JKCI yaweka kambi matibabu ya moyo Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas (wapili kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara, Herbet Masigati(watatu kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya (wakwanza kushoto) wakisalimiana na wagonjwa katika Hospitali ya Kanda ya Kusini wakati wa utolewaji wa huduma za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Florence Sanawa
Muktasari:
Jopo la madaktari 15 kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendesha kambi ya siku tatu kwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya kanda ya Kusini Mtwara.
Mtwara.Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeweka kambi ya siku tatu kwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya kanda ya Kusini, ambapo tayari wameshaona zaidi ya wagonjwa 160.
Akizungunza hospitalini hapo leo Novemba 29, Mkurugenzi wa tiba wa taasisi hiyo, Dk Tatizo Waane amesema kuwa mpaka sasa wagonjwa 70 wameshafanyiwa vipimo vya juu vya magonjwa ya moyo kati ya 160 walioonwa.
“Mbali na vipimo pia tunakusanya taarifa kuhusu magonjwa ya moyo na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ili kusaidia Serikali kwaajli ya mikakati mbalimbali ya huduma za afya ili kujua kiwango cha magonjwa kilipo aina gani watu gani wanaathirika nini kifanyike kupunguza athari hizo,” alisema Waane
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas amesema kuwa serikali inafanya jitihada za kuboresha afya, ambapo tayari kuna hosptali ya Kanda na vifaa vilivyogharimu Sh23 bilioni.
“Matibabu haya yanagharimu fedha nyingi sio rahisi mwananchi kuwa na pesa za kuweza kumudu matibabu ya kibingwa ni vema wananchi wakakata bima ya afya ili ziweze kuwasaidia kwa urahisi kupata hduuma hizo.
“Hosptilai hii inasaidia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na nchi za jirani ikiwmeo Comoro na Msumbiji,” amesema Kanali Abbas.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Herbert Masigati amesema kuwa amepokea timu ya watalaamu 15 wa magonjwa ya moyo wapo kwa siku tatu.
“Wagonjwa ni wengi tunaomba waongeze muda na waendele kututembelea tulianza na timu ya moi leo hii tunayo hii, tunaomba siku ziongezwe ili watu wapate huduma kwa wingi zaidi.
Ametaja vifaa vinavyowezesha kazi hiyo kuwa pamoja na radiologia, Ultra Sound, Digital X-ray, MRI na CT-scan na vifaa vya dharura na chumba cha uangalizi maaluma, ambavyo amesema vimegharimu zaidi ya Sh1.5 bilioni.