Joto kali linavyotesa Ulaya, watu 2,000 wafariki dunia Ufaransa
Watu wakiwa ndani ya maji nchini Ufaransa kutokana na joto kali.
Muktasari:
- Mnamo Juni 24, Ufaransa ilishuhudia siku yenye joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa wastani nchini humo.
Dar es Salaam. Ufaransa imeripoti vifo 2,025 katika wiki ya mwisho wa Juni, kufuatia joto kali lililokumba nchi hiyo na sehemu nyingine za Ulaya, huku wataalamu wakionya hali ya hewa yenye joto kali itaendelea kushuhudiwa siku zijazo.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya ya Umma la Ufaransa zinaonyesha idadi ya vifo kati ya Juni 22 na 28 iliongezeka kwa asilimia 29 ikilinganishwa na wiki iliyotangulia, eneo la Paris pekee, vifo viliongezeka kwa asilimia 62.
Kulingana na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) leo Julai 3,2026 Waziri wa Afya wa Ufaransa, Stéphanie Rist, amesema ongezeko hilo limeonekana zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 45 na kuendelea, akieleza idadi halisi ya vifo huenda ikawa kubwa zaidi kuliko ilivyorekodiwa katika taarifa za awali.
Juni 24, Ufaransa ilishuhudia siku yenye joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa wastani nchini humo, huku halijoto ikifikia karibu nyuzi 41 za Selsiasi jijini Paris na zaidi ya nusu ya maeneo ya nchi hiyo kuwekwa chini ya tahadhari nyekundu kutokana na joto kali.
Mbali na vifo vinavyohusishwa moja kwa moja na joto, mamlaka za Ufaransa zimesema watu 72 wamefariki dunia kwa kuzama kwenye maji tangu Juni 18, tukio linalohusishwa na ongezeko la watu waliokwenda kuogelea ili kujinusuru na joto kali.
Athari za wimbi hilo la joto zimeonekana pia katika mataifa mengine ya Ulaya.
Ubelgiji iliripoti vifo 1,222, sawa na ongezeko la asilimia 39, huku karibu nusu ya waliofariki wakiwa na umri wa miaka 85 na zaidi. Nchini Uholanzi, mamlaka zimeripoti vifo 480, wengi wao wakiwa na umri wa miaka 80 na kuendelea.
Wakati huohuo, wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa joto kali linatarajiwa kurejea mwishoni mwa wiki katika maeneo mengi ya Ulaya.
Kusini mwa Ufaransa kunatarajiwa kushuhudia halijoto ya hadi nyuzi 40 za Selsiasi, huku miji ya Bordeaux, Toulouse na Agen ikitarajiwa kufikia kati ya nyuzi 36 na 37.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka ya hali ya hewa ya Ufaransa imetoa tahadhari kuhusu hatari kubwa ya moto wa misitu katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Waziri Mkuu, Sebastien Lecornu, amesema tangu kuanza kwa msimu wa joto, matukio ya moto karibu 7,000 yameteketeza zaidi ya hekta 8,700 za misitu na uoto wa asili.
Moto mkubwa uliotokea katika mji wa Sainte-Marie-la-Mer ulisababisha watu karibu 3,000 kuhamishwa makazi yao baada ya kusambaa hadi eneo la Canet-en-Roussillon.
Nchini Ureno, Serikali imetangaza hali ya tahadhari itakayodumu hadi usiku wa manane wa Jumanne kutokana na utabiri wa halijoto kuzidi nyuzi 40 za Selsiasi katika baadhi ya maeneo, huku joto la usiku likitarajiwa kubaki juu ya nyuzi 25.
Nchini Hispania, maeneo ya kusini-magharibi yamewekwa katika tahadhari ya kiwango cha machungwa baada ya utabiri kuonesha halijoto inaweza kufikia nyuzi 40 za Selsiasi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa huduma ya Copernicus ya Umoja wa Ulaya, Ulaya ndiyo bara linalopata ongezeko kubwa zaidi la joto duniani, likiongezeka kwa kasi mara mbili ya wastani wa dunia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hali hiyo imeongeza matukio ya mawimbi ya joto wakati wa kiangazi, uhaba wa maji na ongezeko la moto wa misitu, huku wataalamu wakionya kuwa matukio hayo yanatarajiwa kuendelea kujirudia ikiwa hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hazitachukuliwa.