Kajala apewa saa 12 kumuomba radhi Mobetto

Tuesday February 16 2021
kajalapic
By Kelvin Kagambo

Dar es Salaam. Mwigizaji Kajala Masanja amepewa saa 12 kukanusha tuhuma alizomtupia mwanamitindo, Hamisa Mobetto kwamba alimkutanisha mwanaye, Paula na msanii Rayvanny siku aliyodai mwanaye huyo alinyeshwa pombe na kurekodiwa video za ngono.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 16, 2021 na mwanasheria wa mwanamitindo huyo, Elia Rioba aliyebainisha kuwa barua hiyo itamfikia Kajala leo.

Kajala ambaye kwa sasa yupo katika mahusiano na msanii Harmonize alitoa tuhuma hizo Jumapili Februari 14, 2021  kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram yenye wafuasi milioni 4.4, na baada ya muda Mobetto alimjibu kupitia ukurasa wake wa Instagram pia.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Rioba amesema barua hiyo ilitakiwa imfikie Kajala tangu jana lakini ilishindikana kwa kuwa hata simu yake ya mkononi haipokelewi.

Amesema baada ya barua kumfikia mwigizaji huyo, anatakiwa kukanusha ndani ya saa 12 na akikaidi, hatua nyingine za kisheria zitafuatwa.

Katika barua hiyo itakayotumwa kwa Kajala kupitia kampuni ya wanasheria ya Mass Attorneys, inaeleza tuhuma za uongo dhidi ya mteja wao kwamba zinaweza  kuumiza nafasi alizonazo katika jamii ikiwa ni pamoja na ubalozi wa kampuni mbalimbali na biashara pamoja na biashara zenye jina lake.

Advertisement

Katika barua hiyo kuna maagizo mengine mawili kwa Kajala ambayo ni kufuta chapisho Instagram kuhusu tuhuma hizo dhidi na pili  kumuandikia mwanamitindo huyo barua ya kumuomba radhi.

kajapic22

Paula (19) ni mtoto wa Kajala aliyezaa na mwandaaji mkongwe wa muziki nchini, Paul Matthysse maarufu P Funk Majani.

Mwananchi Digital imemtafuta Kajala bila mafanikio kwa kuwa simu yake ya mkononi inaita bila majibu.

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital kwa taarifa zaidi

Advertisement