Joyce Banda asimulia alivyonusurika kuuawa akiwa Makamu wa Rais

Rais mstaafu wa Malawi, Joyce Banda

Muktasari:

Rais mstaafu wa Malawi mama Joyce Banda ameeleza namna, alivyonusurika kuuawa wakati akiwa Makamu wa Rais.


Dar es Salaam.  Rais mstaafu wa Malawi, Joyce Banda ameeleza namna alivyonusurika kuuawa wakati akiwa Makamu wa Rais.

Banda ameeleza hayo leo Desemba 3,2022 wakati wa kongamano la nne la wanawake vijana wa mtandao wa viongozi Afrika lililofanyika visiwani Zanzibar.

Amesema aliwahi kupitia changamoto mbalimbali baada ya kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais kwa kuwa hakukubalika kutokana na kutokuwa maarufu kwani Rais aliyemchagua alimuahidi angemsaidia ili aje kumrithi lakini alibadilisha muelekeo.

  “Aliniambia naweza kuwa Makamu wa Rais kama ningeweza kumpitisha kaka yake, lakini nikamwambia sio sehemu ya majadiliano, nikaanza kukabiliana na changamoto watu wakahitaji mabadiliko na kuanza kufanya maandamano.

 “Kulikuwa na maandamano watu 21 walifariki wasiwasi ulitanda na mimi kutaka kuuawa baada ya lori kugonga gari langu upande niliokuwa nimekaa, kwa bahati nzuri wanausalama walikuwa wameshajua linalotaka kutokea wakaniweka pembeni,”ameeleza  Banda.

Amebainisha kuwa alikuwa ameshatolewa kauli za vitisho, endapo akipatikana angemalizwa, ameeleza kuwa taarifa zilipelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

 “Rais wa Ethiopia alikuja Malawi kunisaidia na kuokoa maisha yangu wakati huo nilikuwa siwezi kutoka ndani lakini alikuja hadi Lilongwe na kuagiza magari ya Umoja wa Mataifa kunifuata,”amesimulia.

Amesema alitumia magari hayo kusafiri hadi kwenye mkutano kwa kuwa Rais wa Ethiopia alitaka kusikia changamoto zake, na kutoa maelekezo magari hayo yasiguswe kwa kuwa yamembeba Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa.

 “Nilitaka mfahamu kusaidia viongozi wanawake inavyosaidia, ni lazima tusaidie kwa uwazi zaidi kama tunavyosaidiana miongoni mwetu,”

 Kuhusu biashara amesema uwezeshaji kiuchumi ni suala la msingi kwa ajili ya uwezeshaji wa kisiasa na kijamii kwani yapo mambo mawili yasipotokea mwanamke anaweza kuwa nyuma kimaendeleo.

  “Watu ambao hawakupata kabisa elimu, rasilimali zilipokuwa chache zilikuwa zimeelekezwa kwa wanaume, fursa walioko nazo sasa ni za uchumi na biashara viongozi tunatakiwa kutengeneza fursa kwa wanawake,”