Jinsi wafugaji wilayani Mbulu wanavyodhibiti magonjwa ya milipuko

Muktasari:
Wafugaji hao kupitia mikutano yao ya vijiji wametunga sheria ya kutoza faini ya Sh30,000 kwa mfugaji ambaye atashindwa kupeleka mifugo yake kwenye josho.
Mbulu. Wafugaji wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara wamefanikiwa kudhibiti magonjwa ya milipuko ya mifugo kutokana na kujenga utaratibu wa kuipeleka kwenye majosho.
Katika kuhakikisha wafugaji wote wanashiriki kuogesha mifugo yao kuingia na magonjwa ya milipuko, wametunga sheria ndogo kwa kuwatoza faini ya Sh30,000 ambao hawatapeleka mifugo yao kuogeshwa.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga amesema wafugaji wa eneo hilo wanashiriki kwa mwamko mkubwa kuhakikisha mifugo inaogeshwa kwenye majosho.
Kamoga amesema Serikali imewezesha uogeshaji wa mifugo kwa kuweka majosho na dawa na wafugaji hao wamejiwekea sheria ndogo vijijini kwa kutoza fedha wasiopeleka mifugo yao kupata dawa.
“Huko vijijini kupitia mikutano mikuu ya vijiji, wananchi wamejiwekea wenyewe sheria ndogo ya kutozana faini kwa kila mfugaji ambaye hatashiriki kupeleka mifugo kwenye majosho hayo,” amesema.
Amesema kupitia mikutano ya vijiji walipitisha sheria ndogo kwa kila mfugaji ambaye atakiuka suala hilo atalipa faini ya Sh30,000.
“Hata wafugaji wenyewe hivi sasa wanakiri kuwa tangu shughuli za uogeshaji mifugo kwenye majosho kuanza wameacha kuwasumbua wataalamu wa mifugo kwani magonjwa yamepungua,” amesema Kamoga.
Mwenyekiti wa wafugaji wa wilaya ya Mbulu, Baraka Gidam amesema wanaishukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa dawa za mifugo yao, hivyo watahakikisha wafugaji wanatumia fursa hiyo.
Ofisa mifugo wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mosses Nduligu amesema suala la kuboresha majosho na kuweka dawa inalenga kulinda afya za mifugo na itakuwa inaogeshwa mara kwa mara.
Nduligu amesema mifugo hupata magonjwa mbalimbali ikiwemo ndigana kali, hivyo kupitia majosho hayo wafugaji watanufaika zaidi.