Jussa ahoji namna elimu ya Katiba itakavyotolewa
Dar es Salaam. Mjumbe wa kamati kuu ya ACT-Wazalendo, Ismail Jussa amehoji namna elimu ya Katiba itakavyotolewa na lengo ni kufikia Watanzania wangapi ili kuwa na sifa ya kusema sasa wananchi wanaijua Katiba.
Jussa ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 6, 2023 wakati akichangia kwenye mjadala wa Mwananchi X – Space ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) ukiwa na mada inayosema: “Nini maoni yako kuhusu miaka mitatu ya elimu ya Katiba kwa wananchi?”
Amesema suala la elimu ya Katiba kwa miaka mitatu ni ulaghai unaofanywa na chama tawala na Serikali yake kwa kutaka kuchelewesha mchakato wa Katiba ambao unapigiwa na makundi yote ya wananchi.
“Ukisema ukatoe elimu kwa miaka mitatu, ni kiwango kipi unachotaka ufikie? Hata wanasheria, siyo wote wanajua sheria zote, unakuta huyu amejikita kwenye sheria za jinai, huyu amejikita kwenye sheria za biashara, huyu amejikita kwenye sheria za Katiba na utawala.
“Hata tukifanya utafiti kwa hao wanaoitwa watunga sheria, hebu wafanyiwe utafiti kidogo wapimwe uelewa wao. Lazima tutapata ambao hawaijui Katiba na wapo wanaoijua,” amesema Jussa.
Kada huyo wa ACT Wazalendo kutoka Zanzibar amebainisha hata nchi zenye demokrasia iliyoendelea kama Marekani, huwezi kukuta hata asilimia 30 ya Wamarekani wanaijua Katiba yao.
“Siyo kila mtu anajishughulisha kutaka kujua Katiba yote, anataka kujua masuala machache yanayomuhusu. Kwa hiyo suala la elimu ya Katiba ni kupoteza muda, ni kujaribu kuahirisha jambo hili,” amesema Jusaa.
Amesisitiza kwamba wananchi wenyewe wanatakiwa kuunda Katiba yao, tangu mwaka 1961 baada ya uhuru, hakujawahi kuwa na Katiba iliyotungwa na wananchi, sasa ni wakati wa wananchi kuandika Katiba yao.