Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TMA yataja sababu baridi kali, mikoa minne kuathirika zaidi

Muktasari:

  • Wananchi wa mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Kilimanjaro wameanza kushuhudia hali hiyo kwa viwango tofauti, huku baadhi wakieleza kuwa baridi ya mwaka huu ni kali zaidi.



Dar/Mikoani. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitaja sababu za kuongezeka kwa baridi nchini mwezi huu wa Julai, wananchi wa mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Kilimanjaro wameanza kushuhudia hali hiyo kwa viwango tofauti, huku baadhi wakieleza kuwa baridi ya mwaka huu ni kali zaidi kulinganisha na mwaka uliopita.

Mchambuzi wa Hali ya Hewa wa TMA, Ramadhani Omari, anasema kupungua kwa viwango vya joto kunasababishwa na mifumo ya upepo unaovuma kutoka kusini mwa Afrika.

Anasema upepo huo umebeba hewa ya ubaridi, sambamba na jua kuwa upande wa kaskazini zaidi mwa Ikweta, hali inayofanya maeneo ya kusini na nyanda za juu kupokea kiwango kikubwa cha baridi kati ya Juni hadi Agosti.

Anasema mwezi huu (Julai) baridi itaongezeka zaidi, huku mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Songwe litakuwa kali zaidi, baadhi ya maeneo ikitarajiwa kufikia nyuzi joto tano au chini ya hapo.

Omari anasema tayari kituo cha hali ya hewa cha Uyole mkoani Mbeya kimesharekodi nyuzi joto tatu hadi nne kati ya Juni 28 na 29, 2026, hali inayoashiria mwezi huu kushuka zaidi.

Kwa maeneo ya Ukanda wa Pwani yanayokuwa na joto, ikiwamo Dar es Salaam, yataendelea kuwa na baridi, ingawa haitafikia kiwango kinachoshuhudiwa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Anasema kwa kawaida Dar es Salaam hupata nyuzi joto 24 hadi 26 nyakati za usiku, kipindi hiki viwango hivyo vimeshuka hadi kati ya nyuzi joto 18 na 20, hali inayowafanya wananchi wengi kuhisi baridi zaidi.

Mbali na hali ya baridi, anasema vipindi vya upepo mkali vitaendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo, ingawa havitarajiwi kuwa vya muda mrefu, na kuwashauri wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.

Pia anashauri wavuvi na watumiaji wa vyombo vya majini kuwa waangalifu wanapokutana na vipindi vya upepo mkali ili kuepusha ajali, na kubainisha kuwa msimu wa baridi utaendelea hadi Agosti, na viwango vya joto vitaanza kupanda taratibu kuanzia Septemba.


Wananchi wanachokisema

Katika mikoa mbalimbali nchini, wananchi wanaeleza adha wanayokumbana nayo kiafya katika msimu huu, huku fursa kwenye biashara za vinywaji vya moto na nguo za baridi ikiongezeka.

Mkoa wa Kilimanjaro, hususan Wilaya ya Rombo, baadhi ya wananchi wanaeleza kushuhudia baridi kali inayoambatana na ukungu mzito pamoja na manyunyu ya mvua nyakati za asubuhi na jioni.

“Hali hii inatukumbusha misimu ya zamani ya baridi kali katika eneo hili,” anasema Jovin Mushi.

Mkoani Njombe, wananchi wanasema hali ya hewa imeendelea kuwa ya baridi kali tangu Juni, hasa katika Wilaya ya Makete.

Neema John anasema nyakati za asubuhi wilayani humo jua huchelewa kuchomoza, na kutolea mfano kwamba jana Jumanne, Juni 30, 2026, saa 3:30 asubuhi ilikuwa kama saa 12 asubuhi na ukungu mzito ulitanda kila eneo.

Mkoani Mbeya, Jane Almisi wa Sabasaba anasema baridi ya mwaka huu imekuwa kali zaidi nyakati za jioni, usiku na alfajiri, kama ilivyo kwa mkoa wa Iringa ambao baadhi ya wananchi wanasema hali hiyo ya hewa inachangia midomo kukauka na wakati mwingine kupasuka na kutoa damu.

Japo daktari wa binadamu katika Hospitali ya Sokoni, Iringa, Neema Mwanjole anasema hali ya hewa ya baridi hupunguza unyevunyevu wa ngozi na midomo, jambo linalochangia ukavu na kuchanika kwa midomo, akishauri watu kutumia mafuta maalumu ya kulainisha midomo, kunywa maji ya kutosha pamoja na kula lishe bora.

“Watu wengi hudhani ni tatizo la kawaida la baridi pekee, lakini wakati mwingine linaweza kuhusishwa na upungufu wa maji mwilini au virutubisho muhimu kama vitamini za kundi B, madini ya iron na zinc,” anasema.

Hata hivyo, kwa mama lishe na baba lishe mkoani Iringa, hali ya baridi imekuwa ni fursa kwenye vinywaji vya uji, chai na alkasusu kama ilivyo kwenye biashara ya nguo za baridi.

Mmoja wa wafanyabiashara, Juma Mkwawa anasema wakati wa joto, biashara ya masweta na makoti huuzwa kwa bei ya chini ili kuvutia wanunuzi, lakini kipindi kama hiki cha baridi, bei hupanda maradufu.

“Kipindi cha joto biashara huwa ngumu sana; unakuta sweta ambalo kipindi hiki linauzwa hadi Sh20,000, wakati wa joto linaweza kuuzwa hata Sh2,000 au zaidi kidogo ili tu bidhaa ziende,” anasema Mkwawa.


Madaktari washauri

Daktari bingwa na mbobevu wa magonjwa ya kinga mwili na mzio katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kassim Mapondela, anasema kufanya mazoezi, kula matunda hususani yenye vitamini C kwa wingi, kunywa maji ya kutosha na mboga mboga ni kinga sahihi nyakati za msimu huu wa baridi ambao unachangia kuwepo kwa magonjwa ya mfumo wa hewa.

“Njia kubwa ya kujilinda ni wale wenye mafua makali kutumia barakoa ili kusaidia wasiwaambukize wenzao na kutumia vitakasa mikono mara kwa mara,” anasema.

Daktari mwingine wa binadamu kutoka Hospitali ya Sokoni katika Manispaa ya Iringa, Fabian Mwasabwite anasema hali ya baridi inaweza kusababisha madhara mbalimbali kiafya kwa watoto na watu wazima endapo hawatajikinga ipasavyo kwa kuvaa mavazi mazito kama masweta, makoti na soksi.

“Watoto wadogo na wazee wako kwenye hatari zaidi kipindi cha baridi kwa sababu kinga zao za mwili huwa dhaifu, mtu asipojikinga vizuri anaweza kupata mafua makali, kikohozi, homa pamoja na matatizo ya mfumo wa upumuaji,” anasema Dk Mwasabwite.

Mfamasia, Joseph Kalinga anasema kipindi cha baridi huambatana na ongezeko la wananchi wanaonunua bidhaa za kulainisha midomo, hususan lip balm na petroleum jelly.

Mtaalamu wa lishe mkoani Iringa, Rehema Mwinuka anasema afya ya midomo inahusiana kwa karibu na lishe bora.

Anasema ulaji wa matunda, mboga za majani na vyakula vyenye madini na vitamini mbalimbali husaidia kuimarisha afya ya ngozi na midomo.

“Kipindi cha baridi watu wengi hupunguza unywaji wa maji kwa sababu hawahisi kiu, lakini mwili bado unahitaji maji ya kutosha. Unywaji wa maji na lishe bora ni sehemu muhimu ya kuzuia ukavu wa midomo,” anasema.

Imeandikwa na Imani Makongoro (Dar), Hawa Mathias (Mbeya), Christina Thobias (Iringa), Janeth Mushi (Kilimanjaro) na Seif Jumanne (Njombe).