JKT yatangaza nafasi mafunzo ya kujitolea

Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena.
Muktasari:
- Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele ametangaza nafasi za mafunzo ya jeshi hilo kwa kujitolea kwa mwaka 2023 huku akiwataka vijana wenye sifa kujitokeza kuomba fursa hiyo.
Chamwino. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limewataka vijana wanaomba kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2023, kuepuka kuingia katika mtego wa matapeli wanaoomba rushwa.
Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 25, 2023; wakati akitangaza nafasi hizo kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele.
“Nafasi zinazotolewa haziuzwi, hivyo umma wa Watanzania, wazazi pamoja na walezi, wasije wakaingia katika mtego wa kutapeliwa, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, anawaalika vijana wote ambao wanasifa waende kwa ajili ya kuzitafuta nafasi hizo,” amesema.
Amesema vijana wataochaguliwa watakwenda katika makambi bila kutoa malipo ya aina yoyote ya fedha.
Aidha, amesema kijana atakayepatikana na nyaraka za kughushi atachukuliwa hatua kali za kisheria kulinganana taratibu zilizopo.
Brigedia Jenerali Mabena amesema utaratibu wa vijana kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo, unaratibiwa na mkoa, wilaya ambako mwombaji anaishi.
“Vijana wenye taaluma za uhandisi wa ujenzi, ufugaji, umwagiliaji, uvuvi, saikolojia na wanyamapori wanashauriwa kujitokeza kwa wingi kupitia mikoa yao,” amesema.
Brigedia Jenerali Mabena amesema maandalizi ya vijana kujiunga na mafunzo hayo kwa kujitolea yataanza Agosti 28, 2023 kwa mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.
Amesema vijana watakaoteuliwa watatakiwa kuripoti kwenye makambi ya JKT kuanzia Septemba 26 hadi 29 mwaka huu.
Amesema sifa za mwombaji na maelekezo ya vifaa vinapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni WWW.jkt.go.tz