Jokate ataja maeneo manne watakayotumia mgawo Sh5 bilioni

Jokate ataja maeneo manne watakayotumia mgawo Sh5 bilioni

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo ametaja maeneo manne watakayotumia mgawo wa Sh5 bilioni walizopewa na Serikali kuwa pamoja na elimu, afya, biashara na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo ametaja maeneo manne watakayotumia mgawo wa Sh5 bilioni walizopewa na Serikali kuwa pamoja na elimu, afya, biashara na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Fedha hizo ni sehemu ya Sh1.3 trilioni zilizotolewa na Serikali hivi karibuni.

DC Jokate ameyasema hayo leo Oktoba 13, wakati akizungumza na waandishi kuhusu kuanzisha kampeni itakayoitwa 'Temeke Gulio'.

Amesema katika fedha hizo Sh3.14 bilioni zitakwenda kujenga madarasa 157 pamoja na kununua madawati ambapo wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wataingia kwa awamu moja.

Amebainisha kuwa Sh250 milioni zitapelekwa kujenga kituo cha afya Toangoma, Sh300 milioni kwaajili ya ujenzi wa jengo la huduma za dharura, Sh700 milioni ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Kibasila na fedha zingine zitapelekwa kwenye kampeni ya kutoa elimu kuhusu Uviko 19.

"Tunamshukuru Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuweza kutupatia fedha hizi, ambazo zitasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika Wilaya yetu," amesema Jokate.

Akizungumzia kuhusu kampeni ya 'Temeke Gulio', DC Jokate amesema lengo lake ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao wadogo kuweza kuuza bidhaa zao.

"Ndugu wafanyabiashara gulio hili linakwenda kutoa fursa kwenu wafanyabiashara na tunatarajia kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla atazindua rasmi hivyo tushirikishe kwa ajili ya maendeleo ya Temeke yetu," alisema Mwegelo.

Amesema litahusisha masoko 20 yaliyotengwa na Halmashauri hiyo kwa wafanyabiashara hao yakiwemo yaliyojengwa katika Mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elihuruma Mabelya amemhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa atahakikisha fedha zote zilizotolewa na Rais Samia zitafanya kazi zilizotarajiwa na haitaliwa hata senti moja.

Naye katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya hiyo, Daniel Sayi amesema mambo yote yanayofanyika ni utekelezaji wa Ilani ya ccm hivyo wao kama viongozi kazi kubwa nikuangalia na kusimamia ahadi zilizohaidiwa na viongozi kama zinatekelezwa ipasavyo.

Meneja wa benki NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard amesema katika kampeni hiyo watawawezesha wajasiriamali kupata elimu kuhusu masuala hayo, namna ya kukabiliana na soko la ushindani na kuwawezesha kupata mikopo kwa haraka na masharti nafuu.