Kadinali Polycarp Pengo kutakatifuza kanisa Geita

Kanisa kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita lililofungwa kwa siku 20 baada ya kutiwa kufuru na najisi ya kiimani

Muktasari:

  • Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga na baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wanatarajiwa kushiriki ibada maalum ya kutakatifuza kanisa kuu la kiaskofu jimbo Geita lililokuwa limefungwa kwa siku 20 baada ya kuvamiwa na kuharibiwa vifaa.

Geita. Askofu mstaafu wa kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam Kadinali Polycarp Pengo anatarajiwa kuongoza ibada ya misa takatifu ya kutakatifuza Kanisa kuu la kiaskofu jimbo la Geita katika ibada maalum inayotarajiwa kufanyika Machi 18, 2023 katika kanisa hilo lililopo mjini Geita.

Ibada hiyo inatarajiwa pia kuhudhuriwa na Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Gervas Nyaisonga na maaskofu wasiopungua 10 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na Mwannachi leo Machi 14, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita Flavian Kassala amesema ibada hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, pamoja na waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Ibada hiyo inayotarajiwa kuanza saa 4 asubuhi itahusisha pia maadhimisho ya toba ya malipizi Baraka kutakatifuza kanisa kuu na kurudisha ekarist takatifu ndani ya kanisa hilo.

Amesema ibada hiyo itatanguliwa na maandamano kutoka Parokia jirani ya Bikira Maria wa Fatima iliyopo mjini Geita kuelekea Kanisa kuu la kiaskofu la jimbo hilo.

"Mwadhama Kadinali Pengo ndie ataongoza ibada na maaskofu kadhaa kama 10 akiwemo Rais wa baraza la Maaskofu na viongozi mbalimbali watashiriki ibada hiyo " amesema Askofu Kassala

Kanisa kuu la Kiaskofu jimbo la Geita lilifungwa Februari 27 baada ya kijana mmoja aliyetumbuliwa kwa jila la Elpidius Edward (22) kudaiwa kuvunja kioo cha lango kuu la Kanisa kisha kufanya kufuru eneo la sakramenti ya ekaristi eakatifu na kunajisi utakatifu wa jengo ikiwemo uharibifu wa vifaa vya ibada vyenye thamani ya zaidi ya Sh40 milioni.

Kipindi ambacho Kanisa hilo lilifungwa kwa siku 20 waumini na viongozi waliingia kwenye adhimisho la toba ya malipizi, kusali, kutubu, kupokea sakramenti ya upatanisho na kuomba huruma ya Mungu katika matendo yaliyotendeka kanisani hapo.