya matumizi ya silaha kwa agizo la mkuu wake (mshtakiwa wa pili- SP Bageni), ili kuonyesha kuwa risasi hizo zilitumika.

Wakili Msafiri pia alidai taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha vifo vya wachimba madini hao iliacha mashaka akidai kuna mambo mengi shahidi ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi huo hakuvijaza kama sheria inavyotaka.

“Hii italeta hoja nyingine kuwa nyaraka hizo (ripoti ya uchunguzi) zisikubaliwe au zikubaliwe zisipokubaliwa, ni hoja nyingine kuwa upande wa mashtaka wameshindwa kuleta uthibitisho kulikuwa na vifo, maana uthibitisho ni ripoti na kama ripoti haipo, basi hilo ni jambo lingine,” alisisitiza Wakili Msafiri na kuhitimisha.

“Hivyo Mheshimiwa Jaji na Waungwana Wazee wa Baraza, naiomba Mahakama yako ifikia uamuzi kuwa mshtakiwa wa 11 na wa 12 hakuna ushahidi wa kuwataka kujitetea na hivyo waachiliwe huru.

Kwa upande wake, Wakili Rongino Myovela kwa niaba ya mshtakiwa wa nane, Koplo Felix Sanduy Cedrick na wa 13, Koplo Gwabisabi katika hoja zake alidai kwa mazingira ya kesi hiyo ilitarajiwa upande wa mashtaka ungewasilisha ushahidi wa mashahidi walioshuhudia matukio yote.

Alidai hatua ya utambuzi wa watuhumiwa (gwaride la utambuzi wa watuhumiwa waliohusika katika matukio hayo) ilikuwa ni muhimu na haijulikani ni kwa nini upande wa mashtaka haukufanya hivyo.

Wakili Myovela alidai ushahidi uko wazi kuwa mshtakiwa wa nane hakushiriki katika tukio hilo la mauaji kwa kuwa ushahidi wa daktari aliyefanya uchunguzi wa chanzo cha vifo hivyo unaonyesha kuwa vilitokana na majeraha ya risasi, lakini mshtakiwa wa nane siku hiyo ushahidi umeonyesha hakuwa na silaha.

Kuhusu mshtakiwa wa 13, siku hiyo ya tukio ushahidi wa upande wa mashtaka ulinyesha alipewa silaha aina ya bastola na risasi nane na alirejesha risasi zote nane zikiwa kamili.

“Hata statement (maelezo ya maandishi) za mshtakiwa wa 11 na wa 12 hazijawataja mshtakiwa wa nane na wa 13 kama walikuwa kwenye eneo la tukio la mauaji,” alidai Wakili Myovela na kusisitiza: “Prosecution (upande wa mashtaka) walitakiwa kuthibitisha mshtakiwa wa nane na wa 13 walihusika katika mauaji. Kwa kuwa wameshindwa, basi naoimba Mahakama iwaone hawana hatia na hawastahili kusimama kujibu mashtaka.”

Itaendelea kesho